Yobu 19:1-29
Yobu 19:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Yobu akajibu: “Mtaendelea kunitesa mpaka lini, na kunivunjavunja kwa maneno? Mara hizi zote kumi mmenishutumu. Je, hamwoni aibu kunitendea vibaya? Hata kama ingekuwa nimekosa kweli, kosa langu lanihusu mimi mwenyewe. Mnaishusha hadhi yangu mpate kujikuza; mnanilaumu kwa kunyenyekezwa kwangu. Jueni kwamba Mungu amenitendea vibaya, na kuninasa katika wavu wake. Tazama napiga yowe: ‘Dhuluma!’ Lakini sijibiwi. Naita kwa sauti kubwa, lakini sipati haki yangu. Njia yangu ameiziba kwa ukuta ili nisipite amezitia giza njia zangu. Amenivua fahari yangu; ameiondoa taji yangu kichwani. Amenivunja pande zote, nami nimekwisha; tumaini langu amelingoa kama mti. Ameichochea ghadhabu yake dhidi yangu; ameniona kuwa kama adui yake. Majeshi yake yanijia kwa pamoja; yametengeneza njia ya kuja kwangu, yamepiga kambi kuizunguka nyumba yangu. Mungu amewaweka ndugu zangu mbali nami; rafiki zangu wakuu wamenitoroka kabisa. Jamaa zangu na marafiki hawanisaidii tena. Wageni nyumbani mwangu wamenisahau; watumishi wangu wa kike waniona kuwa mgeni. Mimi nimekuwa kwao mtu wasiyemjua. Namwita mtumishi wangu lakini haitikii, ninalazimika kumsihi sana kwa maneno. Nimekuwa kinyaa kwa mke wangu; chukizo kwa ndugu zangu mwenyewe. Hata watoto wadogo hunidharau, mara ninapojitokeza wao hunizomea. “Rafiki zangu wakuu wanachukizwa nami, wale niliokuwa nikiwapenda wamenipa kisogo. Mwili wangu umebakia tu mifupa na ngozi, nimeponea chupuchupu baada ya kupoteza yote. Nioneeni huruma, nioneeni huruma enyi rafiki zangu; maana mkono wa Mungu umenifinya. Kwa nini mnanifuatia kama Mungu? Mbona hamtosheki na mwili wangu? “Laiti maneno yangu yangeandikwa! Laiti yangeandikwa kitabuni! Laiti yangechorwa kwa chuma na risasi juu ya jiwe ili yadumu! Najua wazi Mkombozi wangu anaishi, mwishowe yeye atanipa haki yangu hapahapa duniani. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivyo, nitamwona Mungu kwa macho yangu mwenyewe. Mimi mwenyewe nitakutana naye; mimi mwenyewe na si mwingine nitamwona kwa macho. “Nyinyi mwaweza kujisemea: ‘Tutamfuatia namna gani? Tutapataje kwake kisa cha kumshtaki?’ Lakini tahadharini na adhabu. Chuki yenu yaweza kuwaletea kifo! Mnapaswa kujua: Mungu peke yake ndiye hakimu.”
Yobu 19:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Je! Mtanichukiza nafsi yangu hata lini, Na kunivunjavunja kwa maneno? Mara kumi hizi mmenishutumu; Hamwoni haya kunifanyia mambo magumu. Ingawaje nimekosa, Kosa langu hukaa kwangu mwenyewe. Ikiwa mtajitukuza juu yangu, Na kufanya aibu yangu kuwa hoja juu yangu; Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha, Na kunizingira kwa wavu wake. Tazama, nalia, Udhalimu, lakini sisikiwi; Naulilia msaada, wala hapana hukumu. Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita, Na kutia giza katika mapito yangu. Amenivua utukufu wangu, Na kuiondoa taji kichwani mwangu. Amenibomoa pande zote, nami nimetoweka; Na tumaini langu ameling'oa kama mti. Tena ameziwasha ghadhabu zake juu yangu, Akanihesabia kuwa mmoja katika watesi wake. Majeshi yake husongea pamoja, na kunipandishia njia yao, Na kupiga kambi kuizunguka hema yangu. Amewaweka ndugu zangu mbali nami, Na wanijuao wametengwa nami kabisa. Watu wa ukoo wangu wamekoma, Na marafiki zangu niwapendao wamenisahau. Wakaao nyumbani mwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu kuwa mgeni; Wageni nyumbani mwangu, na vijakazi wangu, wanihesabu kuwa mgeni. Namwita mtumishi wangu, wala haniitikii, Ingawa namsihi kwa kinywa changu. Pumzi zangu zimekuwa kinyaa kwa mke wangu, Nami ni machukizo kwa ndugu zangu. Hata watoto wadogo hunidharau; Nikiondoka, huninena. Marafiki zangu wote wa dhati wanichukia; Na hao niliowapenda wamenigeukia. Mfupa wangu unagandamana na ngozi yangu na nyama yangu, Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu. Nihurumieni, nihurumieni, enyi rafiki zangu, Kwa maana mkono wa Mungu umenigusa. Mbona ninyi mnaniudhi kama Mungu, Wala hamkutosheka na nyama yangu? Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa! Laiti yangeandikwa kitabuni! Yakachorwa katika mwamba milele, Kwa kalamu ya chuma na risasi. Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu! Kama mkisema, Jinsi tutakavyomwudhi! Kwa kuwa shina la jambo hili limeonekana kwake; Uogopeni upanga; Kwa maana adhabu za upanga zina ghadhabu, Mpate kujua ya kwamba hukumu iko.
Yobu 19:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Je! Mtanichukiza nafsi yangu hata lini, Na kunivunja-vunja kwa maneno? Mara kumi hizi mmenishutumu; Hamwoni haya kunifanyia mambo magumu. Ingawaje nimekosa, Kosa langu hukaa kwangu mwenyewe. Kwamba mtajitukuza juu yangu, Na kunena juu yangu shutumu langu; Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha, Na kunizingira kwa wavu wake. Tazama, nalia, Udhalimu, lakini sisikiwi; Naulilia msaada, wala hapana hukumu. Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita, Na kutia giza katika mapito yangu. Amenivua utukufu wangu, Na kuiondoa taji kichwani mwangu. Amenibomoa pande zote, nami nimetoweka; Na tumaini langu ameling’oa kama mti. Tena ameziwasha ghadhabu zake juu yangu, Akanihesabia kuwa mmoja katika watesi wake. Majeshi yake husongea pamoja, na kunipandishia njia yao, Na kupiga marago kuizunguka hema yangu. Amewaweka ndugu zangu mbali nami, Na wanijuao wametengwa nami kabisa. Watu wa mbari yangu wamekoma, Na rafiki zangu niwapendao wamenisahau. Wakaao nyumbani mwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu kuwa mgeni; Mimi ni mgeni machoni pao. Namwita mtumishi wangu, wala haniitikii, Ingawa namsihi kwa kinywa changu. Pumzi zangu ni kama za mgeni kwa mke wangu, Nami ni machukizo kwa ndugu zangu. Hata watoto wadogo hunidharau; Nikiondoka, huninena. Wasiri wangu wote wanichukia; Na hao niliowapenda wamenigeukia. Mfupa wangu unagandamana na ngozi yangu na nyama yangu, Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu. Nihurumieni, nihurumieni, enyi rafiki zangu, Kwa maana mkono wa Mungu umenigusa. Mbona ninyi mnaniudhi kama Mungu, Wala hamkutosheka na nyama yangu? Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa! Laiti yangeandikwa kitabuni! Yakachorwa katika mwamba milele, Kwa kalamu ya chuma na risasi. Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu! Kama mkisema, Jinsi tutakavyomwudhi! Kwa kuwa shina la jambo hili limeonekana kwake; Uogopeni upanga; Kwa maana adhabu za upanga zina ghadhabu, Mpate kujua ya kwamba hukumu iko.
Yobu 19:1-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Ayubu akajibu: “Je, mtaendelea kunitesa hadi lini, na kuniponda kwa maneno yenu? Mara kumi hizi mmenishutumu; bila aibu mnanishambulia. Kama ni kweli nimepotoka, kosa langu ninabaki kuhusika nalo mwenyewe. Kama kweli mngejitukuza wenyewe juu yangu, na kutumia unyonge wangu dhidi yangu, basi jueni kuwa Mungu amenitendea yaliyo mabaya, naye amekokota wavu wake kunizunguka. “Ingawa ninalia, ‘Nimetendewa mabaya!’ sipati jibu; ingawa ninaomba msaada, hakuna haki. Yeye ameizuia njia yangu hivyo siwezi kupita; ameyafunika mapito yangu na giza. Amenivua heshima yangu, na kuniondolea taji kichwani pangu. Amenibomoa kila upande hadi nimeisha; amelingʼoa tegemeo langu kama mti. Hasira yake imewaka juu yangu; amenihesabu kuwa miongoni mwa adui zake. Majeshi yake yananisogelea kwa nguvu; yamenizingira, yamepiga kambi kulizunguka hema langu. “Amewatenga ndugu zangu mbali nami; wale tunaojuana nao wamefarakana nami kabisa. Watu wa jamaa zangu wameenda mbali; rafiki zangu wamenisahau. Wageni wangu na wajakazi wangu wananiona kama mgeni; wananitazama kama mgeni. Namwita mtumishi wangu, wala haitiki, ingawa namwomba kwa kinywa changu mwenyewe. Pumzi ya kinywa changu ni kinyaa kwa mke wangu; nimekuwa chukizo mno kwa ndugu zangu mwenyewe. Hata watoto wadogo hunidhihaki; ninapojitokeza, hunifanyia mzaha. Rafiki zangu wa moyoni wote wananichukia kabisa; wale ninaowapenda wamekuwa kinyume nami. Mimi nimebaki mifupa na ngozi tu; nimeponea nikiwa karibu kufa. “Nihurumieni, rafiki zangu, kuweni na huruma, kwa kuwa mkono wa Mungu umenipiga. Kwa nini mnanifuatia kama Mungu afanyavyo? Hamtosheki kamwe na mwili wangu? “Laiti maneno yangu yangewekwa kwenye kumbukumbu, laiti kwamba yangeandikwa kwenye kitabu, kwamba yangechorwa kwenye risasi kwa kifaa cha chuma, au kuyachonga juu ya mwamba milele! Ninajua kwamba Mkombozi wangu yu hai, naye kwamba mwishoni atasimama juu ya nchi. Nami baada ya ngozi yangu kuharibiwa, bado nikiwa na mwili huu nitamwona Mungu; mimi nitamwona kwa macho yangu mwenyewe: mimi, wala si mwingine. Tazama jinsi moyo wangu unavyomtamani sana! “Mkisema, ‘Tazama tutakavyomwinda, maadamu mzizi wa tatizo uko ndani yake,’ ninyi wenyewe uogopeni upanga, kwa kuwa ghadhabu italeta adhabu kwa upanga, nanyi ndipo mtajua kuwa kuna hukumu.”