Yobu 11:1-20
Yobu 11:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Sofari, Mnaamathi, akamjibu Yobu: “Je, wingi huu wa maneno uachwe tu bila kujibiwa? Je, mtu wa maneno mengi aonesha kuwa hana hatia? Je, kuropoka kwako kutanyamazisha watu? Na kama ukidhihaki, je, hamna atakayekuaibisha? Wewe wadai: ‘Ninachosema ni kweli, naam, sina lawama mbele ya Mungu.’ Laiti Mungu angefungua kinywa chake akatoa sauti yake kukujibu! Angekueleza siri za hekima, maana yeye ni mwingi wa maarifa. Jua kwamba Mungu hakuhesabu makosa yako yote. “Je, unaweza kugundua siri zake Mungu na kujua ukomo wake yeye Mungu mwenye nguvu? Ukuu wake wapita mbingu, wewe waweza nini? Kimo chake chapita Kuzimu, wewe waweza kujua nini? Ukuu huo wapita marefu ya dunia, wapita mapana ya bahari. Kama Mungu akipita, akamfunga mtu na kumhukumu, nani awezaye kumzuia? Mungu anajua watu wasiofaa; akiona maovu yeye huchukua hatua. “Mpumbavu hawezi kuwa na maarifa, pundamwitu ni pundamwitu tu. “Yobu, ukiufanya moyo wako mnyofu, utainua mikono yako kumwomba Mungu! Kama una uovu, utupilie mbali. Usikubali ubaya uwemo nyumbani mwako. Hapo utajitokeza mbele ya watu bila lawama, utakuwa thabiti bila kuwa na hofu. Utazisahau taabu zako zote; utazikumbuka tu kama mafuriko yaliyopita. Maisha yako yatangaa kuliko jua la adhuhuri, giza lake litabadilika kuwa mngao wa pambazuko. Utakuwa na ujasiri maana lipo tumaini; utalindwa na kupumzika salama. Utalala bila kuogopeshwa na mtu; watu wengi watakuomba msaada. Lakini waovu macho yao yatafifia, njia zote za kutorokea zitawapotea; tumaini lao la mwisho ni kukata roho!”
Yobu 11:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu, na kusema, Je! Huu wingi wa maneno usijibiwe? Na mtu aliyejaa maneno, je! Ahesabiwe kuwa na haki? Je! Majivuno yako yawanyamazishe watu wawe kimya? Nawe hapo ufanyapo dhihaka, je! Hapana mtu atakayekutahayarisha? Kwa kuwa wewe wasema, Mafunzo yangu ni safi, Nami ni safi machoni pako. Lakini, laiti Mungu angenena, Na kuifunua midomo yake juu yako; Tena akuoneshe hizo siri za hekima, Ya kuwa hufanikiwa katika kuyatimiza makusudi yake! Ujue basi ya kuwa Mungu akuachilia katika uovu wako. Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu? Waweza kuufikia upeo wa huyo Mwenyezi? Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe? Ni wenye kina kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe? Cheo chake ni kirefu kuliko dunia, Ni kipana zaidi ya bahari. Yeye akipita, na kufunga watu, Na kuwaita hukumuni, ni nani basi awezaye kumzuia? Kwa kuwa yeye awajua watu baradhuli; Anapouona uovu, je; hatauangalia? Lakini mpumbavu aweza kupata ufahamu, Ingawa mwanadamu huzaliwa kama mtoto wa punda mwitu. Wewe ukiuweka moyo wako kwa uelekevu, Na kumnyoshea mikono yako; Ikiwa una uovu mkononi mwako, uweke mbali nawe, Wala usikubali upuzi kukaa hemani mwako; Hakika ndipo utakapopata kuinua uso pasipo ila; Naam, utathibitika, wala hutakuwa na hofu; Kwa kuwa utasahau mateso yako; Utayakumbuka kama maji yaliyokwisha pita; Na maisha yako yatakuwa meupe kuliko adhuhuri; Giza lake litakuwa kama alfajiri. Nawe utakuwa salama, kwa sababu kuna matumaini; Naam, utatafutatafuta kando yako, na kupumzika salama. Tena utalala, wala hapana atakayekutia hofu; Naam, wengi watakutafuta uso wako. Lakini macho ya waovu yataingia kiwi, Nao hawatakuwa na njia ya kukimbilia, Na matumaini yao yatakuwa ni kutoa roho.
Yobu 11:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu, na kusema, Je! Huu wingi wa maneno usijibiwe? Na mtu aliyejaa maneno, je! Ahesabiwe kuwa na haki? Je! Majivuno yako yawanyamazishe watu wawe kimya? Nawe hapo ufanyapo dhihaka, je! Hapana mtu atakayekutahayarisha? Kwa kuwa wewe wasema, Mafunzo yangu ni safi, Nami ni safi machoni pako. Lakini, laiti Mungu angenena, Na kuifunua midomo yake juu yako; Tena akuonyeshe hizo siri za hekima, Ya kuwa hufanikiwa katika kuyatimiza makusudi yake! Ujue basi ya kuwa Mungu akuachilia katika uovu wako. Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu? Waweza kuufikilia upeo wa huyo Mwenyezi? Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe? Ni wenye kina kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe? Cheo chake ni kirefu kuliko dunia, Ni kipana zaidi ya bahari. Yeye akipita, na kufunga watu, Na kuwaita hukumuni, ni nani basi awezaye kumzuia? Kwani yeye awajua watu baradhuli; Huona na uovu pia, hata asipoufikiri. Lakini mpumbavu aweza kupata ufahamu, Ingawa mwanadamu huzaliwa kama mtoto wa punda-mwitu. Wewe ukiuweka moyo wako kwa uelekevu, Na kumnyoshea mikono yako; Ikiwa una uovu mkononi mwako, uweke mbali nawe, Wala usikubali upuzi kukaa hemani mwako; Hakika ndipo utakapopata kuinua uso pasipo ila; Naam, utathibitika, wala hutakuwa na hofu; Kwa kuwa utasahau mashaka yako; Utayakumbuka kama maji yaliyokwisha pita; Na maisha yako yatakuwa meupe kuliko adhuhuri; Lijapokuwa ni giza, litakuwa kama alfajiri. Nawe utakuwa salama, kwa sababu kuna matumaini; Naam, utatafuta-tafuta kando yako, na kupumzika katika salama. Tena utalala, wala hapana atakayekutia hofu; Naam, wengi watakutafuta uso wako. Lakini macho ya waovu yataingia kiwi, Nao hawatakuwa na njia ya kukimbilia, Na matumaini yao yatakuwa ni kutoa roho.
Yobu 11:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu: “Je, maneno haya yote yapite bila kujibiwa? Je, huyu mnenaji athibitishwe kuwa na haki? Je, maneno yako ya upuzi yawafanye watu wanyamaze kimya? Je, mtu asikukemee unapofanya dhihaka? Unamwambia Mungu, ‘Imani yangu ni kamili nami ni safi mbele zako.’ Aha! Laiti kwamba Mungu angesema, kwamba angefungua midomo yake dhidi yako, naye akufunulie siri za hekima, kwa kuwa hekima ya kweli ina pande mbili. Ujue hili: Mungu amesahau hata baadhi ya dhambi zako. “Je, unaweza kujua siri za Mungu? Je, unaweza kuyachunguza mambo yote kumhusu Mwenyezi? Ni juu mno kuliko mbingu: unaweza kufanya nini? Kina chake ni kirefu kuliko Kuzimu: wewe unaweza kujua nini? Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia, nacho ni kipana kuliko bahari. “Akija na kukufunga gerezani, na kuitisha mahakama, ni nani awezaye kumpinga? Hakika anawatambua watu wadanganyifu; naye aonapo uovu, je, haangalii? Mpumbavu aweza kuwa mwenye hekima, endapo mtoto wa punda-mwitu atazaliwa mwanadamu. “Hata sasa ukiutoa moyo wako kwake na kumwinulia mikono yako, ukiiondolea mbali ile dhambi iliyo mkononi mwako, wala usiuruhusu uovu ukae kwenye hema lako, ndipo utainua uso wako bila aibu; utasimama imara bila hofu. Hakika utaisahau taabu yako, utaikumbuka tu kama maji yaliyokwisha kupita. Maisha yako yatangʼaa kuliko adhuhuri, nalo giza litakuwa kama alfajiri. Utakuwa salama, kwa kuwa lipo tumaini; utatazama pande zote na kupumzika kwa salama. Utalala, wala hakuna atakayekuogofya, naam, wengi watajipendekeza kwako. Bali macho ya waovu hayataona, wokovu utawaepuka; tarajio lao litakuwa ni hangaiko la mtu anayekata roho.”