Yobu 10:1-22
Yobu 10:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
“Nayachukia maisha yangu! Malalamiko yangu nitayasema bila kizuizi. Nitasema kwa uchungu wa moyo wangu. Nitamwambia Mungu: Usinihukumu. Nijulishe kisa cha kupingana nami. Je, ni sawa kwako kunionea, kuidharau kazi ya mikono yako na kuipendelea mipango ya waovu? Je, una macho kama ya binadamu? Je, waona kama binadamu aonavyo? Je, siku zako ni kama za binadamu? Au miaka yako kama ya binadamu, hata uuchunguze uovu wangu, na kuitafuta dhambi yangu? Wewe wajua kwamba mimi sina hatia, na hakuna wa kuniokoa mikononi mwako. Mikono yako iliniunda na kuniumba, lakini sasa wageuka kuniangamiza. Kumbuka kwamba uliniumba kwa udongo. Je, utanirudisha tena mavumbini? Je, si wewe uliyenimimina kama maziwa, na kunigandisha kama jibini? Uliuumba mwili wangu kwa mifupa na mishipa, ukaifunika mifupa yangu kwa nyama na ngozi. Umenijalia uhai na fadhili, uangalifu wako umeisalimisha nafsi yangu. Hata hivyo mambo haya uliyaficha moyoni. Lakini najua kuwa hiyo ilikuwa nia yako. Ulikuwa unangojea uone kama nitatenda dhambi, ili ukatae kunisamehe uovu wangu. Kama mimi ni mwovu, ole wangu! Kama mimi ni mwadilifu, siwezi kujisifu; kwani nimejaa fedheha, nikiyatazama mateso yangu. Nikiinua kichwa tu waniwinda kama simba na kuniponda tena kwa maajabu yako. Kila mara unao ushahidi dhidi yangu; waiongeza hasira yako dhidi yangu, waniletea maadui wapya wanishambulie. “Ee Mungu, kwa nini ulinitoa tumboni mwa mama? Afadhali ningekufa kabla ya watu kuniona. Ningepelekwa moja kwa moja kaburini, nikawa kama mtu asiyepata kuwako. Je, siku za maisha yangu si chache? Niachie nipate faraja kidogo, kabla ya kwenda huko ambako sitarudi, huko kwenye nchi ya huzuni na giza nene; nchi ya huzuni na fujo, ambako mwanga wake ni kama giza.”
Yobu 10:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nayachukia maisha yangu; Nitayasema malalamiko yangu wazi; Nitanena kwa uchungu wa roho yangu. Nitamwambia Mungu, Usinihukumie makosa; Nijulishe kwa nini unapingana nami. Je! Ni vema kwako wewe kuonea, Na kuidharau kazi ya mikono yako, Na kuiunga mkono mipango ya waovu? Je! Wewe una macho ya kimwili, Au je! Waona kama aonavyo binadamu? Je! Siku zako ni kama siku za mtu, Au je! Miaka yako ni kama miaka ya mtu, Hata ukaulizauliza habari za uovu wangu, Na kuitafuta dhambi yangu, Ujapojua ya kuwa mimi si mwovu; Wala hapana awezaye kuokoa kutoka kwa mkono wako? Mikono yako imeniumba na kunifinyanga; Nawe utageuka na kuniangamiza? Kumbuka, nakusihi ulivyonifinyanga kama vile udongo; Nawe, je! Utanirudisha uvumbini tena? Je! Wewe hukunimimina kama maziwa, Na kunigandisha mfano wa jibini? Umenivika ngozi na nyama, Na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa. Unanijalia uhai na fadhili, Na kwa uangalifu wako roho yangu imetunzwa. Lakini mambo haya uliyaficha moyoni mwako; Najua kuwa haya yamo nafsini mwako; Nikifanya dhambi, ndipo waniangalia, Wala hutaniachilia na uovu wangu. Mimi nikiwa mwovu, ole wangu! Nami nikiwa mwenye haki, walakini sitainua kichwa changu; Maana nimejaa aibu Nikiyaangalia mateso yangu. Kichwa changu kikijiinua, waniwinda kama simba; Tena wajionesha kwangu kuwa wa ajabu. Wewe unafanya upya ushahidi wako juu yangu, Na kuongeza kisirani chako juu yangu; Ukileta jeshi baada ya jeshi juu yangu. Kwa nini basi kunitoa tumboni? Ningekata roho, lisinione jicho lolote. Ningalikuwa kama mtu asiyekuwapo; Ningalichukuliwa kaburini kutoka tumboni. Je! Siku zangu si chache? Acha basi, Usinisumbue, nipate angaa kutulizwa moyo kidogo. Kabla sijaenda huko ambako sitarudi kutoka huko tena, Ni hiyo nchi ya giza, giza tupu; Ni nchi ya giza kuu, kama giza lenyewe lilivyo; Ni nchi ya giza tupu, isiyo na mpango wowote wa mambo, Nchi ambayo nuru yake ni kama giza.
Yobu 10:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nafsi yangu inachoka na maisha yangu; Sitajizuia na kuugua kwangu; Nitanena kwa uchungu wa roho yangu. Nitamwambia Mungu, Usinihukumie makosa; Nionyeshe sababu ya wewe kushindana nami. Je! Ni vema kwako wewe kuonea, Na kuidharau kazi ya mikono yako, Na kuyaangazia mashauri ya waovu? Je! Wewe una macho ya kimwili, Au je! Waona kama aonavyo binadamu? Je! Siku zako ni kama siku za mtu, Au je! Miaka yako ni kama siku za mtu, Hata ukauliza-uliza habari za uovu wangu, Na kuitafuta dhambi yangu, Ujapojua ya kuwa mimi si mwovu; Wala hapana awezaye kuokoa na mkono wako? Mikono yako imeniumba na kunifinyanga; Nawe utageuka na kuniangamiza? Kumbuka, nakusihi ulivyonifinyanga kama vile udongo; Nawe, je! Utanirudisha uvumbini tena? Je! Wewe hukunimimina kama maziwa, Na kunigandisha mfano wa jibini? Umenivika ngozi na nyama, Na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa. Umenijazi uhai na upendeleo, Na maangalizi yako yameilinda roho yangu. Lakini mambo haya uliyaficha moyoni mwako; Najua kuwa haya yamo nafsini mwako; Nikifanya dhambi, ndipo waniangalia, Wala hutaniachilia na uovu wangu. Mimi nikiwa mbaya, ole wangu! Nami nikiwa mwenye haki, walakini sitainua kichwa changu; Mimi nimejaa aibu Na kuyaangalia mateso yangu. Kichwa changu kikijiinua, waniwinda kama simba; Tena wajionyesha kwangu kuwa wa ajabu. Wewe warejeza upya hao mashahidi yako juu yangu, Na kasirani yako waiongeza juu yangu; Jeshi kwa jeshi juu yangu. Kwa nini basi kunitoa tumboni? Ningekata roho, lisinione jicho lo lote. Ningalikuwa kama mtu asiyekuwapo; Ningalichukuliwa kaburini kutoka tumboni. Je! Siku zangu si chache? Acha basi, Usinisumbue, nipate ngaa kutuzwa moyo kidogo. Kabla sijaenda huko ambako sitarudi kutoka huko tena, Ni hiyo nchi ya giza, giza tupu; Ni nchi ya giza kuu, kama giza lenyewe lilivyo; Ni nchi ya giza tupu, isiyo na matengezo ya mambo yo yote, Nchi ambayo nuru yake ni kama giza.
Yobu 10:1-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Nayachukia sana haya maisha yangu; kwa hiyo nitatoa malalamiko yangu kwa wazi bila kujizuia, nami nitanena kutokana na uchungu wa moyo wangu. Nitamwambia Mungu: Usinihukumu, bali niambie una mashtaka gani dhidi yangu. Je, inakupendeza wewe kunidhulumu, kuikataa kazi ya mikono yako, huku ukiunga mkono mipango ya waovu? Je, wewe una macho ya kimwili? Je, wewe huona kama mwanadamu aonavyo? Je, siku zako ni kama zile za mwanadamu, au miaka yako ni kama ile ya mtu, ili utafute makosa yangu na kuichunguza dhambi yangu; ingawa unajua kuwa mimi sina hatia, na hakuna awezaye kunitoa mkononi mwako? “Mikono yako ndiyo iliyoniumba na kunifanya. Je, sasa utageuka na kuniangamiza? Kumbuka kuwa ulinifinyanga kama udongo wa mfinyanzi. Je, sasa utanifanya kuwa mavumbi tena? Je, wewe hukunimimina mimi kama maziwa, na kunigandisha kama jibini, ukanivika ngozi na nyama, na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa? Umenipa uhai na kunitendea wema, katika uangalizi wako umeilinda roho yangu. “Lakini hili ndilo ulilolificha moyoni mwako, nami ninajua kuwa hili lilikuwa katika nia yako: Kama nilifanya dhambi, ungekuwa umeniona, wala usingeacha kosa langu lipite bila kuadhibiwa. Kama nina hatia, ole wangu! Hata kama ningekuwa sina hatia, siwezi kukiinua kichwa changu, kwa kuwa nimejawa na aibu, na kuzama katika mateso yangu. Nikiinua kichwa changu juu, unaniwinda kama simba, na kuonesha tena uwezo wa kutisha dhidi yangu. Wewe waleta mashahidi wapya dhidi yangu na kuzidisha hasira yako juu yangu; nazo nguvu zako zinanijia wimbi moja baada ya jingine. “Kwa nini basi ulinitoa tumboni? Ninatamani ningekufa kabla jicho lolote halijaniona. Laiti nisingezaliwa, au kama ningepelekwa kaburini moja kwa moja kutoka tumboni! Je, siku zangu chache si zimekaribia kuisha? Niachie ili niweze kupata muda mfupi wa kufurahi kabla sijaenda mahali ambapo hakuna kurudi tena, katika nchi ya giza na uvuli wa mauti, nchi ya giza nene sana, yenye uvuli wa giza na machafuko, ambapo hata nuru ni giza.”