Yobu 1:6-11
Yobu 1:6-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, ikatokia siku moja malaika wa Mungu walikwenda kukutana mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye Shetani, akajitokeza pia pamoja nao. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Naye Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Nimetoka kutembeatembea na kuzungukazunguka duniani.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Bila shaka umemtambua mtumishi wangu Yobu. Duniani kote hamna mwingine aliye kama yeye. Yeye ni mtu mnyofu, mcha Mungu na mwenye kujiepusha na uovu.” Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Je, Yobu anamcha Mwenyezi-Mungu bure? Je, si dhahiri kwamba wewe unamlinda pande zote pamoja na jamaa yake na kila kitu alicho nacho? Wewe umembariki na mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini sasa, hebu nyosha tu mkono wako uiguse mali yake kama hutaona akikutukana waziwazi!”
Yobu 1:6-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujiweka mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzungukazunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu anamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.
Yobu 1:6-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.
Yobu 1:6-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku moja wana wa Mungu walienda kujionesha mbele za BWANA. Shetani naye akaja pamoja nao. BWANA akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?” Shetani akamjibu BWANA, “Natoka kuzunguka duniani, nikitembea huku na huko.” Ndipo BWANA akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu, na kuepukana na uovu.” Shetani akamjibu BWANA, “Je, Ayubu anamcha Mungu bure? Je, wewe hukumzingira pande zote, yeye na watu wa nyumbani mwake, pamoja na kila kitu alicho nacho? Kazi za mikono yake umezibariki, na hivyo makundi yake ya kondoo na mbuzi pamoja na ya wanyama yameenea katika nchi nzima. Lakini nyoosha mkono wako na kupiga kila kitu alicho nacho, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”