Yobu 1:1-5
Yobu 1:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Palikuwa na mtu mmoja nchini Usi, aitwaye Yobu. Mtu huyo alikuwa mwema na mnyofu; mtu mcha Mungu na mwenye kuepukana na uovu. Yobu alikuwa na watoto saba wa kiume na watatu wa kike; alikuwa na kondoo 7,000, ngamia 3,000, jozi 500 za ng'ombe na punda majike 500; na watumishi wengi sana; yeye alikuwa mashuhuri kuliko watu wote huko mashariki. Mara kwa mara, wanawe Yobu walifanya karamu nyumbani kwa kila mmoja wao kwa zamu; waliwaalika dada zao kula na kunywa pamoja nao. Kila baada ya karamu, Yobu aliwaita wanawe ili awatakase. Aliamka asubuhi na mapema baada ya karamu, akatoa tambiko za kuteketezwa kwa ajili ya kila mmoja wao kwani aliwaza, “Huenda wanangu wametenda dhambi na kumtukana Mungu mioyoni mwao.”
Yobu 1:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake watoto saba wa kiume, na binti watatu. Mali yake nayo ilikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watumishi wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki. Nao wanawe wa kiume huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakawaalika dada zao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao. Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Pengine hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote.
Yobu 1:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu. Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng’ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki. Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao. Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote.
Yobu 1:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika nchi ya Usi paliishi mtu ambaye aliitwa Ayubu. Mtu huyu alikuwa hana hatia, naye alikuwa mkamilifu; alimcha Mungu na kuepukana na uovu. Alikuwa na wana saba na binti watatu, naye alikuwa na kondoo elfu saba, ngamia elfu tatu, jozi mia tano za maksai, na punda mia tano, tena alikuwa na idadi kubwa ya watumishi. Alikuwa mtu maarufu sana miongoni mwa watu wa Mashariki. Wanawe walikuwa na desturi ya kufanya karamu katika nyumba zao kwa zamu, nao wangewaalika dada zao watatu ili kula na kunywa pamoja nao. Kipindi cha karamu kilipomalizika, Ayubu angetuma waitwe na kuwafanyia utakaso. Angetoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya kila mmoja wao asubuhi na mapema, akifikiri, “Pengine wanangu wametenda dhambi na kumlaani Mungu mioyoni mwao.” Hii ilikuwa ndiyo desturi ya kawaida ya Ayubu.