Yohane 6:41-51
Yohane 6:41-51 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Wayahudi wakaanza kunungunika kwa kuwa alisema: “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunamjua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?” Yesu akawaambia, “Acheni kunungunika nyinyi kwa nyinyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo siku ya mwisho. Manabii wameandika: ‘Watu wote watafundishwa na Mungu.’ Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu. Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uhai wa milele. Mimi ni mkate wa uhai. Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa. Lakini huu ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni ili yeyote atakayeula asife. Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uhai wa ulimwengu.”
Yohane 6:41-51 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Wayahudi wakamnung'unikia, kwa sababu alisema, Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Wakasema, Je! Huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, Nimeshuka kutoka mbinguni? Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung'unike ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenituma; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu. Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye anao uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.
Yohane 6:41-51 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Wayahudi wakamnung’unikia, kwa sababu alisema, Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Wakasema, Je! Huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, Nimeshuka kutoka mbinguni? Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung’unike ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu. Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.
Yohane 6:41-51 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wayahudi wakaanza kunungʼunika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” Wakasema, “Huyu si Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?” Hivyo Yesu akawaambia, “Acheni kunungʼunikiana ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika Manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Yeyote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu. Hakuna mtu yeyote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba. Amin, amin nawaambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele. Mimi ni mkate wa uzima. Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa. Lakini hapa kuna mkate kutoka mbinguni, ambao mtu yeyote akiula, hatakufa. Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”