Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 6:1-71

Yohane 6:1-71 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au ziwa Tiberia). Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa. Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake. Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia. Basi, Yesu alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia Filipo, “Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?” (Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.) Filipo akamjibu, “Mikate ya fedha dinari 200 haiwatoshi watu hawa hata kama kila mmoja atapata kipande kidogo tu!” Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, “Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?” Yesu akasema, “Waketisheni watu.” Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume 5,000. Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka. Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee.” Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili. Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, “Hakika huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni.” Yesu akajua kwamba watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, akaenda mlimani peke yake. Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani, wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado. Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana. Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope!” Basi wakataka kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu walikokuwa wanakwenda. Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua pamoja na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke yao. Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu. Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta. Wale watu walipomkuta Yesu ngambo ya pili wa ziwa walimwuliza, “Mwalimu, ulifika lini hapa?” Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishughulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uhai wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho.” Wao wakamwuliza, “Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?” Yesu akawajibu, “Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu mwifanye: Kumwamini yule aliyemtuma.” Hapo wakamwambia, “Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya kitu gani? Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: ‘Aliwalisha mkate kutoka mbinguni.’” Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye nyinyi mkate wa kweli kutoka mbinguni. Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uhai.” Basi, wakamwambia, “Bwana, tupe daima mkate huo.” Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe. Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini. Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami kamwe sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu, kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma. Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: Nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote siku ya mwisho. Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: Kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uhai wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.” Basi, Wayahudi wakaanza kunungunika kwa kuwa alisema: “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunamjua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?” Yesu akawaambia, “Acheni kunungunika nyinyi kwa nyinyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo siku ya mwisho. Manabii wameandika: ‘Watu wote watafundishwa na Mungu.’ Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu. Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uhai wa milele. Mimi ni mkate wa uhai. Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa. Lakini huu ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni ili yeyote atakayeula asife. Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uhai wa ulimwengu.” Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: “Anawezaje huyu kutupa mwili wake, tule?” Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu. Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uhai wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho. Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake. Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu. Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu zenu, wakafa. Aulaye mkate huu atakuwa hai milele.” Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu. Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, “Haya ni mambo magumu! Nani awezaye kuyasikiliza?” Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananungunika juu ya jambo hilo, akawauliza, “Je, jambo hili linawafanya muwe na mashaka? Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa kwanza? Roho ndiyo iletayo uhai; mwili hauwezi kitu. Maneno niliyowaambia ni roho na uhai. Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini.” (Yesu alisema hivyo kwani alijua tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti). Kisha akasema, “Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu.” Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma, wasiandamane naye tena. Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, “Je, nanyi pia mwataka kwenda zenu?” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno ya uhai wa milele. Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu” Yesu akawaambia, “Je, sikuwachagua nyinyi kumi na wawili? Hata hivyo, mmoja wenu ni Ibilisi!” Yesu alisema hayo juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyu alikuwa ndiye atakayemsaliti, ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili.

Shirikisha
Soma Yohane 6

Yohane 6:1-71 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng'ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akapanda mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, ana mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi wanaume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee chochote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, alipotambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake. Hata ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakateremka baharini wakapanda katika mashua, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kuikaribia mashua; wakaogopa. Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. Basi wakataka kumpokea katika mashua; na mara hiyo mashua ikaifikia nchi waliyokuwa wakiiendea. Kesho yake mkutano waliosimama ng'ambo ya bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja, tena ya kuwa Yesu hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake walikwenda peke yao, (lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka karibu na mahali pale walipokula mikate, wakati Bwana aliposhukuru.) Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. Hata walipomwona ng'ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa? Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa mhuri na Baba, yaani, Mungu. Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye. Wakamwambia, Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani? Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale. Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Sio Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini niliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenituma. Na mapenzi yake aliyenituma ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Basi Wayahudi wakamnung'unikia, kwa sababu alisema, Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Wakasema, Je! Huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, Nimeshuka kutoka mbinguni? Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung'unike ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenituma; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu. Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye anao uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele. Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu. Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung'unikia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mumwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Kumi na Wawili, Je! Ninyi nanyi mnataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumeamini, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu. Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Kumi na Wawili, na mmoja wenu ni shetani? Alimnena Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyo ndiye atakayemsaliti; naye ni mmojawapo wa wale Kumi na Wawili.

Shirikisha
Soma Yohane 6

Yohane 6:1-71 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake. Hata ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakatelemka baharini wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa. Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea. Siku ya pili yake mkutano waliosimama ng’ambo ya bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja, tena ya kuwa Yesu hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake walikwenda peke yao. (Walakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka karibu na mahali pale walipokula mikate, wakati Bwana aliposhukuru.) Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa? Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu. Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye. Wakamwambia, Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani? Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale. Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Basi Wayahudi wakamnung’unikia, kwa sababu alisema, Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Wakasema, Je! Huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, Nimeshuka kutoka mbinguni? Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung’unike ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu. Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele. Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu. Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unikia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu. Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani? Alimnena Yuda, mwana wa Simoni Iskariote; maana huyo ndiye atakayemsaliti; naye ni mmojawapo wa wale Thenashara.

Shirikisha
Soma Yohane 6

Yohane 6:1-71 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Baada ya haya, Yesu alienda ngʼambo ya Bahari ya Galilaya (ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia). Umati mkubwa wa watu waliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa. Kisha Yesu akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. Yesu alipotazama na kuona umati ule mkubwa wa watu wakimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya. Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa ili kila mtu apate kidogo.” Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia, “Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa watu hawa wote?” Yesu akasema, “Waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi (palikuwa na wanaume wapatao elfu tano). Ndipo Yesu akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wameketi. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka. Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee chochote.” Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula. Baada ya watu kuona muujiza ule Yesu aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!” Yesu akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake. Ilipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini. Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Yesu alikuwa hajajumuika nao. Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. Wanafunzi walipokuwa wameenda mwendo wa maili tatu au nne, walimwona Yesu akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana. Lakini Yesu akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.” Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda. Siku iliyofuata, wale watu waliokuwa wamebaki ngʼambo waliona kwamba palikuwa na mashua moja tu, na kwamba Yesu hakuwa ameondoka pamoja na wanafunzi wake, ila walikuwa wameondoka peke yao. Lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia zikafika karibu na mahali pale walipokula mikate baada ya Bwana kumshukuru Mungu. Mara wale watu wakatambua kwamba Yesu hakuwa hapo, wala wanafunzi wake. Wakaingia kwenye mashua hizo, wakaenda Kapernaumu ili kumtafuta Yesu. Walipomkuta Yesu ngʼambo ya bahari wakamuuliza, “Rabi, umefika lini huku?” Yesu akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba amemtia muhuri.” Ndipo wakamuuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?” Yesu akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.” Hivyo wakamuuliza, “Utafanya ishara gani ya muujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani? Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’” Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Musa aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.” Wakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.” Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe. Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini. Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuza nje kamwe. Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. Haya ndio mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.” Wayahudi wakaanza kunungʼunika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” Wakasema, “Huyu si Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?” Hivyo Yesu akawaambia, “Acheni kunungʼunikiana ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika Manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Yeyote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu. Hakuna mtu yeyote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba. Amin, amin nawaambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele. Mimi ni mkate wa uzima. Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa. Lakini hapa kuna mkate kutoka mbinguni, ambao mtu yeyote akiula, hatakufa. Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Ndipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?” Hivyo Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Mtu yeyote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Yeyote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu. Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.” Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu. Wengi wa wafuasi wake waliposikia jambo hili wakasema, “Mafundisho haya ni magumu. Ni nani awezaye kuyapokea?” Yesu alipojua kwamba wafuasi wake wananungʼunika kuhusu mafundisho yake, akawaambia, “Je, jambo hili limewaudhi? Ingekuwaje basi kama mngemwona Mwana wa Adamu akipaa kwenda zake huko alipokuwa kwanza? Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima. Lakini baadhi yenu hamwamini.” Kwa maana Yesu alifahamu tangu mwanzo wale ambao hawangemwamini miongoni mwao na yule ambaye angemsaliti. Akaendelea kusema, “Hii ndiyo sababu niliwaambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.” Tangu wakati huo wafuasi wake wengi wakarejea nyuma wakaacha kumfuata. Hivyo Yesu akawauliza wale wanafunzi wake kumi na wawili, “Je, ninyi pia mnataka kuondoka?” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Tunaamini na kujua kuwa wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu.” Ndipo Yesu akajibu, “Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Lakini mmoja wenu ni ibilisi.” (Hapa alikuwa anasema kuhusu Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili, ndiye ambaye baadaye angemsaliti Yesu.)

Shirikisha
Soma Yohane 6