Yohane 5:1-9
Yohane 5:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu. Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye matao. Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: Vipofu, viwete na waliopooza. [Walikuwa wakingojea maji yatibuliwe, maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.] Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane. Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo na kujua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, “Je, wataka kupona?” Naye akajibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia.” Yesu akamwambia, “Inuka, chukua mkeka wako utembee.” Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato.
Yohane 5:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akapanda kwenda Yerusalemu. Na huko Yerusalemu karibu na mlango wa kondoo pana bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, nalo lilikuwa na matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke. Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika lile bwawa, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.] Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa mgonjwa muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa katika hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia katika bwawa, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.
Yohane 5:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akakwea kwenda Yerusalemu. Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke. Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.] Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.
Yohane 5:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya haya, kulikuwa na Sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akapanda kwenda Yerusalemu. Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa Bethzatha kwa Kiebrania, ambalo lilikuwa limezungukwa na makumbi matano. Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani vipofu, viwete, na waliopooza [wakingojea maji yatibuliwe. Kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji. Yule angekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao]. Mtu mmoja aliyekuwa ameugua kwa miaka thelathini na nane alikuwa hapo. Yesu alipomwona akiwa amelala hapo, na akijua amekuwa katika hali hiyo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?” Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.” Yesu akamwambia, “Inuka! Chukua mkeka wako na uende.” Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea. Basi siku hiyo ilikuwa siku ya Sabato.