Yohane 4:7-14
Yohane 4:7-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, “Nipatie maji ninywe.” (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.) Lakini huyo mwanamke akamwambia, “Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?” (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu). Yesu akamjibu, “Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekuambia: ‘Nipatie maji ninywe,’ ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yenye uhai.” Huyo mama akasema, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yenye uhai? Au, labda wewe wajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo wake walikunywa maji ya kisima hiki.” Yesu akamjibu, “Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uhai na kumpatia uhai wa milele.”
Yohane 4:7-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawatangamani na Wasamaria.) Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake? Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; lakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.
Yohane 4:7-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.) Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake? Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.
Yohane 4:7-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mwanamke mmoja Msamaria alipokuja kuteka maji, Yesu akamwambia, “Naomba maji ninywe.” (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wameenda mjini kununua chakula.) Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe maji ya kunywa?” (Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.) Yesu akamjibu, “Kama ungeijua karama ya Mungu, na ni nani anakuomba maji ya kunywa, ungemwomba yeye, naye angekupa maji ya uzima.” Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi? Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?” Yesu akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki ataona kiu tena. Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika uzima wa milele.”