Yohane 3:3-11
Yohane 3:3-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, mtu asipozaliwa tena hataweza kuuona ufalme wa Mungu.” Nikodemo akamwuliza, “Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa tena!” Yesu akamjibu, “Kweli nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu. Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho. Usistaajabu kwamba nimekuambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya. Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho.” Nikodemo akamwuliza, “Mambo haya yanawezekanaje?” Yesu akamjibu, “Je, wewe ni mwalimu katika Israeli na huyajui mambo haya? Kweli nakuambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia tuliyoyaona, lakini nyinyi hamkubali ujumbe wetu.
Yohane 3:3-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho. Nikodemo akajibu, akamwambia, Mambo haya yawezaje kuwa? Yesu akajibu, akamwambia, Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu? Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo tunalinena, na lile tuliloliona tunalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali.
Yohane 3:3-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho. Nikodemo akajibu, akamwambia, Yawezaje kuwa mambo haya? Yesu akajibu, akamwambia, Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu? Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali.
Yohane 3:3-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu akamjibu, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu anayeweza kuuona ufalme wa Mungu kama hajazaliwa mara ya pili.” Nikodemo akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa akiwa mzee? Hakika hawezi kuingia mara ya pili kwenye tumbo la mama yake ili azaliwe!” Yesu akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia ufalme wa Mungu kama hajazaliwa kwa maji na kwa Roho. Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho. Kwa hiyo usishangae ninapokuambia, ‘Huna budi kuzaliwa mara ya pili.’ Upepo huvuma kokote unakopenda. Mvumo wake unausikia lakini huwezi ukafahamu unakotoka wala unakoenda. Ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa na Roho.” Nikodemo akamuuliza, “Mambo haya yanawezekanaje?” Yesu akamwambia, “Wewe ni mwalimu wa Waisraeli, nawe huelewi mambo haya? Amin, amin ninakuambia, sisi tunazungumza lile tunalolijua na tunashuhudia lile tuliloliona. Lakini ninyi watu hamkubali ushuhuda wetu.