Yohane 3:1-16
Yohane 3:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Kulikuwa na kiongozi mmoja Myahudi, wa kikundi cha Mafarisayo, jina lake Nikodemo. Siku moja Nikodemo alimwendea Yesu usiku, akamwambia, “Rabi, tunajua kwamba wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye.” Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, mtu asipozaliwa tena hataweza kuuona ufalme wa Mungu.” Nikodemo akamwuliza, “Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa tena!” Yesu akamjibu, “Kweli nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu. Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho. Usistaajabu kwamba nimekuambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya. Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho.” Nikodemo akamwuliza, “Mambo haya yanawezekanaje?” Yesu akamjibu, “Je, wewe ni mwalimu katika Israeli na huyajui mambo haya? Kweli nakuambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia tuliyoyaona, lakini nyinyi hamkubali ujumbe wetu. Ikiwa nimewaambieni mambo ya kidunia nanyi hamniamini, mtawezaje kuamini nikiwaambieni mambo ya mbinguni? Hakuna mtu aliyepata kwenda juu mbinguni isipokuwa Mwana wa Mtu, ambaye ameshuka kutoka mbinguni. “Kama vile Mose alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani, naye Mwana wa Mtu atainuliwa juu vivyo hivyo, ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele. Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa milele.
Yohane 3:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, tunajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho. Nikodemo akajibu, akamwambia, Mambo haya yawezaje kuwa? Yesu akajibu, akamwambia, Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu? Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo tunalinena, na lile tuliloliona tunalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali. Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni? Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
Yohane 3:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho. Nikodemo akajibu, akamwambia, Yawezaje kuwa mambo haya? Yesu akajibu, akamwambia, Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu? Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali. Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni? Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
Yohane 3:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi palikuwa na mtu mmoja Farisayo, jina lake Nikodemo, mmoja wa Baraza la Wayahudi lililotawala. Huyu alimjia Yesu usiku akamwambia, “Rabi, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kufanya miujiza hii uifanyayo wewe, kama Mungu hayuko pamoja naye.” Yesu akamjibu, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu anayeweza kuuona ufalme wa Mungu kama hajazaliwa mara ya pili.” Nikodemo akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa akiwa mzee? Hakika hawezi kuingia mara ya pili kwenye tumbo la mama yake ili azaliwe!” Yesu akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia ufalme wa Mungu kama hajazaliwa kwa maji na kwa Roho. Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho. Kwa hiyo usishangae ninapokuambia, ‘Huna budi kuzaliwa mara ya pili.’ Upepo huvuma kokote unakopenda. Mvumo wake unausikia lakini huwezi ukafahamu unakotoka wala unakoenda. Ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa na Roho.” Nikodemo akamuuliza, “Mambo haya yanawezekanaje?” Yesu akamwambia, “Wewe ni mwalimu wa Waisraeli, nawe huelewi mambo haya? Amin, amin ninakuambia, sisi tunazungumza lile tunalolijua na tunashuhudia lile tuliloliona. Lakini ninyi watu hamkubali ushuhuda wetu. Nimewaambia mambo ya duniani, nanyi hamkuniamini, mtaniaminije basi nitakapowaambia mambo ya mbinguni? Hakuna mtu yeyote aliyeenda mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani Mwana wa Adamu. Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu, ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.