Yohane 21:6-11
Yohane 21:6-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akawaambia, “Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua nanyi mtapata samaki.” Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza kuuvuta tena kwa wingi wa samaki. Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa), akarukia majini. Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua huku wanauvuta wavu uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa yapata mita mia kutoka ukingoni. Walipofika nchi kavu waliona moto wa makaa umewashwa na juu yake pamewekwa samaki na mkate. Yesu akawaambia, “Leteni hapa baadhi ya samaki mliovua.” Basi, Simoni Petro akapanda mashuani, akavuta hadi nchi kavu ule wavu uliokuwa umejaa samaki wakubwa 153. Na ingawa walikuwa wengi hivyo, wavu haukukatika.
Yohane 21:6-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kulia wa mashua, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki. Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini. Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki. Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi. Basi Simoni Petro akapanda katika mashua, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka.
Yohane 21:6-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki. Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini. Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki. Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi. Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka.
Yohane 21:6-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu, na tazama, wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua. Basi yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia kwamba ni Bwana, akajifunga nguo yake (kwa kuwa alikuwa ameitoa), naye akajitosa baharini. Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa mia mbili. Walipofika ufuoni, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake, na mikate. Yesu akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.” Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu ufuoni. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa mia moja hamsini na watatu (153). Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika.