Yohane 2:6-11
Yohane 2:6-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha. Yesu akawaambia, “Ijazeni mitungi hiyo maji.” Nao wakaijaza mpaka juu. Kisha akawaambia, “Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu.” Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi, akamwambia, “Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!” Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini.
Yohane 2:6-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kunawa, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza mpaka juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa sherehe. Wakapeleka. Naye mkuu wa sherehe alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa sherehe alimwita bwana arusi, akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; na watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.
Yohane 2:6-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.
Yohane 2:6-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi hapo palikuwa na mitungi sita iliyotengenezwa kwa mawe; iliwekwa hapo kwa ajili ya desturi ya Kiyahudi ya kujitakasa; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu. Yesu akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi hadi juu. Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo; mpelekeeni mkuu wa sherehe.” Hivyo wakachota, wakampelekea. Yule mkuu wa sherehe akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilishwa kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando, akamwambia, “Watu wote hutoa divai nzuri kwanza, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa sana; lakini wewe umeiweka ile nzuri zaidi hadi sasa.” Huu ndio muujiza wa kwanza wa Yesu; aliufanya huko Kana ya Galilaya. Hivyo Yesu alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.