Yohane 14:21-31
Yohane 14:21-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, “Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?” Yesu akamjibu, “Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye. Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma. “Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi, lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni. “Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike. Mlikwisha sikia nikiwaambieni: ‘Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.’ Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi. Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini. Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu; lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!
Yohane 14:21-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskarioti), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenituma. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi niliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, ili litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana anakuja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.
Yohane 14:21-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskariote), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.
Yohane 14:21-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye. Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” Ndipo Yuda (siyo Iskariote) akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?” Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu, na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma. “Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. Lakini huyo Msaidizi, yaani huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachia; amani yangu nawapa. Amani hii ninayowapa si kama ile ulimwengu unatoa. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope. “Mlisikia nikisema, ‘Ninaenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngenipenda, mngefurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuliko mimi. Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru. “Haya inukeni; twendeni zetu.