Yohane 14:1-31
Yohane 14:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliwaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama isingekuwa hivyo, ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi. Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi. Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda.” Thoma akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?” Yesu akamjibu, “Mimi ni njia, na ukweli na uhai. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu. Ikiwa mnanijua mimi, mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona.” Filipo akamwambia, “Bwana, tuoneshe Baba, nasi tutatosheka.” Yesu akamwambia, “Nimekaa nanyi muda wote huu, nawe Filipo hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: ‘Tuoneshe Baba?’ Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake. Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya. Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, kwani ninakwenda kwa Baba. Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni. “Mkinipenda mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele. Yeye ni Roho wa ukweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini nyinyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu. “Sitawaacha nyinyi yatima; nitakuja tena kwenu. Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini nyinyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai. Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu. Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, “Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?” Yesu akamjibu, “Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye. Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma. “Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi, lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni. “Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike. Mlikwisha sikia nikiwaambieni: ‘Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.’ Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi. Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini. Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu; lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!
Yohane 14:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo. Nami niendako mwaijua njia. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi tunaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuoneshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuoneshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya. Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu. Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskarioti), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenituma. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi niliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, ili litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana anakuja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.
Yohane 14:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu. Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskariote), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.
Yohane 14:1-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mnamwamini Mungu, mniamini pia. Nyumbani mwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningewaambia. Naenda kuwaandalia makao. Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo nanyi mpate kuwepo. Ninyi mnajua njia ya kufika ninakoenda.” Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui unakoenda, tutaijuaje njia?” Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kupitia kwangu. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.” Filipo akamwambia, “Bwana, tuoneshe Baba, na hiyo itatutosha.” Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuoneshe Baba’? Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba, na Baba yuko ndani yangu; la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo. Amin, amin nawaambia, yeyote anayeniamini mimi, kazi ninazozifanya naye atazifanya. Naam, na atazifanya kazi kubwa kuliko hizi, kwa sababu mimi ninaenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lolote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. Mkiniomba lolote kwa Jina langu, nitalifanya. “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi, naye anakaa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona. Kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, na ninyi mko ndani yangu, na mimi niko ndani yenu. Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye. Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” Ndipo Yuda (siyo Iskariote) akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?” Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu, na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma. “Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. Lakini huyo Msaidizi, yaani huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachia; amani yangu nawapa. Amani hii ninayowapa si kama ile ulimwengu unatoa. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope. “Mlisikia nikisema, ‘Ninaenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngenipenda, mngefurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuliko mimi. Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru. “Haya inukeni; twendeni zetu.