Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 13:3-17

Yohane 13:3-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu. Basi, aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia. Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, “Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?” Yesu akamjibu, “Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye.” Petro akamwambia, “Wewe hutaniosha miguu kamwe!” Yesu akamjibu, “Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami tena.” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na kichwa pia.” Yesu akamwambia, “Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Nyinyi mmetakata, lakini si nyote.” ( Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: “Nyinyi mmetakata, lakini si nyote.”) Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, “Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni? Nyinyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi. Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu nimewaosha nyinyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu. Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni. Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu kuliko yule aliyemtuma. Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza.

Shirikisha
Soma Yohane 13

Yohane 13:3-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi. Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo. Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka. Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda.

Shirikisha
Soma Yohane 13

Yohane 13:3-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Yesu, akijua kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake, na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni. Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?” Yesu akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.” Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.” Yesu akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.” Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, Bwana, bali pamoja na mikono na kichwa pia!” Yesu akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.” Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi. Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi. Akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana’; hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri kwenu mkiyatenda.

Shirikisha
Soma Yohane 13