Yohane 13:3-10
Yohane 13:3-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu. Basi, aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia. Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, “Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?” Yesu akamjibu, “Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye.” Petro akamwambia, “Wewe hutaniosha miguu kamwe!” Yesu akamjibu, “Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami tena.” Simoni Petro akamjibu, “Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na kichwa pia.” Yesu akamwambia, “Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Nyinyi mmetakata, lakini si nyote.” (
Yohane 13:3-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu, huku akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Akamfikia Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe waniosha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutaniosha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Nisipokuosha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga mwili hana haja ila ya kuosha miguu, maana yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote.
Yohane 13:3-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote.
Yohane 13:3-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu, akijua kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake, na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni. Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?” Yesu akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.” Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.” Yesu akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.” Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, Bwana, bali pamoja na mikono na kichwa pia!” Yesu akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.”