Yohane 11:1-6
Yohane 11:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake. Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa). Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: “Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!” Yesu aliposikia hivyo, akasema, “Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe.” Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro. Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi.
Yohane 11:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi mtu mmoja alikuwa mgonjwa, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa mgonjwa. Basi wale dada wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye ni mgonjwa. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. Naye Yesu alimpenda Martha na dada yake na Lazaro. Basi aliposikia ya kwamba ni mgonjwa, bado alikaa siku mbili pale pale alipokuwapo.
Yohane 11:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi. Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro. Basi aliposikia ya kwamba hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo.
Yohane 11:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi mtu mmoja, jina lake Lazaro, alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania, kijiji cha Mariamu na Martha dada yake. (Huyu Mariamu, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye alimpaka Bwana mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake.) Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Yesu kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.” Lakini Yesu aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti, bali ni wa kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.” Yesu aliwapenda Martha, Mariamu na Lazaro ndugu yao. Hata hivyo, baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, alikawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi.