Yohane 1:6-32
Yohane 1:6-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane, ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini. Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote. Basi, Neno alikuwako ulimwenguni, na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua. Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu, ambao walizaliwa si kwa maumbile ya kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala mapenzi ya mtu, bali kutokana na Mungu mwenyewe. Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli. Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: ‘Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.’” Kutokana na ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema kupita neema. Maana Mungu alitoa sheria kwa njia ya Mose, nayo neema na kweli vimetujia kwa njia ya Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu. Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani na Walawi, wamwulize: “Wewe u nani?” Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.” Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Elia?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!” Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.” Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: ‘Sauti ya mtu anaita jangwani: Nyosheni njia ya Bwana.’” Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo. Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Masiha, wala Elia, wala yule nabii, mbona wabatiza?” Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado. Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.” Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ngambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza. Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyeongea juu yake niliposema: ‘Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!’ Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.” Yohane alishuhudia hivi: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.
Yohane 1:6-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua. Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Na tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wanenaje juu yako mwenyewe? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya. Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza kamba ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng'ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza. Kesho yake alimwona Yesu akija kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini ili adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nilikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake.
Yohane 1:6-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua. Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya. Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng’ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza. Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake.
Yohane 1:6-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kupitia kwake watu wote waweze kuamini. Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. Nuru halisi inayomwangazia kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni. Huyo Neno alikuwako ulimwenguni, na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. Bali wote waliompokea, yaani wale walioliamini jina lake, aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu. Hawa hawakuzaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali wamezaliwa kwa mapenzi ya Mungu. Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’ ” Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema. Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Musa, lakini neema na kweli zimekuja kupitia Yesu Kristo. Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba, ndiye ambaye amemdhihirisha. Huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati viongozi wa Wayahudi waliwatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Yohana alikiri waziwazi pasipo kuficha, akasema, “Mimi si Kristo.” Wakamuuliza, “Wewe ni nani, basi? Je, wewe ni Eliya?” Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.” “Je, wewe ni yule Nabii?” Akajibu, “Hapana.” Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?” Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Bwana.’” Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo, wakamuuliza, “Kama wewe si Kristo, wala si Eliya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?” Yohana akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji, lakini kati yenu yupo mtu msiyemjua. Yeye anakuja baada yangu, nami sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.” Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ngʼambo ya Yordani, mahali Yohana alipokuwa akibatiza. Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’ Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.” Kisha Yohana akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake.