Yohane 1:19-28
Yohane 1:19-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani na Walawi, wamwulize: “Wewe u nani?” Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.” Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Elia?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!” Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.” Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: ‘Sauti ya mtu anaita jangwani: Nyosheni njia ya Bwana.’” Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo. Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Masiha, wala Elia, wala yule nabii, mbona wabatiza?” Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado. Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.” Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ngambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.
Yohane 1:19-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Na tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wanenaje juu yako mwenyewe? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya. Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza kamba ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng'ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza.
Yohane 1:19-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya. Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng’ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza.
Yohane 1:19-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati Wayahudi walipowatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Yohana alikiri waziwazi pasipo kuficha akasema, “Mimi si Kristo.” Wakamuuliza, “Wewe ni nani basi? Je, wewe ni Eliya?” Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.” “Je, wewe ni yule Nabii?” Akajibu, “Hapana.” Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?” Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Bwana.’ ” Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo wakamuuliza, “Kama wewe si Kristo, wala si Eliya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?” Yohana akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji, lakini katikati yenu yupo mtu msiyemjua. Yeye ajaye baada yangu, sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.” Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ngʼambo ya Mto Yordani, mahali Yohana alipokuwa akibatiza.