Yohane 1:1-51
Yohane 1:1-51 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu. Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu. Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye. Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu. Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda. Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane, ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini. Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote. Basi, Neno alikuwako ulimwenguni, na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua. Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu, ambao walizaliwa si kwa maumbile ya kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala mapenzi ya mtu, bali kutokana na Mungu mwenyewe. Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli. Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: ‘Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.’” Kutokana na ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema kupita neema. Maana Mungu alitoa sheria kwa njia ya Mose, nayo neema na kweli vimetujia kwa njia ya Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu. Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani na Walawi, wamwulize: “Wewe u nani?” Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.” Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Elia?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!” Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.” Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: ‘Sauti ya mtu anaita jangwani: Nyosheni njia ya Bwana.’” Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo. Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Masiha, wala Elia, wala yule nabii, mbona wabatiza?” Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado. Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.” Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ngambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza. Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyeongea juu yake niliposema: ‘Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!’ Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.” Yohane alishuhudia hivi: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake. Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma kubatiza watu kwa maji alikuwa ameniambia: ‘Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’ Mimi nimeona na nimeshuhudia kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.” Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili. Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazameni! Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu.” Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu. Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, “Mnatafuta nini?” Nao wakamjibu, “Rabi, (yaani Mwalimu), unakaa wapi?” Yesu akawaambia, “Njoni, nanyi mtaona.” Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu. Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, “Tumemwona Masiha” (maana yake Kristo). Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa” (Kigiriki ni Petro, yaani, “Mwamba”). Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.” Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro. Naye Filipo akamkuta Nathanaeli, akamwambia, “Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti.” Naye Nathanaeli akamwuliza Filipo, “Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.” Yesu alipomwona Nathanaeli akimjia, alisema juu yake, “Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: Hamna hila ndani yake.” Naye Nathanaeli akamwuliza, “Umepataje kunijua?” Yesu akamwambia, “Ulipokuwa chini ya mtini, hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona.” Hapo Nathanaeli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!” Yesu akamwambia, “Je, umeamini kwa kuwa nimekuambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya.” Yesu akaendelea kusema, “Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu.”
Yohane 1:1-51 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua. Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Na tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wanenaje juu yako mwenyewe? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya. Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza kamba ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng'ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza. Kesho yake alimwona Yesu akija kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini ili adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nilikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenituma kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu. Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu. Tena kesho yake Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake. Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu! Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu. Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi? Akawaambia, Njooni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana na kumfuata Yesu. Huyo akamwona kwanza Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo). Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe). Kesho yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate. Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro. Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti. Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone. Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona. Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli. Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.
Yohane 1:1-51 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua. Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya. Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng’ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza. Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu. Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu. Tena siku ya pili yake Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake. Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu! Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu. Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi? Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana na kumfuata Yesu. Huyo akamwona kwanza Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo). Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe). Siku ya pili yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate. Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro. Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti. Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone. Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona. Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli. Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.
Yohane 1:1-51 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hapo mwanzo alikuwako Neno, naye huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu. Vitu vyote viliumbwa kupitia kwake, na hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa pasipo yeye. Ndani yake kulikuwa na uzima, nao huo uzima ulikuwa nuru ya watu. Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda. Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kupitia kwake watu wote waweze kuamini. Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. Nuru halisi inayomwangazia kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni. Huyo Neno alikuwako ulimwenguni, na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. Bali wote waliompokea, yaani wale walioliamini jina lake, aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu. Hawa hawakuzaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali wamezaliwa kwa mapenzi ya Mungu. Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’ ” Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema. Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Musa, lakini neema na kweli zimekuja kupitia Yesu Kristo. Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba, ndiye ambaye amemdhihirisha. Huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati viongozi wa Wayahudi waliwatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Yohana alikiri waziwazi pasipo kuficha, akasema, “Mimi si Kristo.” Wakamuuliza, “Wewe ni nani, basi? Je, wewe ni Eliya?” Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.” “Je, wewe ni yule Nabii?” Akajibu, “Hapana.” Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?” Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Bwana.’” Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo, wakamuuliza, “Kama wewe si Kristo, wala si Eliya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?” Yohana akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji, lakini kati yenu yupo mtu msiyemjua. Yeye anakuja baada yangu, nami sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.” Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ngʼambo ya Yordani, mahali Yohana alipokuwa akibatiza. Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’ Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.” Kisha Yohana akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake. Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’ Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.” Siku iliyofuata, Yohana alikuwa huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili. Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!” Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yohana akisema haya, wakamfuata Yesu. Yesu akageuka, akawaona wakimfuata, akawauliza, “Mnataka nini?” Wakamwambia, “Rabi” (maana yake “Mwalimu”), “unaishi wapi?” Yesu akawajibu, “Njooni, nanyi mtapaona!” Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yohana alisema na kumfuata Yesu. Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masiya” (yaani Kristo). Naye akamleta kwa Yesu. Yesu akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro). Siku iliyofuata Yesu aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.” Filipo alikuwa raia wa Bethsaida, mji walikotoka Andrea na Petro. Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Musa aliandika habari zake katika Sheria, na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani Yesu wa Nazareti, mwana wa Yusufu.” Nathanaeli akauliza, “Nazareti! Je, kitu chochote chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.” Yesu alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake, akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli; hana hila ndani yake.” Nathanaeli akamuuliza, “Umenifahamuje?” Yesu akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.” Nathanaeli akamwambia, “Rabi, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!” Yesu akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu kuliko hilo.” Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”