Yeremia 6:1-9
Yeremia 6:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Enyi watu wa Benyamini, ondokeni Yerusalemu mkimbilie usalama! Pigeni tarumbeta mjini Tekoa; onesheni ishara huko Beth-hakeremu, maana maafa na maangamizi makubwa yanakuja kutoka upande wa kaskazini. Mji wa Siyoni ni mzuri na mwororo, lakini utaangamizwa. Watu wataujia kama wachungaji na makundi yao, watapiga hema zao kuuzunguka kila mmoja sehemu yake, wapate kuyaongoza makundi yao. Watasema: “Jitayarisheni kuushambulia Siyoni. Haya! Tuanze kushambulia adhuhuri! Bahati mbaya; jua linatua! Kivuli cha jioni kinarefuka. Basi, tutaushambulia usiku; tutayaharibu majumba yake ya kifalme.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Kateni miti yake, rundikeni udongo kuuzingira Yerusalemu. Mji huu ni lazima uadhibiwe, maana hamna lolote ndani yake ila dhuluma. Kama kisima kinavyohifadhi maji yake yakabaki safi, ndivyo Yerusalemu unavyohifadhi uovu wako. Ukatili na uharibifu vyasikika ndani yake, magonjwa na majeraha yake nayaona daima. Hilo na liwe onyo kwako ee Yerusalemu, la sivyo nitakutupa kabisa kwa chuki; nikakufanya uwe jangwa, mahali pasipokaliwa na mtu.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Kusanyeni watu wote wa Israeli waliobaki kama watu wakusanyavyo zabibu zote; kama afanyavyo mchumazabibu, pitisheni tena mikono yenu katika matawi yake.”
Yeremia 6:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kimbieni mpate kuwa salama, enyi wana wa Benyamini; tokeni katika Yerusalemu, pigeni tarumbeta katika Tekoa, simamisheni ishara juu ya Beth-hakeremu; kwa maana mabaya yanachungulia toka kaskazini, na uharibifu mkuu. Binti Sayuni aliye mzuri, mwororo, nitamkatilia mbali. Wachungaji na makundi yao ya kondoo watamjia; watapiga hema zao karibu naye pande zote; watalisha kila mmoja mahali pake. Takaseni vita juu yake; inukeni, na tupande juu wakati wa adhuhuri. Ole wetu, kwa kuwa mchana umeanza kupungua, vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu. Inukeni, na tupande juu wakati wa usiku, tukayaharibu majumba yake. Maana BWANA wa majeshi asema hivi, Jikatieni miti, mjenge boma juu ya Yerusalemu. Mji huu ni mji unaojiwa; dhuluma tupu imo ndani yake. Kama vile kisima kitoavyo maji yake, ndivyo utoavyo uovu wake; jeuri na kuharibu kwasikiwa ndani yake; ugonjwa na jeraha zi mbele zangu daima. Uonyeke, Ee Yerusalemu, nafsi yangu, isije ikafarakana nawe; nisije nikakufanya ukiwa, nchi isiyokaliwa na watu. BWANA wa majeshi asema hivi, Wataokota mabaki ya Israeli kama mzabibu; rudisha mkono wako ndani ya vikapu, kama mchuma zabibu.
Yeremia 6:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kimbieni mpate kuwa salama, enyi wana wa Benyamini; tokeni katika Yerusalemu, pigeni tarumbeta katika Tekoa, simamisheni ishara juu ya Beth-hakeremu; kwa maana mabaya yanachungulia toka kaskazini, na uharibifu mkuu. Binti Sayuni aliye mzuri, mwororo, nitamkatilia mbali. Wachungaji na makundi yao ya kondoo watamjilia; watapiga hema zao karibu naye pande zote; watalisha kila mmoja mahali pake. Takaseni vita juu yake; inukeni, na tupande juu wakati wa adhuhuri. Ole wetu, kwa kuwa mchana umeanza kupungua, vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu. Inukeni, na tupande juu wakati wa usiku, tukayaharibu majumba yake. Maana BWANA wa majeshi asema hivi, Jikatieni miti, mfanyize boma juu ya Yerusalemu. Mji huu ni mji unaojiliwa; dhuluma tupu imo ndani yake. Kama vile kisima kitoavyo maji yake, ndivyo utoavyo uovu wake; jeuri na kuharibu kwasikiwa ndani yake; ugonjwa na jeraha zi mbele zangu daima. Uadhibishwe, Ee Yerusalemu, nafsi yangu, isije ikafarakana nawe; nisije nikakufanya ukiwa, nchi isiyokaliwa na watu. BWANA wa majeshi asema hivi, Wataokota mabaki ya Israeli kama mzabibu; rudisha mkono wako ndani ya vikapu, kama mchuma zabibu.
Yeremia 6:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Kimbieni kwa usalama wenu, enyi watu wa Benyamini! Kimbieni kutoka Yerusalemu! Pigeni tarumbeta katika Tekoa! Inueni ishara juu ya Beth-Hakeremu! Kwa kuwa maafa yanaonekana yakitoka kaskazini, na uharibifu wa kutisha. Nitamwangamiza Binti Sayuni, aliye mzuri sana na mwororo. Wachungaji pamoja na makundi yao watakuja dhidi yake; watapiga mahema yao kumzunguka, kila mmoja akichunga kundi lake mwenyewe.” “Jiandaeni kwa vita dhidi yake! Inukeni tumshambulie mchana! Lakini, ole wetu, mchana unaisha, na vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu. Kwa hiyo inukeni, tufanye mashambulizi usiku, na kuharibu ngome zake!” Hivi ndivyo asemavyo BWANA wa majeshi: “Kateni miti mjenge boma kuzingira Yerusalemu. Mji huu ni lazima uadhibiwe; umejazwa na uonevu. Kama vile kisima kinavyomwaga maji yake, ndivyo anavyomwaga uovu wake. Ukatili na maangamizi vyasikika ndani yake, ugonjwa wake na majeraha yake viko mbele yangu daima. Pokea onyo, ee Yerusalemu, la sivyo nitageukia mbali nawe na kuifanya nchi yako kuwa ukiwa, asiweze mtu kuishi ndani yake.” Hivi ndivyo asemavyo BWANA wa majeshi: “Wao na wayakusanye mabaki ya Israeli kwa uangalifu kama kwenye mzabibu; pitisha mkono wako kwenye matawi tena, kama yeye avunaye zabibu.”