Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 52:1-34

Yeremia 52:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, mkazi wa mji wa Liba. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama mabaya yote aliyotenda Yehoyakimu. Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia sana watu wa Yerusalemu na Yuda hata akawafukuza mbali naye. Sedekia alimwasi mfalme wa Babuloni. Ikawa katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, mwaka wa tisa wa kutawala kwake Sedekia, Nebukadneza mfalme wa Babuloni, alifika na jeshi lake lote kuushambulia Yerusalemu, wakauzingira kila upande. Mji uliendelea kuzingirwa mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia. Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ilikuwa kali sana mjini hata hapakuwa na chakula chochote kwa ajili ya wakazi wake. Basi, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa, nao askari walikimbia wakatoka nje ya mji wakati wa usiku wakipitia njia ya lango katikati ya kuta mbili, kwenye bustani ya mfalme, wakaenda upande wa Araba, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji wote. Waisraeli walikimbia kuelekea bonde la mto Yordani. Lakini jeshi la Wakaldayo lilimfuatia mfalme na kumteka katika tambarare za Yeriko, jeshi lake lote likatawanyika na kumwacha. Basi Wakaldayo walimteka mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babuloni, huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, naye akamhukumu. Hukohuko Ribla, mfalme wa Babuloni aliwaua wana wa Sedekia mbele ya baba yao. Aliwaua pia maofisa wote wa Yuda. Kisha aliyangoa macho ya Sedekia na kumfunga pingu, akamchukua Sedekia Babuloni na kumtia kizuizini mpaka siku alipokufa. Katika siku ya kumi ya mwezi wa tano, mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme ambaye alimtumikia mfalme wa Babuloni, aliingia Yerusalemu. Alichoma moto nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu na nyumba zote za Yerusalemu; kila nyumba kubwa ilichomwa moto. Askari wote wa Wakaldayo waliokuwa pamoja na kapteni wa walinzi, walizibomoa kuta zote zilizouzunguka mji wa Yerusalemu. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwachukua uhamishoni watu waliokuwa wamebakia mjini na wale waliokuwa wamejisalimisha kwa mfalme wa Babuloni pamoja na mafundi. Lakini Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwaacha baadhi ya watu waliokuwa maskini kabisa nchini, wawe watunza mizabibu na wakulima. Wakaldayo walivunja vipandevipande nguzo za shaba nyeusi ambazo zilikuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu pamoja na vikalio na birika kubwa la shaba nyeusi lililokuwamo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaichukua shaba nyeusi yote mpaka Babuloni. Kadhalika, walichukua vyungu, sepetu, mikasi, makarai, vijiko vikubwa na vyombo vyote vya shaba nyeusi vilivyotumiwa katika huduma ya hekalu. Pia kapteni wa walinzi wa mfalme alichukua vibakuli, vyetezo, mabirika, vyungu, vinara vya taa, vijiko vikubwa na mabakuli ya sadaka za vinywaji, vyombo hivyo vikiwa vya dhahabu au vya fedha. Kuhusu vitu Solomoni alivyotengeneza: Nguzo mbili, birika kubwa moja na sanamu za fahali kumi na mbili za shaba nyeusi ambazo zilikuwa chini ya hilo birika kubwa pamoja na vikalio, shaba nyeusi ya vitu hivi vyote ilikuwa na uzito mwingi sana. Kila moja ya nguzo hizo mbili ilikuwa na urefu wa mita 8, mzingo wake mita 5.25, na unene wa milimita 75, zote zilikuwa wazi ndani. Juu ya kila nguzo kulikuwa na kichwa cha shaba nyeusi; urefu wa kila kichwa ulikuwa mita 2 na sentimita 20. Kila kichwa kilizungushiwa mapambo ya wavu ya makomamanga, yote ya shaba nyeusi. Kulikuwa na makomamanga tisini na sita ubavuni mwa nguzo hizo; jumla ya makomamanga yote ilikuwa 100 na mapambo kandokando yake. Kisha Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, alimchukua mateka Seraya kuhani mkuu, na Sefania kuhani wa pili, pamoja na walinda mlango watatu; na kutoka mjini alimchukua ofisa mmoja ambaye alikuwa akiongoza askari vitani, pamoja na watu saba washauri wa mfalme ambao aliwakuta mjini. Kadhalika alimchukua katibu wa kamanda mkuu wa jeshi ambaye alitunza kumbukumbu za jeshi pamoja na watu mashuhuri sitini ambao aliwakuta mjini Yerusalemu. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwachukua watu hao na kuwapeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliwapiga na kuwaua watu hao huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Basi, watu wa Yuda walikwenda uhamishoni nje ya nchi yao. Ifuatayo ni idadi ya watu ambao Nebukadneza aliwachukua uhamishoni mnamo mwaka wa saba wa utawala wake: Alichukua Wayahudi 3,023; mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, alichukua kutoka Yerusalemu mateka 832; mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake Nebukadneza, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, alichukua mateka Wayahudi 745. Jumla ya mateka wote ilikuwa watu 4,600. Mnamo mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda alipopelekwa uhamishoni, siku ya ishirini na tano ya mwezi wa kumi na mbili, Evil-merodaki mfalme wa Babuloni, mwaka uleule alipofanywa mfalme, alimsamehe Yehoyakini mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani. Aliongea naye vizuri na kumpa nafasi ya heshima kuliko wafalme wengine waliokuwa pamoja naye uhamishoni huko Babuloni. Basi, Yehoyakini alibadili mavazi yake ya kifungoni, akawa anapata chakula chake daima mezani kwa mfalme. Daima alipewa posho na mfalme wa Babuloni kulingana na mahitaji yake ya kila siku, mpaka alipofariki.

Shirikisha
Soma Yeremia 52

Yeremia 52:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja hapo alipoanza kumiliki; naye akamiliki miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Hamutali, binti Yeremia wa Libna. Naye alitenda yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyatenda Yehoyakimu. Maana, kwa sababu ya hasira ya BWANA, mambo haya yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata akawaondosha wasiwe mbele za uso wake, naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli. Ikawa, katika mwaka wa tisa wa kumiliki kwake, katika mwezi wa kumi, na siku ya kumi ya mwezi huo, Nebukadneza, mfalme wa Babeli, akaja, yeye na jeshi lake lote, juu ya Yerusalemu, akapanga hema zake juu yake; nao wakajenga ngome juu yake pande zote. Basi mji huo ulizingirwa hata mwaka wa kumi na mmoja wa mfalme Sedekia. Katika mwezi wa nne, siku ya tisa ya mwezi, njaa ilizidi sana ndani ya mji, hata hapakuwa na chakula kwa watu wa nchi. Ukuta wa mji ukabomolewa, watu wote wa vita wakakimbia, wakatoka mjini usiku, kwa njia ya lango lililokuwa kati ya zile kuta mbili, karibu na bustani ya mfalme; (basi wale Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji pande zote;) wakaenda zao kwa njia ya Araba. Lakini jeshi la Wakaldayo wakamfuatia mfalme, wakampata Sedekia katika nchi tambarare ya Yeriko, na jeshi lake lote walikuwa wametawanyika na kumwacha. Nao wakamshika mfalme, wakamchukua kwa mfalme wa Babeli, aliyekuwa huko Ribla katika nchi ya Hamathi, naye akatoa hukumu juu yake. Ndipo mfalme wa Babeli akawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake; pia akawaua wakuu wote wa Yuda huko Ribla. Akampofusha macho Sedekia; tena mfalme wa Babeli akamfunga kwa pingu, akamchukua mpaka Babeli, akamtia gerezani hata siku ya kufa kwake. Basi katika mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, ndio mwaka wa kumi na tisa wa mfalme Nebukadneza, mfalme wa Babeli; Nebuzaradani, kamanda wa askari walinzi, aliyesimama mbele ya mfalme wa Babeli, aliingia Yerusalemu. Akaiteketeza nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme; na nyumba zote za Yerusalemu, naam, kila nyumba kubwa aliiteketeza kwa moto. Na jeshi lote la Wakaldayo, waliokuwa pamoja na huyo kamanda wa askari walinzi, wakazibomoa kuta zote za Yerusalemu pande zote. Kisha Nebuzaradani, kamanda wa askari walinzi, akawachukua wafungwa baadhi ya watu waliokuwa maskini, na mabaki wa watu walioachwa katika mji, nao wale walioasi na kumkimbilia mfalme wa Babeli, nao mabaki wa vibarua. Lakini Nebuzaradani, kamanda wa askari walinzi, akawaacha watu walio maskini kabisa ili wawe watunza mizabibu na wakulima. Na nguzo za shaba zilizokuwa katika nyumba ya BWANA, na vikalio vya mazulia ya shaba iliyokuwa katika nyumba ya BWANA, Wakaldayo walivivunja vipande vipande, wakaichukua shaba yake yote mpaka Babeli. Nayo masufuria, na majembe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyombo vyote vya shaba walivyokuwa wakivitumia, wakavichukua vyote. Navyo vikombe, na vyombo vya kutolea majivu, na mabakuli, na masufuria, na vinara, na miiko, na vyetezo, vilivyokuwa vya dhahabu katika dhahabu, na vilivyokuwa vya fedha katika fedha, kamanda wa askari walinzi akavichukua. Nguzo mbili, beseni, na ng'ombe kumi na mbili za shaba zilizokuwa chini ya vikalio vyake, ambavyo mfalme Sulemani aliifanyia nyumba ya BWANA; shaba ya vitu hivyo vyote ilikuwa haiwezi kupimwa kwa kuwa nyingi sana. Na nguzo hizo, urefu wa nguzo moja ulikuwa dhiraa kumi na nane, na uzi wa dhiraa kumi na mbili ungeweza kuizunguka; na unene wake ulikuwa nyanda nne; nayo ilikuwa ya uvungu. Nayo ilikuwa na kichwa cha shaba juu yake; na urefu wa kichwa kimoja ulikuwa dhiraa tano; palikuwa na mapambo ya wavu na makomamanga juu ya kichwa hicho pande zote; vyote vilikuwa vya shaba; nayo nguzo ya pili ilikuwa na mapambo kama hayo, na makomamanga. Palikuwa na makomamanga tisini na sita katika pande zake; makomamanga; yote yalikuwa mia moja juu ya wavu huo pande zote. Naye mkuu wa askari walinzi akamtwaa Seraya, kuhani mkuu, na Sefania, kuhani wa pili, na wale walinzi watatu wa mlango; na katika mji akatwaa towashi mmoja aliyewasimamia watu wa vita; na watu saba katika wale waliouona uso wa mfalme, walioonekana katika mji; na karani wa jemadari wa jeshi, aliyewaandika watu wa nchi; na watu sitini katika watu wa nchi, walioonekana ndani ya mji. Na Nebuzaradani, mkuu wa askari walinzi, akawatwaa, akawaleta kwa mfalme wa Babeli huko Ribla. Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Ndivyo Yuda alivyochukuliwa utumwani, akatolewa katika nchi yake. Watu hawa ndio wale ambao Nebukadneza aliwachukua mateka; katika mwaka wa saba, Wayahudi elfu tatu na ishirini na watatu; katika mwaka wa kumi na nane wa Nebukadneza aliwachukua toka Yerusalemu watu mia nane na thelathini na wawili; katika mwaka wa ishirini na tatu wa Nebukadneza, Nebuzaradani, mkuu wa askari walinzi, akawachukua mateka katika Wayahudi watu mia saba na arubaini na watano; jumla ya watu hao wote ni watu elfu nne na mia sita. Hata ikawa, katika mwaka wa thelathini na saba wa kuhamishwa kwake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi na mbili, siku ya ishirini na tano ya mwezi, Evil-merodaki, mfalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, akamwinua kichwa chake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani. Akasema naye maneno mazuri, akaweka kiti chake juu ya viti vya wafalme waliokuwa pamoja naye huko Babeli. Naye akabadili mavazi yake ya gerezani, akala chakula mbele yake daima, siku zote za maisha yake. Na kwa posho yake, alipewa posho ya daima na mfalme wa Babeli; kila siku alipewa posho hata siku ya kufa kwake, siku zote za maisha yake.

Shirikisha
Soma Yeremia 52

Yeremia 52:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja hapo alipoanza kumiliki; naye akamiliki miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Hamutali, binti Yeremia wa Libna. Naye alitenda yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyatenda Yehoyakimu. Maana, kwa sababu ya hasira ya BWANA, mambo haya yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata akawaondosha wasiwe mbele za uso wake, naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli. Ikawa, katika mwaka wa kenda wa kumiliki kwake, katika mwezi wa kumi, na siku ya kumi ya mwezi huo, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaja, yeye na jeshi lake lote, juu ya Yerusalemu, akapanga hema zake juu yake; nao wakajenga ngome juu yake pande zote. Basi mji huo ulihusuriwa hata mwaka wa kumi na mmoja wa mfalme Sedekia. Katika mwezi wa nne, siku ya kenda ya mwezi, njaa ilizidi sana ndani ya mji, hata hapakuwa na chakula kwa watu wa nchi. Ukuta wa mji ukabomolewa, watu wote wa vita wakakimbia, wakatoka mjini usiku, kwa njia ya lango lililokuwa kati ya zile kuta mbili, karibu na bustani ya mfalme; (basi wale Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji pande zote;) wakaenda zao kwa njia ya Araba. Lakini jeshi la Wakaldayo wakamfuatia mfalme, wakampata Sedekia katika nchi tambarare ya Yeriko, na jeshi lake lote walikuwa wametawanyika na kumwacha. Nao wakamshika mfalme, wakamchukua kwa mfalme wa Babeli, aliyekuwa huko Ribla katika nchi ya Hamathi, naye akatoa hukumu juu yake. Ndipo mfalme wa Babeli akawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake; pia akawaua wakuu wote wa Yuda huko Ribla. Akampofusha macho Sedekia; tena mfalme wa Babeli akamfunga kwa pingu, akamchukua mpaka Babeli, akamtia gerezani hata siku ya kufa kwake. Basi katika mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, ndio mwaka wa kumi na kenda wa mfalme Nebukadreza, mfalme wa Babeli; Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, aliyesimama mbele ya mfalme wa Babeli, aliingia Yerusalemu. Akaiteketeza nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme; na nyumba zote za Yerusalemu, naam, kila nyumba kubwa aliiteketeza kwa moto. Na jeshi lote la Wakaldayo, waliokuwa pamoja na huyo amiri wa askari walinzi, wakazibomoa kuta zote za Yerusalemu pande zote. Kisha Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua wafungwa baadhi ya watu waliokuwa maskini, na mabaki ya watu walioachwa katika mji, nao wale walioasi na kumkimbilia mfalme wa Babeli, nao mabaki ya vibarua. Lakini Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawaacha watu walio maskini kabisa ili wawe watunza mizabibu na wakulima. Na nguzo za shaba zilizokuwa katika nyumba ya BWANA, na matako ya bahari ya shaba iliyokuwa katika nyumba ya BWANA, Wakaldayo walivivunja vipande vipande, wakaichukua shaba yake yote mpaka Babeli. Nayo masufuria, na majembe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyombo vyote vya shaba walivyokuwa wakivitumia, wakavichukua vyote. Navyo vikombe, na vyombo vya kutolea majivu, na mabakuli, na masufuria, na vinara, na miiko, na vyetezo, vilivyokuwa vya dhahabu katika dhahabu, na vilivyokuwa vya fedha katika fedha, amiri wa askari walinzi akavichukua. Nguzo mbili, bahari moja, na ng’ombe kumi na mbili za shaba zilizokuwa chini ya matako yake, ambavyo mfalme Sulemani aliifanyia nyumba ya BWANA; shaba ya vitu hivyo vyote ilikuwa haiwezi kupimwa kwa kuwa nyingi sana. Na nguzo hizo, urefu wa nguzo moja ulikuwa dhiraa kumi na nane, na uzi wa dhiraa kumi na mbili ungeweza kuizunguka; na unene wake ulikuwa nyanda nne; nayo ilikuwa ya uvungu. Nayo ilikuwa na kichwa cha shaba juu yake; na urefu wa kichwa kimoja ulikuwa dhiraa tano; palikuwa na mapambo ya wavu na makomamanga juu ya kichwa hicho pande zote; vyote vilikuwa vya shaba; nayo nguzo ya pili ilikuwa na mapambo kama hayo, na makomamanga. Palikuwa na makomamanga tisini na sita katika pande zake; makomamanga; yote yalikuwa mia juu ya wavu huo pande zote. Naye amiri wa askari walinzi akamtwaa Seraya, kuhani mkuu, na Sefania, kuhani wa pili, na wale walinzi watatu wa mlango; na katika mji akatwaa towashi mmoja aliyewasimamia watu wa vita; na watu saba katika wale waliouona uso wa mfalme, walioonekana katika mji; na karani wa jemadari wa jeshi, aliyewaandika watu wa nchi; na watu sitini katika watu wa nchi, walioonekana ndani ya mji. Na Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawatwaa, akawaleta kwa mfalme wa Babeli huko Ribla. Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Ndivyo Yuda alivyochukuliwa utumwani, akatolewa katika nchi yake. Watu hawa ndio wale ambao Nebukadreza aliwachukua mateka; katika mwaka wa saba, Wayahudi elfu tatu na ishirini na watatu; katika mwaka wa kumi na nane wa Nebukadreza aliwachukua toka Yerusalemu watu mia nane na thelathini na wawili; katika mwaka wa ishirini na tatu wa Nebukadreza, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka katika Wayahudi watu mia saba na arobaini na watano; jumla ya watu hao wote ni watu elfu nne na mia sita. Hata ikawa, katika mwaka wa thelathini na saba wa kuhamishwa kwake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi na mbili, siku ya ishirini na tano ya mwezi, Evil-merodaki, mfalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, akamwinua kichwa chake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani. Akasema naye maneno mazuri, akaweka kiti chake juu ya viti vya wafalme waliokuwa pamoja naye huko Babeli. Naye akabadili mavazi yake ya gerezani, akala chakula mbele yake daima, siku zote za maisha yake. Na kwa posho yake, alipewa posho ya daima na mfalme wa Babeli; kila siku alipewa posho hata siku ya kufa kwake, siku zote za maisha yake.

Shirikisha
Soma Yeremia 52

Yeremia 52:1-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na moja. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia kutoka Libna. Alifanya maovu machoni pa BWANA, kama alivyofanya Yehoyakimu. Haya yote yalitendeka Yerusalemu na Yuda kwa sababu ya hasira ya BWANA, naye mwishoni akawaondoa mbele zake. Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli. Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akiwa na jeshi lake lote alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Wakapiga kambi nje ya mji na kuuzingira pande zote. Mji ulizingirwa na jeshi hadi mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia. Ilipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu. Kisha ukuta wa mji ukavunjwa na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba. Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia Mfalme Sedekia na kumpata katika nchi tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika, naye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ambapo alimtangazia hukumu. Huko Ribla mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Pia akawaua maafisa wote wa Yuda. Kisha akayangʼoa macho ya Sedekia, akamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli, alipomweka gerezani hadi siku ya kifo chake. Siku ya kumi ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme, aliyemtumikia mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu. Alichoma moto Hekalu la BWANA, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu. Jeshi lote la Wakaldayo chini ya mkuu wa askari walinzi wa mfalme walivunja kuta zote zilizoizunguka Yerusalemu. Nebuzaradani, mkuu wa askari walinzi, akawapeleka uhamishoni baadhi ya watu maskini sana na wale waliobaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli. Lakini Nebuzaradani akawaacha mabaki ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine. Wakaldayo walivunja nguzo za shaba, vishikilio vya shaba, na Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la BWANA. Kisha wakaichukua shaba yote wakaipeleka Babeli. Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika Hekaluni. Mkuu wa askari walinzi wa mfalme akachukua yale masinia, vile vyetezo, yale mabakuli ya kunyunyizia, zile sufuria, vile vinara vya taa, zile sahani na yale mabakuli yaliyotumika kwa sadaka za vinywaji, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha. Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na wale mafahali kumi na wawili wa shaba waliokuwa chini yake, pamoja na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Mfalme Sulemani alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la BWANA, ilikuwa na uzito mwingi usioweza kupimika. Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane, kimo chake na mzunguko dhiraa kumi na mbili, na unene wa nyanda nne, na zote zilikuwa wazi ndani. Sehemu ya shaba juu ya ile nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tano, na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na makomamanga yake ilifanana na hiyo ya kwanza. Kulikuwa na makomamanga tisini na sita pembeni; jumla ya makomamanga juu ya wavu uliokuwa umezunguka yalikuwa mia moja. Yule mkuu wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu. Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua afisa kiongozi wa wapiganaji, na washauri saba wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji. Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla. Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe. Hivyo Yuda wakaenda utumwani, mbali na nchi yao. Hii ndiyo hesabu ya watu ambao Nebukadneza aliwachukua kwenda uhamishoni: katika mwaka wa saba, Wayahudi elfu tatu na ishirini na watatu (3,023); katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Nebukadneza, watu mia nane na thelathini na wawili (832) kutoka Yerusalemu; katika mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake, Wayahudi mia saba na arobaini na watano (745) walichukuliwa kwenda uhamishoni na Nebuzaradani, mkuu wa askari walinzi wa mfalme. Jumla ya watu wote walikuwa elfu nne mia sita. Katika mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda apelekwe uhamishoni, katika mwaka ule ambao Evil-Merodaki alifanyika mfalme wa Babeli, alimwacha huru Yehoyakini mfalme wa Yuda, na kumfungua kutoka gerezani siku ya ishirini na tano ya mwezi wa kumi na mbili. Alizungumza naye kwa upole na kumpa kiti cha heshima kuliko wafalme wengine aliokuwa nao huko Babeli. Hivyo Yehoyakini akayavua mavazi yake ya gerezani, na siku zote za maisha yake zilizobaki alikula mezani mwa mfalme. Siku kwa siku mfalme wa Babeli alimpa Yehoyakini posho siku zote za maisha yake, hadi siku ya kifo chake.

Shirikisha
Soma Yeremia 52