Yeremia 38:1-28
Yeremia 38:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Shefatia mwana wa Matani, Gedalia mwana wa Pashuri, mwana wa Malkia, walisikia maneno ambayo Yeremia aliwatangazia watu wote akisema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Yeyote atakayebaki katika mji huu atakufa kwa vita, njaa na maradhi; lakini yule atakayeondoka na kujisalimisha kwa Wakaldayo, ataishi. Atakuwa ametekwa nyara na kuishi. Mwenyezi-Mungu asema kuwa hakika mji huu utatiwa mikononi mwa jeshi la mfalme wa Babuloni na kutekwa.” Wakuu wakamwambia mfalme, “Yafaa mtu huyu auawe kwa maana anawavunja moyo askari ambao wameachwa katika mji huu na watu wote kwa jumla, kwa kusema maneno kama hayo. Yeye hawatakii watu hawa mema bali mabaya.” Mfalme Sedekia akasema, “Haya! Mtu huyu yumo mikononi mwenu; mimi siwezi kuwapinga.” Basi, wakamchukua Yeremia wakamtumbukiza katika kisima cha Malkia mwana wa mfalme ambacho kilikuwa katika ukumbi wa walinzi. Walimshusha Yeremia ndani kwa kamba. Ndani ya kisima hicho hakukuwa na maji bali tope, naye Yeremia akazama katika tope. Lakini Ebedmeleki, towashi Mwethiopia aliyekuwa akifanya kazi katika ikulu, alipata habari kwamba walikuwa wamemtumbukiza Yeremia kisimani. Wakati huo mfalme alikuwa anabarizi penye lango la Benyamini. Basi, Ebedmeleki akamwendea mfalme, akamwambia, “Bwana wangu mfalme, watu hawa wamefanya kitu kibaya. Wamemtumbukiza yule nabii Yeremia kisimani ambamo kwa kweli atakufa kwa njaa, kwa maana hamna chakula tena mjini.” Hapo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mwethiopia: “Chukua watu watatu kutoka hapa uende ukamtoe nabii Yeremia kisimani, kabla hajafa.” Basi, Ebedmeleki akawachukua watu hao na kwenda pamoja nao ikulu kwa mfalme, wakaingia katika ghala ya ikulu; Ebedmeleki akatwaa nguo zilizotumika na matambara makuukuu, akamteremshia Yeremia kisimani kwa kamba. Kisha Ebedmeleki, Mwethiopia, akamwambia Yeremia, “Weka hayo matambara kwapani mwako, kisha pitisha kamba hizo chini ya matambara hayo.” Yeremia akafanya hivyo. Kisha wakamvuta Yeremia kwa kamba, wakamtoa kisimani. Baada ya hayo, Yeremia akaendelea kukaa katika ukumbi wa walinzi. Wakati fulani mfalme Sedekia alitaka kumwona nabii Yeremia. Basi, akaagiza Yeremia aletwe kwenye mlango wa tatu wa hekalu la Mwenyezi-Mungu. Huko, mfalme alimwambia Yeremia, “Nataka kukuuliza jambo fulani; usinifiche kitu chochote.” Yeremia akamjibu Sedekia, “Je, nikikuambia ukweli hutaniua? Na kama nikikushauri, hutanisikiliza.” Hapo, mfalme Sedekia alimwapia Yeremia kwa siri akisema, “Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu aliyetupa uhai, sitakuua wala sitakutia mikononi mwa hawa wanaotaka kukuua.” Hapo Yeremia akamwambia Sedekia: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Kama ukijitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, utayaokoa maisha yako na mji hautateketezwa kwa moto; nawe pamoja na jamaa yako mtaendelea kuishi. Lakini usipojitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, basi, mji huu utatekwa na Wakaldayo nao watauteketeza kwa moto, nawe hutaweza kujiepusha mikononi mwao.” Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, “Nawaogopa Wayahudi waliokimbilia kwa Wakaldayo. Huenda nikakabidhiwa kwao, wakanitesa.” Yeremia akamjibu, “Hutakabidhiwa kwao. Wewe sasa tii anachosema Mwenyezi-Mungu, kama ninavyokuambia, na mambo yote yatakuendea vema, na maisha yako yatasalimika. Lakini kama ukikataa kujitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwao, haya ndiyo maono ambayo Mwenyezi-Mungu amenionesha. Katika maono hayo, niliona wanawake waliobaki katika ikulu ya mfalme wa Yuda wakipelekwa kwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, nao walikuwa wakisema hivi: ‘Marafiki zako uliowaamini wamekudanganya, nao wamekushinda; kwa kuwa miguu yako imezama matopeni, wamekugeuka na kukuacha.’ Wake zako wote na watoto wako watapelekwa kwa Wakaldayo, nawe mwenyewe hutanusurika. Utachukuliwa mateka na mfalme wa Babuloni na mji huu utateketezwa kwa moto.” Sedekia akamwambia Yeremia: “Mtu yeyote asijue habari hizi, nawe hutauawa. Kama viongozi wakisikia kuwa nimeongea nawe, kisha wakaja na kukuambia, ‘Hebu tuambie, ulizungumza nini na mfalme. Usitufiche chochote nasi hatutakuua’; wewe utawaambia hivi: ‘Nilikuwa ninamsihi mfalme kwa unyenyekevu asinirudishe gerezani nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafia huko.’” Kisha, viongozi walimjia Yeremia wakamwuliza mambo hayo, naye akawajibu kama mfalme alivyomwelekeza. Ndipo walipoacha kuzungumza naye kwa sababu hakuna mtu aliyekuwa amesikia mazungumzo yake na mfalme. Yeremia alibaki katika ukumbi wa walinzi mpaka siku mji wa Yerusalemu ulipotekwa.
Yeremia 38:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na Shefatia, mwana wa Matani, na Gedalia, mwana wa Pashuri, na Yukali, mwana wa Shelemia, na Pashuri, mwana wa Malkiya, wakayasikia maneno ambayo Yeremia aliwaambia watu wote, akisema, BWANA asema hivi, Akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; bali yeye atokaye kwenda kwa Wakaldayo ataishi, naye atapewa maisha yake yawe kama nyara, naye ataishi. BWANA asema hivi, Bila shaka mji huu utatiwa katika mikono ya jeshi la mfalme wa Babeli, naye atautwaa. Ndipo wakuu wakamwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri, bali shari. Naye mfalme Sedekia akasema, Tazama, yuko mikononi mwenu; maana mfalme siye awezaye kufanya neno lolote kinyume chenu. Basi wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo katika ukumbi wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo. Basi, Ebedmeleki, Mkushi, towashi, aliyekuwa katika nyumba ya mfalme, aliposikia kwamba wamemtia Yeremia shimoni; na wakati huo mfalme alikuwa amekaa katika lango la Benyamini; Ebedmeleki akatoka nyumbani mwa mfalme, akamwambia mfalme, akisema, Ee bwana wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika mambo yote waliyomtenda Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi atakufa pale alipo, kwa sababu ya njaa; kwa kuwa hakuna mkate kabisa katika mji. Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mkushi, akisema, Chukua pamoja nawe watu thelathini toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla hajafa. Basi Ebedmeleki akawachukua watu hao pamoja naye, akaingia ndani ya nyumba ya mfalme chini ya ghala, akatoa mle nguo zilizotupwa, na vitambaa vikuukuu, akamteremshia Yeremia shimoni kwa kamba. Naye Ebedmeleki, Mkushi, akamwambia Yeremia, Tia nguo hizi zilizotupwa, na vitambaa hivi vikuukuu, chini ya kamba kwapani. Naye Yeremia akafanya hivyo. Basi wakamwinua Yeremia kwa kamba hizo, wakamtoa shimoni; naye Yeremia akakaa katika ukumbi wa walinzi. Kisha mfalme Sedekia akatuma watu, akamleta nabii Yeremia kwake, ndani ya maingilio ya tatu ya nyumba ya BWANA; mfalme akamwambia Yeremia, Nataka kukuuliza neno, nawe usinifiche neno lolote. Basi Yeremia akamwambia Sedekia, Kama nikikufunulia neno hilo, je! Hutaniua wewe? Tena, mimi nikikupa ushauri wewe hutanisikiliza. Basi Sedekia mfalme akamwapia Yeremia kwa siri, akisema, Kama BWANA aishivyo, yeye aliyetupa roho zetu, sitakuua, wala sitakutia katika mikono ya watu hao wanaokutafuta wakuue. Ndipo Yeremia akamwambia Sedekia, BWANA, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama ukitoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi nafsi yako utaishi, wala mji huu hautateketezwa; nawe utaishi na nyumba yako; bali ukikataa kutoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi, mji huu utatiwa katika mikono ya Wakaldayo nao watauteketeza, hata na wewe hutajiepusha na mikono yao. Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, Nawaogopa Wayahudi waliowakimbilia Wakaldayo, wasije wakanitia katika mikono yao, nao wakanidhihaki. Lakini Yeremia akasema, La! Hawatakutoa. Nakusihi, uitii sauti ya BWANA katika hayo ninayokuambia; ndivyo itakavyokufaa, na nafsi yako utaishi. Lakini kama ukikataa kutoka, hili ndilo neno ambalo BWANA amenionesha; Tazama, wanawake wote, walioachwa ndani ya nyumba ya mfalme wa Yuda, watatolewa na kuchukuliwa kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, na wanawake hao watasema, Rafiki zako walio karibu wamekudanganya, nao wamekushinda; na kwa kuwa miguu yako imezama matopeni sasa, wamegeuka na kurudi nyuma. Na watawatoa wake zako, na watoto wako wote, na kuwachukua kwa Wakaldayo; wala wewe hutapona na mikono yao, bali utakamatwa kwa mkono wa mfalme wa Babeli, nawe utakuwa sababu ya kuteketezwa mji huu. Ndipo Sedekia akamwambia Yeremia, Mtu yeyote asipate habari ya maneno haya, nawe hutakufa. Lakini kama wakuu wakisikia ya kuwa nimenena nawe, nao wakija kwako, na kukuambia, Tufunulie sasa uliyomwambia mfalme; usimfiche, nasi hatutakuua; na pia uliyoambiwa na mfalme; basi, utawaambia, Nilimwomba mfalme asinirudishe nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafa humo. Ndipo wakuu wakamwendea Yeremia, wakamwuliza; naye akawaambia sawasawa na maneno aliyoamriwa na mfalme. Basi wakaacha kunena naye; maana neno lile halikujulikana. Basi Yeremia akakaa katika ukumbi wa walinzi hadi siku ile Yerusalemu ulipotwaliwa.
Yeremia 38:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na Shefatia, mwana wa Matani, na Gedalia, mwana wa Pashuri, na Yukali, mwana wa Shelemia, na Pashuri, mwana wa Malkiya, wakayasikia maneno ambayo Yeremia aliwaambia watu wote, kusema, BWANA asema hivi, Akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; bali yeye atokaye kwenda kwa Wakaldayo ataishi, naye atapewa maisha yake yawe kama nyara, naye ataishi. BWANA asema hivi, Bila shaka mji huu utatiwa katika mikono ya jeshi la mfalme wa Babeli, naye atautwaa. Ndipo wakuu wakamwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri, bali shari. Naye mfalme Sedekia akasema, Tazama, yu mikononi mwenu; maana mfalme siye awezaye kufanya neno lo lote kinyume chenu. Basi wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo katika uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo. Basi, Ebedmeleki, Mkushi, towashi, aliyekuwa katika nyumba ya mfalme, aliposikia kama wamemtia Yeremia shimoni; na wakati huo mfalme alikuwa amekaa katika lango la Benyamini; Ebedmeleki akatoka nyumbani mwa mfalme, akamwambia mfalme, akisema, Ee bwana wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika mambo yote waliyomtenda Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi atakufa pale alipo, kwa sababu ya njaa; kwa kuwa hapana mkate kabisa katika mji. Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mkushi, akisema, Chukua pamoja nawe watu thelathini toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla hajafa. Basi Ebedmeleki akawachukua watu hao pamoja naye, akaingia ndani ya nyumba ya mfalme chini ya ghala, akatoa mle nguo zilizotupwa, na vitambaa vikuukuu, akamtelemshia Yeremia shimoni kwa kamba. Naye Ebedmeleki, Mkushi, akamwambia Yeremia, Tia nguo hizi zilizotupwa, na vitambaa hivi vikuukuu, chini ya kamba kwapani. Naye Yeremia akafanya hivyo. Basi wakamwinua Yeremia kwa kamba hizo, wakamtoa shimoni; naye Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi. Kisha mfalme Sedekia akatuma watu, akamleta nabii Yeremia kwake, ndani ya maingilio ya tatu ya nyumba ya BWANA; mfalme akamwambia Yeremia, Nataka kukuuliza neno, nawe usinifiche neno lo lote. Basi Yeremia akamwambia Sedekia, Kama nikikufunulia neno hilo, je! Hutaniua wewe? Tena, mimi nikikupa shauri wewe hutanisikiliza. Basi Sedekia mfalme akamwapia Yeremia kwa siri, akisema, Kama BWANA aishivyo, yeye aliyetufanyia roho zetu, sitakuua, wala sitakutia katika mikono ya watu hao wanaokutafuta wakuue. Ndipo Yeremia akamwambia Sedekia, BWANA, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama ukitoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi nafsi yako utaishi, wala mji huu hautateketezwa; nawe utaishi na nyumba yako; bali ukikataa kutoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi, mji huu utatiwa katika mikono ya Wakaldayo nao watauteketeza, hata na wewe hutajiepusha na mikono yao. Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, Nawaogopa Wayahudi waliowakimbilia Wakaldayo, wasije wakanitia katika mikono yao, nao wakanidhihaki. Lakini Yeremia akasema, La! Hawatakutoa. Nakusihi, uitii sauti ya BWANA katika hayo ninayokuambia; ndivyo itakavyokufaa, na nafsi yako utaishi. Lakini kama ukikataa kutoka, hili ndilo neno ambalo BWANA amenionyesha; Tazama, wanawake wote, walioachwa ndani ya nyumba ya mfalme wa Yuda, watatolewa na kuchukuliwa kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, na wanawake hao watasema, Rafiki zako walio karibu wamekudanganya, nao wamekushinda; na kwa kuwa miguu yako imezama matopeni sasa, wamegeuka na kurudi nyuma. Na watawatoa wake zako, na watoto wako wote, na kuwachukua kwa Wakaldayo; wala wewe hutapona na mikono yao, bali utakamatwa kwa mkono wa mfalme wa Babeli, nawe utakuwa sababu ya kuteketezwa mji huu. Ndipo Sedekia akamwambia Yeremia, Mtu ye yote asipate habari ya maneno haya, nawe hutakufa. Lakini kama wakuu wakisikia ya kuwa nimenena nawe, nao wakija kwako, na kukuambia, Tufunulie sasa uliyomwambia mfalme; usimfiche, nasi hatutakuua; na pia uliyoambiwa na mfalme; basi, utawaambia, Nalimwomba mfalme asinirudishe nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafa humo. Ndipo wakuu wakamwendea Yeremia, wakamwuliza; naye akawaambia sawasawa na maneno aliyoamriwa na mfalme. Basi wakaacha kunena naye; maana neno lile halikujulikana. Basi Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi hata siku ile Yerusalemu ulipotwaliwa.
Yeremia 38:1-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Shefatia mwana wa Matani, na Gedalia mwana wa Pashuri, na Yehukali mwana wa Shelemia, na Pashuri mwana wa Malkiya wakasikia kile Yeremia alichokuwa akiwaambia watu wote aliposema, “Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Yeyote akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, njaa au tauni, lakini yeyote atakayejisalimisha kwa Wakaldayo ataishi. Atakayeyatoa maisha yake kama nyara, ataishi.’ Tena hili ndilo asemalo BWANA: ‘Mji huu kwa hakika utatiwa mikononi mwa jeshi la mfalme wa Babeli, ambaye atauteka.’ ” Ndipo maafisa wakamwambia mfalme, “Mtu huyu imempasa kuuawa. Anawakatisha tamaa askari waliobaki katika mji huu na watu wote kutokana na mambo anayowaambia. Mtu huyu hawatakii mema watu hawa, bali maangamizi yao.” Mfalme Sedekia akajibu, “Yeye yuko mikononi mwenu! Mfalme hawezi kufanya lolote kuwapinga ninyi.” Basi wakamchukua Yeremia na kumtia kwenye kisima cha Malkiya, mwana wa mfalme, kilichokuwa katika ua wa walinzi. Wakamteremsha Yeremia kwa kamba ndani ya kisima. Hakikuwa na maji ndani yake, ila tope tu, naye Yeremia akazama ndani ya matope. Lakini Ebed-Meleki Mkushi, aliyekuwa afisa katika jumba la kifalme, akasikia kuwa walikuwa wamemtia Yeremia ndani ya kisima. Mfalme alipokuwa ameketi katika Lango la Benyamini, Ebed-Meleki akatoka nje ya jumba la kifalme na kumwambia, “Mfalme bwana wangu, watu hawa wamefanya uovu kwa yote waliomtendea nabii Yeremia. Wamemtupa ndani ya kisima, ambamo atakufa kwa njaa chakula kitakapokosekana katika mji.” Basi mfalme akamwamuru Ebed-Meleki Mkushi, akisema, “Chukua watu thelathini kutoka hapa pamoja nawe, mkamtoe nabii Yeremia huko kwenye kisima kabla hajafa.” Basi Ebed-Meleki akawachukua watu pamoja naye, wakaenda kwenye chumba kilicho chini ya hazina, ndani ya jumba la kifalme. Akachukua matambaa makuukuu pamoja na nguo zilizochakaa kutoka huko, na kumshushia Yeremia kwa kamba ndani ya kisima. Ebed-Meleki Mkushi akamwambia Yeremia, “Weka haya matambaa makuukuu na hizo nguo zilizochakaa makwapani ili kuzuia kamba.” Yeremia akafanya hivyo, nao wakamvuta juu kwa kamba na kumtoa katika kisima. Yeremia akakaa katika ua wa walinzi. Ndipo Mfalme Sedekia akatuma watu wamwitie nabii Yeremia wamlete kwake kwenye ingilio la tatu la Hekalu la BWANA. Mfalme akamwambia Yeremia, “Ninataka kukuuliza jambo fulani, usinifiche kitu chochote.” Yeremia akamwambia Sedekia, “Nikikupa jibu, je, hutaniua? Hata nikikupa ushauri, wewe hutanisikiliza.” Lakini Mfalme Sedekia akamwapia Yeremia kiapo hiki kwa siri, akisema, “Hakika kama BWANA aishivyo, ambaye ametupatia pumzi, sitakuua wala sitakutia mikononi mwa wale wanaotafuta uhai wako.” Kisha Yeremia akamwambia Sedekia, “Hili ndilo asemalo BWANA Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli: ‘Ikiwa utajisalimisha kwa maafisa wa mfalme wa Babeli, maisha yako yatasalimika, na mji huu hautateketezwa kwa moto. Pia wewe na jamaa yako mtaishi. Lakini ikiwa hutajisalimisha kwa maafisa wa jeshi la mfalme wa Babeli, mji huu utatiwa mikononi mwa Wakaldayo; nao watauteketeza kwa moto, nawe mwenyewe hutaweza kujiokoa mikononi mwao.’ ” Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, “Ninawaogopa Wayahudi ambao wamekimbilia kwa Wakaldayo, kwa kuwa Wakaldayo wanaweza kunitia mikononi mwao, nao wakanitenda vibaya.” Yeremia akajibu, “Hawatakutia mikononi mwao. Mtii BWANA kwa kufanya kile ninachokuambia. Kisha utafanikiwa na maisha yako yatakuwa salama. Lakini ukikataa kujisalimisha, hili ndilo BWANA alilonifunulia: Wanawake wote walioachwa katika jumba la kifalme la mfalme wa Yuda wataletwa mbele ya maafisa wa mfalme wa Babeli. Wanawake hao watakuambia: “ ‘Walikupotosha na kukushinda, wale rafiki zako uliowaamini. Miguu yako imezama matopeni; rafiki zako wamekuacha.’ “Wake zako wote na watoto wataletwa na kutiwa mikononi mwa Wakaldayo. Wewe mwenyewe hutaweza kujiokoa mikononi mwao. Lakini utatekwa na mfalme wa Babeli, na mji huu utateketezwa kwa moto.” Kisha Sedekia akamwambia Yeremia, “Usiruhusu mtu yeyote ajue kuhusu haya mazungumzo, la sivyo utakufa. Maafisa wakisikia kwamba nimezungumza nawe, nao wakakujia na kusema, ‘Tuambie kile ulichozungumza na mfalme na kile mfalme alichokuambia, usitufiche au sivyo tutakuua,’ basi waambie, ‘Nilikuwa ninamsihi mfalme asinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani nisije nikafia humo.’ ” Viongozi wote wakamjia Yeremia na kumuuliza, naye Yeremia akawaambia kila kitu mfalme alichomwagiza kusema. Kisha hawakusema lolote zaidi na Yeremia kwa sababu hakuna hata mmoja aliyekuwa amesikia mazungumzo yake na mfalme. Naye Yeremia akabaki katika ua wa walinzi hadi siku Yerusalemu ilipotekwa.