Yeremia 37:6-16
Yeremia 37:6-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndipo neno la Mwenyezi-Mungu likamjia nabii Yeremia: “Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Utamwambia hivi mfalme wa Yuda ambaye amekutuma uniombe kwa niaba yake: Tazama! Jeshi la Farao lililokuja kukusaidia, liko karibu kurudi makwao Misri. Na Wakaldayo watarudi kuushambulia mji huu. Watauteka mji na kuuteketeza kwa moto. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba msijidanganye wenyewe na kusema kwamba jeshi la Wakaldayo litaondoka; kweli halitaondoka. Hata kama mkilishinda jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki majeruhi tu katika mahema yao, majeruhi hao watainuka na kuuteketeza mji huu kwa moto.” Jeshi la Wakaldayo lilipoondoka Yerusalemu kuliepa jeshi la Farao lililokuwa linakaribia, Yeremia aliondoka Yerusalemu kwenda nchi ya Benyamini ili kupokea sehemu ya urithi wake. Alipokuwa katika lango la Benyamini, mlinzi mmoja aitwaye Iriya mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania, alimkamata Yeremia na kumwambia, “Wewe unatoroka uende kujiunga na Wakaldayo!” Yeremia akamwambia, “Huo ni uongo! Mimi sitoroki na kwenda kujiunga na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakusadiki maneno ya Yeremia. Basi akamtia nguvuni na kumpeleka kwa maofisa. Maofisa hao walimkasirikia sana Yeremia wakampiga, kisha wakamfunga gerezani katika nyumba ya katibu Yonathani iliyokuwa imegeuzwa kuwa gereza. Yeremia alipokuwa amefungwa gerezani kwa muda wa siku nyingi
Yeremia 37:6-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo neno la BWANA likamjia nabii Yeremia, kusema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mtamwambia hivi mfalme wa Yuda, aliyewatuma kwangu kuniuliza; Angalieni, jeshi la Farao, ambalo linakuja kuwasaidia, litarudi Misri, nchi yao wenyewe. Na Wakaldayo watakuja tena, na kupigana na mji huu; nao watautwaa, na kuuteketeza. BWANA asema hivi, Msijidanganye mkisema, Bila shaka Wakaldayo watatuacha na kwenda zao; maana hawatawaacha. Maana mngelipiga jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki kati yao watu waliojeruhiwa tu, hata hivyo wangeondoka kila mtu katika hema yake, na kuuteketeza mji huu. Hata ikawa, jeshi la Wakaldayo lilipokuwa limevunja kambi yao mbele ya Yerusalemu, kwa kuliogopa jeshi la Farao, ndipo Yeremia akatoka Yerusalemu, ili aende mpaka katika nchi ya Benyamini, alipokee huko fungu lake kati ya watu. Naye alipokuwa katika lango la Benyamini, mkuu wa walinzi alikuwapo, jina lake Iriya, mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania; akamkamata Yeremia, nabii, akisema, Unakwenda kujiunga na Wakaldayo. Ndipo Yeremia akasema, Ni uongo, siendi kujiunga na Wakaldayo; lakini yeye asimwamini; basi Iriya akamkamata Yeremia, akamleta kwa wakuu. Nao wakuu wakamkasirikia Yeremia, wakampiga, wakamtia gerezani katika nyumba ya Yonathani, mwandishi; kwa maana ndiyo waliyoifanya kuwa gereza. Basi, Yeremia alipokuwa ameingia katika nyumba ya shimo, na katika vyumba vya ndani; na Yeremia alipokuwa amekaa humo siku nyingi
Yeremia 37:6-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo neno la BWANA likamjia nabii Yeremia, kusema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mtamwambia hivi mfalme wa Yuda, aliyewatuma kwangu kuniuliza; Angalieni, jeshi la Farao, ambalo linakuja kuwasaidia, litarudi Misri, nchi yao wenyewe. Na Wakaldayo watakuja tena, na kupigana na mji huu; nao watautwaa, na kuuteketeza. BWANA asema hivi, Msijidanganye mkisema, Bila shaka Wakaldayo watatuacha na kwenda zao; maana hawatawaacha. Maana mngelipiga jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki kati yao watu waliojeruhiwa tu, hata hivyo wangeondoka kila mtu katika hema yake, na kuuteketeza mji huu. Hata ikawa, jeshi la Wakaldayo lilipokuwa limevunja kambi yao mbele ya Yerusalemu, kwa kuliogopa jeshi la Farao, ndipo Yeremia akatoka Yerusalemu, ili aende mpaka nchi ya Benyamini, alipokee huko fungu lake kati ya watu. Naye alipokuwa katika lango la Benyamini, akida wa walinzi alikuwapo, jina lake Iriya, mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania; akamkamata Yeremia, nabii, akisema, Unakwenda kujiunga na Wakaldayo. Ndipo Yeremia akasema, Ni uongo, siendi kujiunga na Wakaldayo; lakini yeye asimsadiki; basi Iriya akamkamata Yeremia, akamleta kwa wakuu. Nao wakuu wakamkasirikia Yeremia, wakampiga, wakamtia gerezani katika nyumba ya Yonathani, mwandishi; kwa maana ndiyo waliyoifanya kuwa gereza. Basi, Yeremia alipokuwa ameingia katika nyumba ya shimo, na katika vyumba vya ndani; na Yeremia alipokuwa amekaa humo siku nyingi
Yeremia 37:6-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo neno la BWANA likamjia nabii Yeremia kusema: “Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli: Mwambie mfalme wa Yuda aliyekutuma uniulize mimi, ‘Jeshi la Farao lililokuja kukusaidia litarudi katika nchi yake yenyewe, yaani Misri. Kisha Wakaldayo watarudi na kushambulia mji huu, watauteka na kuuchoma moto.’ “Hili ndilo asemalo BWANA: Msijidanganye wenyewe mkifikiri, ‘Hakika Wakaldayo watatuacha na kwenda zao.’ Hakika hawatawaacha! Hata kama mngelishinda jeshi lote la Wakaldayo linalowashambulia ninyi, na wakawa ni watu waliojeruhiwa tu waliobaki kwenye mahema yao, wangetoka na kuuchoma mji huu moto.” Baada ya jeshi la Wakaldayo kujiondoa kutoka Yerusalemu kwa sababu ya jeshi la Farao, Yeremia akaondoka mjini kwenda nchi ya Benyamini ili akapate huko sememu yake ya milki miongoni mwa watu. Lakini alipofika kwenye Lango la Benyamini, mkuu wa walinzi aliyeitwa Iriya mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania, akamkamata Yeremia na kusema, “Wewe unaenda kujiunga na Wakaldayo!” Yeremia akasema, “Hiyo si kweli, mimi sijiungi na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakumsikiliza; badala yake, akamkamata Yeremia na kumpeleka kwa maafisa. Wakamkasirikia Yeremia, wakaamuru apigwe, na akafungwa katika nyumba ya Yonathani mwandishi waliyokuwa wameifanya kuwa gereza. Yeremia akawekwa kwenye chumba kilichofukuliwa chini, kilichojengwa kwa zege ndani ya gereza chini ya ngome, akakaa huko kwa muda mrefu.