Yeremia 27:1-7
Yeremia 27:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwanzoni mwa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Yeremia, jitengenezee kamba na nira ujivike shingoni. Kisha, peleka ujumbe kwa mfalme wa Edomu, mfalme wa Moabu, mfalme wa Amoni, mfalme wa Tiro na mfalme wa Sidoni, kupitia kwa wajumbe waliokuja Yerusalemu kumwona Sedekia mfalme wa Yuda. Waamuru wajumbe hao wawaambie wakuu wao kwamba mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Mimi ndimi niliyeiumba dunia, watu na wanyama waliomo kwa uwezo wangu na kwa mkono wangu wenye nguvu, nami humpa mtu yeyote kama nionavyo mimi kuwa sawa. Sasa nimemkabidhi mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babuloni, nchi hizi zote; kadhalika nimempa wanyama wa porini wamtumikie. Mataifa yote yatamtumikia yeye, mwanawe na mjukuu wake, mpaka wakati nchi yake itakapoanguka. Kisha mataifa mengi na wafalme wengi watamfanya kuwa mtumwa wao.
Yeremia 27:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema, BWANA ameniambia hivi, Jitengenezee vifungo na nira, ukajivike shingoni; kisha uvipeleke kwa mfalme wa Edomu, na mfalme wa Moabu, na mfalme wa wana wa Amoni, na mfalme wa Tiro, na mfalme wa Sidoni, kwa mikono ya wajumbe watakaofika Yerusalemu kwa Sedekia, mfalme wa Yuda. Uwaagize waende kwa bwana zao, na kuwaambia, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mtawaambia bwana zenu maneno haya; Mimi nimeiumba dunia hii, wanadamu na wanyama walio katika nchi, kwa uweza wangu mkuu, na kwa mkono wangu ulionyoshwa; nami nawapa watu kama inipendezavyo. Na sasa nimetia nchi hizi zote katika mkono wa Nebukadneza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu; na wanyama pori pia nimempa wamtumikie. Na mataifa yote watamtumikia yeye, na mwanawe, na mwana wa mwanawe, hata utakapowadia wakati wa nchi yake mwenyewe, ndipo mataifa mengi na wafalme wakuu watamtumikisha yeye.
Yeremia 27:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema, BWANA ameniambia hivi, Jifanyizie vifungo na nira, ukajivike shingoni; kisha uvipeleke kwa mfalme wa Edomu, na mfalme wa Moabu, na mfalme wa wana wa Amoni, na mfalme wa Tiro, na mfalme wa Sidoni, kwa mikono ya wajumbe watakaofika Yerusalemu kwa Sedekia, mfalme wa Yuda. Uwaagize waende kwa bwana zao, na kuwaambia, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mtawaambia bwana zenu maneno haya; Mimi nimeiumba dunia hii, wanadamu na wanyama walio juu ya uso wa nchi, kwa uweza wangu mkuu, na kwa mkono wangu ulionyoshwa; nami nawapa watu kama inipendezavyo. Na sasa nimetia nchi hizi zote katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu; na wanyama wa mwituni pia nimempa wamtumikie. Na mataifa yote watamtumikia yeye, na mwanawe, na mwana wa mwanawe, hata utakapowadia wakati wa nchi yake mwenyewe, ndipo mataifa mengi na wafalme wakuu watamtumikisha yeye.
Yeremia 27:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa BWANA: Hili ndilo BWANA aliloniambia: “Tengeneza nira, ujivike shingoni mwako, uifunge kwa kamba za ngozi. Kisha utume ujumbe kwa wafalme wa Edomu, Moabu, Amoni, Tiro na Sidoni kupitia wajumbe ambao wamekuja Yerusalemu kwa Sedekia mfalme wa Yuda. Wape ujumbe kwa ajili ya mabwana zao na uwaambie: Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli: ‘Waambieni hivi mabwana zenu: Kwa uwezo wangu mkuu na kwa mkono wangu ulionyooka nimeumba dunia na watu wake na wanyama walio ndani yake, nami humpa yeyote ninayependa. Sasa nitazitia nchi zenu zote mkononi mwa mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli, na nitawafanya hata wanyama pori wamtumikie. Mataifa yote yatamtumikia yeye, pamoja na mwanawe, na mjukuu wake, hadi wakati wa nchi yake utakapowadia, kisha mataifa mengi na wafalme wenye nguvu nyingi watamshinda.