Yeremia 25:1-14
Yeremia 25:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo mwaka wa nne wa utawala wa mfalme Yehoyakimu mwana wa Yosia, katika Yuda, Mwenyezi-Mungu alinimpa mimi Yeremia ujumbe kuhusu watu wa Yuda. Mwaka huo ulikuwa wa kwanza wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babuloni. Mimi Yeremia niliwaambia ujumbe huo watu wote wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu: “Kwa muda wa miaka ishirini na mitatu sasa, yaani tangu mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa mfalme Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, mpaka hivi leo, nimekuwa nikipata neno la Mungu na kuwaambieni kila wakati, lakini nyinyi hamkusikiliza. Hamkutaka kusikiliza wala hamkutega sikio msikie, ingawa Mwenyezi-Mungu aliwaleteeni watumishi wake manabii kila wakati, wakawaambieni kwamba kila mmoja wenu aachane na mwenendo wake mwovu na matendo yake mabaya, ili mpate kuishi katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu amewapa nyinyi na wazee wenu tangu zamani, muimiliki milele. Mwenyezi-Mungu aliwaonya Mmsifuate miungu mingine wala kuitumikia na kumkasirisha Mungu kwa kuabudu sanamu ambazo mmejitengenezea wenyewe. Kama Mmkimtii Mwenyezi-Mungu basi, yeye hatawaadhibu. Lakini Mwenyezi-Mungu asema kuwa nyinyi mlikataa kumsikiliza. Badala yake, mlimkasirisha kwa sanamu mlizojitengenezea wenyewe, na hivyo mkajiletea madhara nyinyi wenyewe. “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: “Kwa kuwa hamkuyatii maneno yangu, basi, nitayaita makabila yote ya kaskazini, pamoja na mtumishi wangu Nebukadneza, mfalme wa Babuloni. Nitawaleta waishambulie nchi hii na wakazi wake pamoja na mataifa yote ya jirani. Nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kuwa kitu cha kuchukiza, kuzomewa na kudharauliwa milele. Tena, nitakomesha miongoni mwao sauti za furaha, sauti za bwana arusi na bibi arusi. Sauti za kusaga hazitakuwapo, wala mwanga wa taa. Nchi hii yote itakuwa magofu matupu na ukiwa, na mataifa ya jirani yatamtumikia mfalme wa Babuloni kwa muda wa miaka sabini. Kisha baada ya miaka hiyo sabini kukamilika nitamwadhibu mfalme wa Babuloni pamoja na taifa hilo. Nitaiangamiza nchi hiyo ya Wakaldayo kwa sababu ya uovu wao na kuifanya nchi iwe magofu milele. Nitailetea nchi hiyo mambo yote niliyotamka dhidi yake na yote yaliyoandikwa katika kitabu hiki ambayo Yeremia alitabiri dhidi ya mataifa yote. Wababuloni nao itawalazimu kuwa watumwa wa mataifa mengine na wafalme wengine. Nitawaadhibu kadiri ya maovu yao waliyotenda.”
Yeremia 25:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, katika habari za watu wote wa Yuda; katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda mwaka ule ndio mwaka wa kwanza wa Nebukadneza, mfalme wa Babeli; ambalo Yeremia, nabii, aliwaambia watu wote wa Yuda, na wenyeji wote wa Yerusalemu, kusema, Tangu mwaka wa kumi na tatu wa kutawala kwake Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, hata siku hii ya leo, miaka hii ishirini na mitatu, neno la BWANA limenijia, nami nimesema nanyi, nikiamka mapema na kusema; lakini ninyi hamkusikiliza. Naye BWANA ametuma kwenu watumishi wake wote, hao manabii, akiamka mapema na kuwatuma, lakini ninyi hamkusikiliza, wala hamkutega masikio yenu, msikilize. Akasema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya; uacheni uovu wa matendo yenu, mkae katika nchi ambayo BWANA aliwapa, ninyi na baba zenu, tangu zamani za kale na hata milele; wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia na kuwasujudia, wala msinikasirishe kwa kazi ya mikono yenu; basi, mimi sitawadhuru ninyi kwa dhara lolote. Lakini ninyi hamkunisikiliza, asema BWANA; ili mnikasirishe kwa kazi ya mikono yenu, na kujidhuru nafsi zenu. Basi BWANA wa majeshi asema hivi, Kwa kuwa hamkuyasikiliza maneno yangu, angalieni, nitatuma watu na kuzitwaa jamaa zote za upande wa kaskazini, asema BWANA, nami nitatuma ujumbe kwa Nebukadneza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu, nami nitawaleta juu ya nchi hii, na juu yao wakaao ndani yake, na juu ya mataifa haya yote yaliyoko pande zote; nami nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kitu cha kushangaza, na kitu cha kuzomewa, na ukiwa wa daima. Tena, nitawaondolea sauti ya kicheko, na sauti ya furaha, sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na nuru ya mishumaa. Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo mataifa haya yatamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini. Na itakuwa miaka hiyo sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na taifa lile, asema BWANA, kwa sababu ya uovu wao, na nchi ya Wakaldayo pia; nami nitaifanya kuwa ukiwa wa milele. Nami nitaleta juu ya nchi ile maneno yangu yote niliyoyanena juu yake, naam, yote yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki, aliyotabiri Yeremia juu ya mataifa haya yote. Kwa maana mataifa mengi na wafalme wakuu watawatumikisha; naam, hao pia; nami nitawalipa kwa kadiri ya matendo yao, na kwa kadiri ya kazi ya mikono yao.
Yeremia 25:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, katika habari za watu wote wa Yuda; katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda mwaka ule ndio mwaka wa kwanza wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli; ambalo Yeremia, nabii, aliwaambia watu wote wa Yuda, na wenyeji wote wa Yerusalemu, kusema, Tangu mwaka wa kumi na tatu wa kutawala kwake Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, hata siku hii ya leo, miaka hii ishirini na mitatu, neno la BWANA limenijia, nami nimesema nanyi, nikiamka mapema na kusema; lakini ninyi hamkusikiliza. Naye BWANA ametuma kwenu watumishi wake wote, hao manabii, akiamka mapema na kuwatuma, lakini ninyi hamkusikiliza, wala hamkutega masikio yenu, msikilize. Akasema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya; uacheni uovu wa matendo yenu, mkae katika nchi ambayo BWANA aliwapa, ninyi na baba zenu, tangu zamani za kale na hata milele; wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia na kuwasujudia, wala msinikasirishe kwa kazi ya mikono yenu; basi, mimi sitawadhuru ninyi kwa dhara lo lote. Lakini ninyi hamkunisikiliza, asema BWANA; ili mnikasirishe kwa kazi ya mikono yenu, na kujidhuru nafsi zenu. Basi BWANA wa majeshi asema hivi, Kwa kuwa hamkuyasikiliza maneno yangu, angalieni, nitapeleka watu na kuzitwaa jamaa zote za upande wa kaskazini, asema BWANA, nami nitatuma ujumbe kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu, nami nitawaleta juu ya nchi hii, na juu yao wakaao ndani yake, na juu ya mataifa haya yote yaliyopo pande zote; nami nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kitu cha kushangaza, na kitu cha kuzomewa, na ukiwa wa daima. Tena, nitawaondolea sauti ya kicheko, na sauti ya furaha, sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na nuru ya mishumaa. Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini. Na itakuwa miaka hiyo sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na taifa lile, asema BWANA, kwa sababu ya uovu wao, nayo nchi ya Wakaldayo pia; nami nitaifanya kuwa ukiwa wa milele. Nami nitaleta juu ya nchi ile maneno yangu yote niliyoyanena juu yake, naam, yote yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki, aliyotabiri Yeremia juu ya mataifa haya yote. Kwa maana mataifa mengi na wafalme wakuu watawatumikisha; naam, hao pia; nami nitawalipa kwa kadiri ya matendo yao, na kwa kadiri ya kazi ya mikono yao.
Yeremia 25:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno likamjia Yeremia kuhusu watu wote wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kwanza wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli. Nabii Yeremia akawaambia watu wote wa Yuda na wote wanaoishi Yerusalemu: Kwa miaka ishirini na tatu, kuanzia mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda, hadi siku hii ya leo, neno la BWANA limekuwa likinijia, nami nimesema nanyi mara kwa mara, lakini hamkusikiliza. Ingawa BWANA aliwatuma kwenu mara kwa mara watumishi na manabii wake wote, ninyi hamkusikiliza wala hamkujali. Walisema, “Geukeni sasa, kila mmoja wenu kutoka njia yake mbaya na matendo yake maovu, ndipo mtaweza kukaa katika nchi ambayo BWANA aliwapa ninyi na baba zenu milele. Msiifuate miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu. Msinikasirishe kwa vitu mlivyovitengeneza kwa mikono yenu.” “Lakini ninyi hamkunisikiliza, tena mkanikasirisha kwa vitu mlivyovitengeneza kwa mikono yenu, nanyi mmejiletea madhara juu yenu wenyewe,” asema BWANA. Kwa hiyo BWANA wa majeshi asema hivi: “Kwa sababu hamkuyasikiliza maneno yangu, nitayaita mataifa yote ya kaskazini na mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli,” asema BWANA. “Nitawaleta waishambulie nchi hii na wakazi wake wote, na dhidi ya mataifa yote yanayowazunguka. Nitawaangamiza kabisa na kuwafanya kitu cha kuchukiwa na kudharauliwa, na kuwa magofu daima. Nitawaondolea sauti ya shangwe na furaha, sauti ya bibi arusi na ya bwana arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na mwanga wa taa. Nchi hii yote itakuwa ukiwa na isiyofaa kitu, nayo mataifa haya yatamtumikia mfalme wa Babeli kwa miaka sabini. “Miaka sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli na taifa lake na nchi ya Wakaldayo kwa ajili ya hatia yao,” asema BWANA. “Nitaifanya kuwa ukiwa milele. Nitaleta juu ya nchi hiyo mambo yote niliyosema dhidi yake, yote yaliyoandikwa katika kitabu hiki, na kutolewa unabii na Yeremia dhidi ya mataifa yote. Wao wenyewe watakuwa watumwa wa mataifa mengi na wafalme wakuu. Nitawalipizia sawasawa na matendo yao na kazi ya mikono yao.”