Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 22:1-30

Yeremia 22:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nenda katika ikulu ya mfalme wa Yuda, uwape watu ujumbe huu: Wewe mfalme wa Yuda unayekikalia kiti cha enzi cha mfalme Daudi, pamoja na watumishi wako na watu wako wanaopita katika malango haya, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tendeni mambo ya haki na uadilifu. Mwokoeni mikononi mwa mdhalimu mtu yeyote aliyenyanganywa mali zake. Msiwatendee vibaya au ukatili wageni, yatima na wajane wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia mahali hapa. Kama mkishika neno hili nililowaambia basi, wafalme wanaokikalia kiti cha enzi cha Daudi wataendelea kuingia kwa kupitia malango ya ikulu hii. Watapita pamoja na watumishi wao na watu wao, wakiwa wamepanda farasi na magari ya farasi. Lakini kama hamtatii maneno haya, mimi Mwenyezi-Mungu naapa kwa nafsi yangu kwamba mahali hapa patakuwa magofu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi kuhusu ikulu ya mfalme wa Yuda: “Ingawa waonekana kuwa mzuri kama nchi ya Gileadi kama kilele cha Lebanoni, Lakini naapa kuwa nitakufanya uwe jangwa, uwe mji usiokaliwa na watu. Nitawatayarisha waangamizi dhidi yako, kila mmoja na silaha yake mkononi. Wataikata mierezi yako mizuri, na kuitumbukiza motoni. “Kisha watu wengi wa mataifa watapita karibu na mji huu, na kila mmoja atamwuliza mwenzake: ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ameutenda hivi mji huu mkubwa?’ Wenzao watawajibu, ‘Ni kwa sababu waliliacha agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakaiabudu miungu mingine na kuitumikia.’” Msimlilie mtu aliyekufa, wala msiombolezee kifo chake. Bali mlilieni kwa uchungu yule aendaye mbali, kwa kuwa hatarudi tena kuiona nchi yake. Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Shalumu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, aliyetawala baada ya Yosia baba yake, na ambaye aliondoka mahali hapa: “Shalumu hatarudi tena mahali hapa, bali atafia hukohuko walikomchukua utumwani. Kamwe hataiona tena nchi hii. “Ole wako Yehoyakimu wewe unayejenga nyumba kwa dhuluma na kuiwekea ghorofa bila kutumia haki. Unawaajiri watu wakutumikie bure wala huwalipi mishahara yao. Wewe wasema: ‘Nitalijenga jumba kubwa, lenye vyumba vikubwa ghorofani.’ Kisha huifanyia madirisha, ukafunika kuta zake kwa mbao za mierezi, na kuipaka rangi nyekundu! Unadhani umekuwa mfalme kwa kushindana kujenga kwa mierezi? Baba yako alikula na kunywa, akatenda mambo ya haki na mema ndipo mambo yake yakamwendea vema. Aliwapatia haki maskini na wahitaji, na mambo yake yakamwendea vema. Hii ndiyo maana ya kunijua mimi Mwenyezi-Mungu. Lakini macho yako wewe na moyo wako, hungangania tu mapato yasiyo halali. Unamwaga damu ya wasio na hatia, na kuwatendea watu dhuluma na ukatili. “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu ya Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda: Wakati atakapokufa, hakuna atakayemwombolezea akisema, ‘Ole, kaka yangu!’ ‘Ole, dada yangu!’ Hakuna atakayemlilia akisema, ‘Maskini, bwana wangu!’ ‘Maskini, mfalme wangu!’ Atazikwa bila heshima kama punda, ataburutwa na kutupiliwa mbali, nje ya malango ya Yerusalemu.” Enyi watu wa Yerusalemu, pandeni Lebanoni mpige kelele, pazeni sauti zenu huko Bashani; lieni kutoka milima ya Abarimu, maana wapenzi wenu wote wameangamizwa. Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi mlipokuwa na fanaka, lakini nyinyi mkasema, “Hatutasikiliza.” Hii ndiyo tabia yenu tangu ujana wenu, hamjapata kuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu. Viongozi wenu watapeperushwa na upepo, wapenzi wenu watachukuliwa uhamishoni. Ndipo mtakapoona haya na kufadhaika, kwa sababu ya uovu wenu wote mliotenda. Enyi wakazi wote wa Lebanoni, nyinyi mkaao salama kati ya mierezi; jinsi gani mtakavyopiga kite uchungu utakapowakumba, uchungu kama wa mama anayejifungua! Na kuhusu Konia mfalme wa Yuda, mwanawe Yehoyakimu, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Naapa kwa nafsi yangu mimi Mwenyezi-Mungu kwamba hata kama wewe Konia mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yangu ya mhuri katika mkono wangu wa kulia, ningekuvulia mbali. Nitakutia mikononi mwa wale wanaotaka kuyamaliza maisha yako; naam, mikononi mwa wale unaowaogopa, mikononi mwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni; naam, mikononi mwa Wakaldayo. Nitakufukuzia mbali katika nchi ya kigeni, wewe pamoja na mama yako mzazi. Mtakuwa watumwa katika nchi hiyo ambamo nyote wawili hamkuzaliwa, nanyi mtafia hukohuko. Mtatamani kwa hamu kubwa kurudi katika nchi hii, lakini hamtarudi kamwe. Je, huyu mtu Konia, amekuwa kama chungu kilichovunjika, ambacho hudharauliwa na kutupwa nje? Kwa nini yeye na watoto wake wametupwa mbali wakatupwa katika nchi wasiyoijua? Ee nchi, ee nchi, ee nchi! Sikia neno la Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu asema hivi: Mwandike mtu huyu kwamba hana watoto, mtu ambaye hatafanikiwa maishani mwake. Maana hakuna hata mmoja wa wazawa wake atakayekikalia kiti cha enzi cha Daudi na kutawala tena katika Yuda.

Shirikisha
Soma Yeremia 22

Yeremia 22:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akasema hivi, Shuka nyumbani kwa mfalme wa Yuda, ukaseme neno hili huko, ya kwamba, Sikia neno la BWANA, Ee mfalme wa Yuda; wewe uketiye katika kiti cha enzi cha Daudi, wewe, na watumishi wako, na watu wako wote waingiao kwa malango haya; BWANA asema hivi, Fanyeni hukumu na haki, mkamtoe yeye aliyetekwa katika mikono ya mdhalimu; wala msiwatende mabaya mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kuwadhulumu, wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia katika mahali hapa. Kwa maana mkifanya haya kweli kweli, ndipo watakapoingia kwa malango ya nyumba hii wafalme wenye kuketi katika kiti cha enzi cha Daudi, wanakwenda kwa magari, na wamepanda farasi, yeye, na watumishi wake, na watu wake. Lakini kama hamtaki kusikia maneno haya, mimi naapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, ya kuwa nyumba hii itakuwa ukiwa. Kwa maana BWANA asema hivi, kuhusu habari za nyumba ya mfalme wa Yuda; Wewe u Gileadi kwangu, na kichwa cha Lebanoni; Ila hakika nitakufanya kuwa jangwa, na miji isiyokaliwa na watu. Nami nitawatayarisha waangamizi juu yako, kila mtu na silaha zake; Nao watakata mierezi yako miteule, na kuitupa motoni. Na mataifa mengi watapita karibu na mji huu, nao watasema kila mtu na jirani yake, Nini maana yake BWANA kuutenda hivi mji huu mkubwa? Ndipo watakapojibu, Ni kwa sababu waliliacha agano la BWANA, Mungu wao, wakaabudu miungu mingine, na kuitumikia. Msimlilie aliyekufa, wala msimwombolezee, Bali mlilieni huyo aendaye zake mbali; Kwa maana yeye hatarudi tena, Wala hataiona nchi aliyozaliwa. Maana BWANA asema hivi, kuhusu habari za Shalumu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; aliyemiliki badala ya Yosia, baba yake, yeye aliyetoka mahali hapa; Hatarudi huku tena; bali katika mahali pale walipomchukua mateka ndipo atakapokufa, wala hataiona nchi hii tena kamwe. Ole wake aijengaye nyumba yake kwa uovu! Na vyumba vyake kwa udhalimu! Atumiaye utumishi wa mwenzake bila ujira, Wala hampi mshahara wake; Asemaye, Nitajijengea nyumba kubwa yenye vyumba vipana; Naye hujikatia madirisha; Na kuta zake zimefunikwa kwa mierezi, Na kupakwa rangi nyekundu. Je! Utatawala kwa sababu unashindana na watu kwa mierezi? Baba yako, je! Hakula na kunywa, na kufanya hukumu na haki? Hapo ndipo alipofanikiwa. Alihukumu maneno ya maskini na mhitaji; hapo ndipo alipofanikiwa. Je! Huku siko kunijua, asema BWANA? Bali macho yako na moyo wako hauna utakalo ila kutamani, na kumwaga damu isiyo na hatia, na kudhulumu, na kutenda jeuri. Basi, BWANA asema hivi, kuhusu habari za Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; Hawatamwombolezea, wakisema, Aa! Ndugu yangu; au, Aa! Dada yangu; wala hawatamlilia, wakisema, Aa! Bwana wangu; au, Aa! Utukufu wake. Atazikwa maziko ya punda, akibururwa, na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu. Haya panda Lebanoni, ukalie Upalize sauti yako katika Bashani; Ukalie kutoka Abarimu; Maana wapenzi wako wote wameangamia. Mimi nilisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako; lakini ulisema, Sitaki kusikia. Hii ndiyo iliyokuwa desturi yako tangu ujana wako, kutoitii sauti yangu. Upepo utawalisha wachungaji wako wote, na wapenzi wako watakwenda kufungwa; hakika wakati huo utatahayarika, na kufadhaika kwa sababu ya uovu wako wote. Wewe ukaaye Lebanoni, Ujengaye kiota chako katika mierezi, Utakuwa na hali ya kuhurumiwa sana, Upatapo uchungu kama wa mwanamke azaaye. Kama niishivyo mimi, asema BWANA, hata Konia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, angekuwa pete yenye mhuri katika mkono wangu wa kulia, ningekung'oa wewe hapo; nami nitakutia katika mikono ya watu wale wakutafutao roho yako, na katika mikono yao unaowaogopa, naam, katika mikono ya Nebukadneza, mfalme wa Babeli, na katika mikono ya Wakaldayo. Nami nitakutupa nje, wewe na mama yako aliyekuzaa, mwende katika nchi nyingine ambayo hamkuzaliwa huko, nanyi mtakufa huko. Lakini nchi ile ambayo wanatamani kuirudia, hawatairudia kamwe. Je! Mtu huyu, Konia, ni chombo kilichodharauliwa, na kuvunjika? Ni chombo kisichopendeza? Mbona wametupwa, yeye na wazao wake, na kutupwa katika nchi wasiyoijua? Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la BWANA. BWANA asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda.

Shirikisha
Soma Yeremia 22

Yeremia 22:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akasema hivi, Shuka nyumbani kwa mfalme wa Yuda, ukaseme neno hili huko, ya kwamba, Sikia neno la BWANA, Ee mfalme wa Yuda; wewe uketiye katika kiti cha enzi cha Daudi, wewe, na watumishi wako, na watu wako wote waingiao kwa malango haya; BWANA asema hivi, Fanyeni hukumu na haki, mkamtoe yeye aliyetekwa katika mikono ya mdhalimu; wala msiwatende mabaya mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kuwadhulumu, wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia katika mahali hapa. Kwa maana mkifanya haya kweli kweli, ndipo watakapoingia kwa malango ya nyumba hii wafalme wenye kuketi katika kiti cha enzi cha Daudi, wanakwenda kwa magari, na wamepanda farasi yeye, na watumishi wake, na watu wake. Lakini kama hamtaki kusikia maneno haya, mimi naapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, ya kuwa nyumba hii itakuwa ukiwa. Kwa maana BWANA asema hivi, katika habari ya nyumba ya mfalme wa Yuda; Wewe u Gileadi kwangu, na kichwa cha Lebanoni; Ila hakika nitakufanya kuwa jangwa, na miji isiyokaliwa na watu. Nami nitakufanyia tayari watu wenye kuharibu, kila mtu na silaha zake; Nao watakata mierezi miteule yako, na kuitupa motoni. Na mataifa mengi watapita karibu na mji huu, nao watasema kila mtu na jirani yake, Nini maana yake BWANA kuutenda hivi mji huu mkubwa? Ndipo watakapojibu, Ni kwa sababu waliliacha agano la BWANA, Mungu wao, wakaabudu miungu mingine, na kuitumikia. Msimlilie aliyekufa, wala msimwombolezee, Bali mlilieni huyo aendaye zake mbali; Kwa maana yeye hatarudi tena, Wala hataiona nchi aliyozaliwa. Maana BWANA asema hivi, katika habari za Shalumu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; aliyemiliki badala ya Yosia, baba yake, yeye aliyetoka mahali hapa; Hatarudi huku tena; bali katika mahali pale walipomchukua mateka ndipo atakapokufa, wala hataiona nchi hii tena kamwe. Ole wake aijengaye nyumba yake kwa uovu! Na vyumba vyake kwa udhalimu! Atumiaye utumishi wa mwenzake bila ujira, Wala hampi mshahara wake; Asemaye, Nitajijengea nyumba pana na vyumba vipana; Naye hujikatia madirisha; Na kuta zake zimefunikwa kwa mierezi, Na kupakwa rangi nyekundu. Je! Utatawala kwa sababu unashindana na watu kwa mierezi? Baba yako, je! Hakula na kunywa, na kufanya hukumu na haki? Hapo ndipo alipofanikiwa. Alihukumu maneno ya maskini na mhitaji; hapo ndipo alipofanikiwa. Je! Huku siko kunijua, asema BWANA? Bali macho yako na moyo wako hauna utakalo ila kutamani, na kumwaga damu isiyo na hatia, na kudhulumu, na kutenda jeuri. Basi, BWANA asema hivi, katika habari ya Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; Hawatamwombolezea, wakisema, Aa! Ndugu yangu; au, Aa! Dada yangu; wala hawatamlilia, wakisema, Aa! Bwana wangu; au, Aa! Utukufu wake. Atazikwa maziko ya punda, akibururwa, na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu. Haya panda Lebanoni, ukalie Upalize sauti yako katika Bashani; Ukalie kutoka Abarimu; Maana wapenzi wako wote wameangamia. Mimi nalisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako; lakini ulisema, Sitaki kusikia. Hii ndiyo iliyokuwa desturi yako tangu ujana wako, kutokuitii sauti yangu. Upepo utawalisha wachungaji wako wote, na wapenzi wako watakwenda kufungwa; hakika wakati huo utatahayarika, na kufadhaika kwa sababu ya uovu wako wote. Wewe ukaaye Lebanoni, Ufanyaye kioto chako katika mierezi, Utakuwa na hali ya kuhurumiwa sana, Upatapo utungu kama wa mwanamke azaaye. Kama niishivyo mimi, asema BWANA, hata Konia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, angekuwa pete yenye muhuri katika mkono wangu wa kuume, ningekung’oa wewe hapo; nami nitakutia katika mikono ya watu wale wakutafutao roho yako, na katika mikono yao unaowaogopa, naam, katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na katika mikono ya Wakaldayo. Nami nitakutupa nje, wewe na mama yako aliyekuzaa, mwende nchi nyingine ambayo hamkuzaliwa huko, nanyi mtakufa huko. Lakini nchi ile ambayo wanatamani kuirudia, hawatairudia kamwe. Je! Mtu huyu, Konia, ni chombo kilichodharauliwa, na kuvunjika? Ni chombo kisichopendeza? Mbona wametupwa, yeye na wazao wake, na kutupwa katika nchi wasiyoijua? Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la BWANA. BWANA asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda.

Shirikisha
Soma Yeremia 22

Yeremia 22:1-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hili ndilo asemalo BWANA: “Shuka kwenye jumba la kifalme la mfalme wa Yuda, utangaze ujumbe huu huko: ‘Sikia neno la BWANA, ee mfalme wa Yuda, wewe uketiye kwenye kiti cha utawala cha Daudi: wewe, wakuu wako na watu wako mnaopitia malango haya. Hili ndilo asemalo BWANA: Tenda haki na adili. Mwokoe mkononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara. Usimtendee mabaya wala ukatili mgeni, yatima au mjane, wala usimwage damu isiyo na hatia mahali hapa. Ukiwa mwangalifu kushika maagizo haya, wafalme watakaokalia kiti cha utawala cha Daudi wataingia kupitia malango ya jumba la kifalme wakiwa wamepanda magari na farasi huku wakifuatana na watumishi wao na watu wao. Lakini kama hutayatii maagizo haya, asema BWANA, ninaapa kwa nafsi yangu kwamba jumba hili litakuwa gofu.’ ” Hili ndilo asemalo BWANA kuhusu jumba la kifalme la mfalme wa Yuda: “Ingawa uko kama Gileadi kwangu, kama kilele cha Lebanoni, hakika nitakufanya uwe kama jangwa, kama miji ambayo haijakaliwa na watu. Nitawatuma waharibifu dhidi yako, kila mtu akiwa na silaha zake, nao watazikata boriti zako bora za mwerezi na kuzitupa motoni. “Watu kutoka mataifa mengi watapita karibu na mji huu na kuulizana, ‘Kwa nini BWANA amefanya jambo la namna hii kwa mji huu mkubwa?’ Nalo jibu litakuwa: ‘Kwa sababu wameliacha agano la BWANA, Mungu wao, na wameabudu na kuitumikia miungu mingine.’ ” Usimlilie yeye aliyekufa, wala usimwombolezee; badala yake, afadhali umlilie kwa uchungu yule aliyepelekwa uhamishoni, kwa sababu kamwe hatairudia wala kuiona tena nchi yake aliyozaliwa. Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA kuhusu Shalumu mwana wa Yosia, aliyeingia mahali pa baba yake kuwa mfalme wa Yuda, lakini ameondoka mahali hapa: “Yeye kamwe hatarudi tena. Atafia huko mahali walipompeleka kuwa mateka; hataiona tena nchi hii.” “Ole wake yeye ajengaye jumba lake la kifalme kwa dhuluma, vyumba vyake vya juu kwa udhalimu, akiwatumikisha watu wa nchi yake pasipo malipo, bila kuwalipa kwa utumishi wao. Anasema, ‘Nitajijengea jumba kuu la kifalme, na vyumba vya juu vyenye nafasi kubwa.’ Hivyo anaweka ndani yake madirisha makubwa, huweka kuta za mbao za mwerezi, na kuzipaka kwa rangi nyekundu. “Je, huko kuongeza idadi ya mierezi kutakufanya uwe mfalme? Je, baba yako hakula na kunywa? Alifanya yaliyo sawa na haki, naye akafanikiwa kwa yote. Aliwatetea maskini na wahitaji, hivyo yeye akafanikiwa katika yote. Je, hiyo si ndiyo maana ya kunijua mimi?” asema BWANA. “Lakini macho yako na moyo wako vimeelekezwa tu katika mapato ya udhalimu, kumwaga damu isiyo na hatia, na katika uonevu na ukatili.” Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA kuhusu Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda: “Hawatamwombolezea wakisema: ‘Ole, ndugu yangu! Ole, dada yangu!’ Hawatamwombolezea wakisema: ‘Ole, bwana wangu! Ole, fahari yake!’ Atazikwa maziko ya punda: ataburutwa na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu.” “Panda Lebanoni ukapige kelele, sauti yako na isikike huko Bashani, piga kelele toka Abarimu, kwa kuwa wote waliojiunga nawe wameangamizwa. Nilikuonya wakati ulipojisikia kwamba uko salama, lakini ulisema, ‘Mimi sitasikiliza!’ Hii imekuwa kawaida yako tangu ujana wako; hujanitii mimi. Upepo utawaondoa wachungaji wako wote, na wandani wako wataenda uhamishoni. Kisha utaaibika na kufedheheka kwa sababu ya uovu wako wote. Wewe uishiye Lebanoni, wewe uliyetulia kwenye majengo ya mwerezi, tazama jinsi utakavyoomboleza maumivu makali yatakapokupata, maumivu kama ya mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa! “Hakika kama niishivyo,” asema BWANA, “hata kama wewe, Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yangu ya muhuri katika mkono wangu wa kuume, bado ningekungʼoa hapo. Nitakutia mikononi mwa wanaoutafuta uhai wako, wale unaowaogopa, yaani Nebukadneza mfalme wa Babeli na kwa Wakaldayo. Nitakutupa mbali wewe na mama aliyekuzaa mwende katika nchi nyingine, ambayo hakuna hata mmoja wenu aliyezaliwa huko, nanyi mtafia huko. Kamwe hamtarudi katika nchi mliyotamani kuirudia.” Je, huyu mtu Yekonia ni chungu kilichodharauliwa, chungu kilichovunjika, chombo kisichotakiwa na mtu yeyote? Kwa nini yeye na watoto wake watupwe nje kwa nguvu, na kutupwa kwenye nchi wasioijua? Ee nchi, nchi, nchi, sikia neno la BWANA! Hili ndilo asemalo BWANA: “Mwandike huyu mtu kama asiye na mtoto, mtu ambaye hatafanikiwa maisha yake yote, kwa maana hakuna mzao wake atakayefanikiwa, wala kukaa kwenye kiti cha utawala cha Daudi wala kuendelea kutawala katika Yuda.”

Shirikisha
Soma Yeremia 22