Yeremia 16:1-9
Yeremia 16:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia na kusema: “Wewe hutaoa wala hutapata watoto mahali hapa. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu ya watoto wa kiume na wa kike watakaozaliwa mahali hapa, na juu ya wazazi wao: Hao watakufa kwa maradhi mabaya, na hakuna atakayewaombolezea wala kuwazika. Maiti zao zitazagaa kama mavi juu ya ardhi. Wataangamia kwa upanga na kwa njaa; na maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wakali wa nchi. “Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Usiingie kabisa katika nyumba ya matanga wala usiende kuomboleza wala kuwalilia. Kwa maana nimeondoa amani yangu, fadhili zangu na huruma yangu kutoka kwa watu hawa. Wote, wakubwa kwa wadogo, watakufa katika nchi hii; nao hawatazikwa, wala hakuna atakayewaombolezea. Hakuna atakayejikatakata au kunyoa upara wa matanga. Hakuna atakayemshirikisha aliyefiwa chakula cha kumfariji, wala kumpatia kinywaji cha kumfariji anywe kwa ajili ya kufiwa na mama au baba yake. “Usiingie katika nyumba wanamofanya karamu. Usiketi kula na kunywa pamoja nao. Maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nitazikomesha kabisa kutoka mahali hapa sauti za furaha na za shangwe, pamoja na sauti za bwana arusi na bibi arusi. Yote haya nitayafanya wakati wa uhai wenu mkiwa mnaona waziwazi.
Yeremia 16:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe hutaoa mke, wala hutakuwa na wana wala binti mahali hapa. Maana BWANA asema hivi, kuhusu habari za wana, na kuhusu habari za binti, wazaliwao mahali hapa, na kuhusu habari za mama zao waliowazaa, na kuhusu habari za baba zao waliowazaa, katika nchi hii; watakufa kwa maradhi mabaya; hawataliliwa, wala hawatazikwa; watakuwa kama samadi juu ya uso wa nchi; nao wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa; na mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi. Maana BWANA asema hivi, Usiingie ndani ya nyumba yenye matanga, wala usiende kuwaombolezea, wala kuwalilia; maana nimewaondolea watu hawa amani yangu, asema BWANA, hata fadhili zangu na rehema zangu. Wakubwa kwa wadogo wote pia watakufa katika nchi hii; hawatazikwa, wala watu hawatawalilia, wala kujikatakata kwa ajili yao, wala kujinyoa kwa ajili yao; wala watu hawatamega mkate kwa ajili yao, wakati wa kuomboleza, ili kuwafariji kwa ajili yao waliokufa; wala watu hawatawapa kikombe cha faraja, wanywe kwa ajili ya baba yao au mama yao. Wala usiingie ndani katika nyumba yenye karamu, kuketi pamoja nao, na kula na kunywa. Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi, mbele ya macho yenu, na katika siku zenu, nitaikomesha sauti ya furaha, na sauti ya kicheko, mahali hapa; sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi.
Yeremia 16:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe hutaoa mke, wala hutakuwa na wana wala binti mahali hapa. Maana BWANA asema hivi, katika habari za wana, na katika habari za binti, wazaliwao mahali hapa, na katika habari za mama zao waliowazaa, na katika habari za baba zao waliowazaa, katika nchi hii; watakufa kwa maradhi mabaya; hawataliliwa, wala hawatazikwa; watakuwa kama samadi juu ya uso wa nchi; nao wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa; na mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi. Maana BWANA asema hivi, Usiingie ndani ya nyumba yenye matanga, wala usiende kuwaombolezea, wala kuwalilia; maana nimewaondolea watu hawa amani yangu, asema BWANA, hata fadhili zangu na rehema zangu. Wakubwa kwa wadogo wote pia watakufa katika nchi hii; hawatazikwa, wala watu hawatawalilia, wala kujikata-kata kwa ajili yao, wala kujinyoa kwa ajili yao; wala watu hawatamega mkate kwa ajili yao, wakati wa kuomboleza, ili kuwafariji kwa ajili yao waliokufa; wala watu hawatawapa kikombe cha faraja, wanywe kwa ajili ya baba yao au mama yao. Wala usiingie ndani katika nyumba yenye karamu, kuketi pamoja nao, na kula na kunywa. Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi, mbele ya macho yenu, na katika siku zenu, nitaikomesha sauti ya furaha, na sauti ya kicheko, mahali hapa; sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi.
Yeremia 16:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha neno la BWANA likanijia: “Kamwe usioe na kuwa na wana wala binti mahali hapa.” Kwa maana hili ndilo asemalo BWANA kuhusu wana wa kiume na wa kike wanaozaliwa katika nchi hii, na kuhusu wale wanawake ambao ni mama zao, na wale wanaume ambao ni baba zao: “Watakufa kwa magonjwa ya kufisha. Hawataombolezewa wala kuzikwa, lakini watakuwa kama kinyesi juu ya ardhi. Watakufa kwa upanga na kwa njaa. Mizoga yao itakuwa chakula cha ndege na wanyama wa porini.” Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA: “Usiingie katika nyumba ambayo kuna chakula cha matanga; usiende kuwaombolezea wala kuwahurumia, kwa sababu nimeondoa amani yangu, upendo wangu na huruma zangu kutoka kwa watu hawa,” asema BWANA. “Wakubwa na wadogo watakufa katika nchi hii. Hawatazikwa wala kuombolezewa, na hakuna atakayejikatakata au kunyoa nywele za kichwa chake kwa ajili yao. Hakuna yeyote atakayewapa chakula ili kuwafariji wanaoomboleza kwa ajili ya waliokufa, hata akiwa amefiwa na baba au mama, wala hakuna yeyote atakayewapa kinywaji ili kuwafariji. “Usiingie katika nyumba ambayo kuna karamu, na kuketi humo ili kula na kunywa. Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi, aliye Mungu wa Israeli: ‘Mbele ya macho yako na katika siku zako, nitakomesha sauti zote za shangwe na za furaha, na pia sauti za bibi arusi na bwana arusi mahali hapa.’