Yeremia 13:1-27
Yeremia 13:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Nenda ukajinunulie kikoi cha kitani, ukajifunge kiunoni; lakini usikitie majini.” Basi, nikaenda, nikanunua kikoi kama alivyoniagiza Mwenyezi-Mungu, nikajifunga kiunoni. Kisha, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili: “Kichukue kikoi ulichonunua na ambacho umejifunga kiunoni, uende kwenye mto Eufrate na kukificha katika pango mwambani.” Basi, nikaenda na kukificha kikoi hicho karibu na mto Eufrate, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniamuru. Ikawa, baada ya siku nyingi, Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Nenda kwenye mto Eufrate, ukakichukue kile kikoi nilichokuamuru ukifiche huko.” Basi, nikaenda kwenye mto Eufrate, nikachimbua na kukitoa kile kikoi mahali nilipokuwa nimekificha. Nilipokitoa, nilishangaa kukiona kuwa kilikuwa kimeharibika kabisa; kilikuwa hakifai tena. Ndipo neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hivi ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikubwa cha Yerusalemu. Watu hawa waovu wanakataa kusikia maneno yangu, na badala yake wanakuwa wakaidi na kufuata mawazo yao wenyewe. Wanaifuata miungu mingine, wanaitumikia na kuiabudu. Hao watakuwa kama kikoi hiki ambacho hakifai kitu. Kama vile kikoi kinavyoshikamana na kiuno cha mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami watu wa Israeli na watu wa Yuda, ili wajulikane kwa jina langu, wanisifu na kunitukuza. Lakini wao hawakunisikiliza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliniambia hivi: “Waambie watu wa Israeli kwamba kila mtungi utajazwa divai. Lakini utakapowaambia hivyo, wao watakujibu hivi: ‘Kwani unadhani sisi hatujui kwamba kila mtungi utajazwa divai?’ Nawe utawaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawalewesha wenyeji wote wa nchi hii; wafalme wanaotawala mahali pa Daudi, makuhani, manabii na wakazi wote wa Yerusalemu. Nitawagonganisha wao kwa wao kina baba na watoto. Sitawahurumia, sitawaachia wala sitawarehemu, bali nitawaangamiza.” Enyi Waisraeli, sikilizeni kwa makini, msiwe na majivuno maana Mwenyezi-Mungu anasema nanyi. Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kabla hajawaletea giza, nanyi mkajikwaa miguu kwenye milima ya giza. Nyinyi mnatazamia mwanga, lakini anaugeuza kuwa utusitusi na kuufanya kuwa giza nene. Lakini kama msiponisikiliza, moyo wangu utalia machozi faraghani, kwa sababu ya kiburi chenu. Nitalia kwa uchungu na kububujika machozi, kwa kuwa watu wa Mwenyezi-Mungu wametekwa. Mwambie mfalme na mama yake hivi: “Shukeni kwenye viti vyenu vya enzi, maana taji zenu nzuri zimeanguka vichwani mwenu. Miji ya Negebu imezingirwa; hakuna awezaye kufungua malango yake. Watu wa Yuda wamechukuliwa mateka, wote kabisa wamepelekwa utumwani.” Inua macho yako, ee Yerusalemu! Tazama! Madui zako waja kutoka kaskazini. Kundi ulilokabidhiwa liko wapi? Kundi lako zuri li wapi? Utasemaje juu ya wale uliodhani ni rafiki, wale ambao wewe mwenyewe uliwafundisha, watakapokushinda na kukutawala? Je, si utakumbwa na uchungu kama wa mama anayejifungua? Nawe utajiuliza moyoni mwako, “Kwa nini mambo haya yamenipata?” Sawa! Kama vazi lako limepandishwa juu, nawe ukatendewa kwa ukatili mno, hayo ni matokeo ya makosa yako mengi mno. Je, Mwethiopia aweza kubadili rangi yake, au chui madoadoa yake? Ikiwezekana, nanyi pia mnaweza kutenda mema, nyinyi mliozoea kutenda maovu! Mwenyezi-Mungu atawatawanya kama makapi yanayopeperushwa na upepo kutoka jangwani. Mwenyezi-Mungu asema: “Hayo ndiyo yatakayokupata, ndivyo nilivyoamua kukutenda mimi Mwenyezi-Mungu, kwa sababu umenisahau mimi, ukaamini miungu ya uongo. Nitalipandisha vazi lako hadi kichwani na aibu yako yote itaonekana wazi. Nimeyaona machukizo yako: Naam, uzinifu wako na uzembe wako, na uasherati wako wa kupindukia, juu ya milima na mashambani. Ole wako ee Yerusalemu! Mpaka lini utakaa bila kutakaswa?”
Yeremia 13:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akaniambia hivi, Nenda ukajinunulie kitambaa cha kitani, ukajifunge kiunoni, wala usikitie majini. Basi nikanunua kitambaa cha kitani sawasawa na neno la BWANA, nikajivika viunoni. Nalo neno la BWANA likanijia mara ya pili, kusema, Twaa kitambaa kile ulichonunua, kilicho viunoni mwako, kisha ondoka, nenda mpaka mto Frati, ukaufiche huko katika pango la jabali. Basi nikaenda, nikakificha karibu na mto Frati, kama BWANA alivyoniamuru. Hata ikawa, baada ya siku nyingi, BWANA akaniambia, Ondoka, nenda mpaka mto Frati, ukakitwae kile kitambaa, nilichokuamuru kukificha huko. Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikakitwaa kile kitambaa katika mahali pale nilipokificha; na tazama, kitambaa kilikuwa kimeharibika, hakikufaa tena kwa lolote. Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema, BWANA asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu. Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na kitambaa hiki kisichofaa kwa lolote. Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na kiuno cha mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli; na nyumba yote ya Yuda, asema BWANA; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia. Basi utawaambia neno hili, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila chupa itajazwa divai; nao watakuambia, Je, sisi hatujui ya kuwa kila chupa itajazwa divai? Ndipo utakapowaambia, BWANA asema hivi, Tazama, nitawajaza ulevi wenyeji wote wa nchi hii, hata wafalme wanaoketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na makuhani, na manabii, na wenyeji wote wa Yerusalemu. Nitawagonganisha, mtu na mwenzake, naam, baba za watu na watoto wao pamoja, asema BWANA; sitahurumia, wala sitaachilia, wala sitarehemu, hata nisiwaangamize. Sikilizeni ninyi, kategeni masikio yenu; msifanye kiburi; maana BWANA amenena. Mtukuzeni BWANA, Mungu wenu, kabla hajaleta giza, na kabla miguu yenu haijakwaa juu ya milima yenye giza; na wakati mnapoitazamia nuru, kabla hajaigeuza kuwa kivuli cha mauti, na giza nene. Bali kama hamtaki kusikia, roho yangu italia kwa siri, kwa sababu ya kiburi chenu; na jicho langu litalia sana na kutoka machozi mengi, kwa kuwa kundi la BWANA limechukuliwa mateka. Mwambie mfalme, na mama ya mfalme, Nyenyekeeni na kuketi chini; Kwa maana vilemba vyenu vimeshuka, naam, taji la utukufu wenu. Miji ya Negebu imefungwa malango yake, wala hapana mtu wa kuyafungua; Yuda amechukuliwa mateka; amechukuliwa kabisa mateka. Inua macho yako, Ee Yerusalemu, ukawatazame hawa wanaokuja kutoka kaskazini; liko wapi kundi lako ulilopewa, kundi lile zuri? Utasema nini wewe, atakapowaweka rafiki zako kuwa kichwa juu yako, ikiwa wewe mwenyewe umewafundisha kuwa juu yako? Je! Huzuni haitakushika, kama uchungu wa mwanamke aliye katika kuzaa? Nawe ukisema moyoni mwako, Mbona mambo haya yamenipata mimi? Ni kwa sababu ya wingi wa uovu wako, marinda yako yamefunuliwa, na visigino vya miguu yako vimeumia. Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoadoa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya. Kwa sababu hiyo nitawatawanya, kama makapi yapitayo, kwa upepo wa jangwani. Hiyo ndiyo kura yako, fungu lako ulilopimiwa na mimi, asema BWANA; kwa kuwa umenisahau, na kuutumainia uongo. Kwa ajili ya hayo, mimi nami nitayafunua marinda yako mbele ya uso wako, na aibu yako itaonekana. Nimeona machukizo yako, naam, uzinifu wako, na ubembe wako, na uasherati wa ukahaba wako, juu ya milima katika mashamba. Ole wako, Ee Yerusalemu! Hutaki kutakaswa; mambo hayo yataendelea hata lini?
Yeremia 13:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akaniambia hivi, Enenda, ukajinunulie mshipi wa kitani, ukajivike viuno, wala usiutie majini. Basi nikanunua mshipi sawasawa na neno la BWANA, nikajivika viunoni. Nalo neno la BWANA likanijia mara ya pili, kusema, Twaa mshipi ule ulioununua, ulio viunoni mwako, kisha ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukaufiche huko katika pango la jabali. Basi nikaenda, nikauficha karibu na mto Frati, kama BWANA alivyoniamuru. Hata ikawa, baada ya siku nyingi, BWANA akaniambia, Ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukautwae ule mshipi, niliokuamuru kuuficha huko. Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikautwaa ule mshipi katika mahali pale nilipouficha; na tazama, mshipi ulikuwa umeharibika, haukufaa tena kwa lo lote. Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema, BWANA asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu. Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na mshipi huu, usiofaa kwa lo lote. Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na viuno vya mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli; na nyumba yote ya Yuda, asema BWANA; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia. Basi utawaambia neno hili, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila chupa itajazwa divai; nao watakuambia, Je, sisi hatujui ya kuwa kila chupa itajazwa divai? Ndipo utakapowaambia, BWANA asema hivi, Tazama, nitawajaza ulevi wenyeji wote wa nchi hii, hata wafalme wanaoketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na makuhani, na manabii, na wenyeji wote wa Yerusalemu. Nitawagonganisha, mtu na mwenzake, naam, baba za watu na watoto wao pamoja, asema BWANA; sitahurumia, wala sitaachilia, wala sitarehemu, hata nisiwaangamize. Sikilizeni ninyi, kategeni masikio yenu; msifanye kiburi; maana BWANA amenena. Mtukuzeni BWANA, Mungu wenu, kabla hajaleta giza, na kabla miguu yenu haijakwaa juu ya milima yenye giza; na wakati mnapoitazamia nuru, kabla hajaigeuza kuwa kivuli cha mauti, na giza nene. Bali kama hamtaki kusikia, roho yangu italia kwa siri, kwa sababu ya kiburi chenu; na jicho langu litalia sana na kutoka machozi mengi, kwa kuwa kundi la BWANA limechukuliwa hali ya kufungwa. Mwambie mfalme, na mama ya mfalme, Nyenyekeeni na kuketi chini; Kwa maana vilemba vyenu vimeshuka, naam, taji ya utukufu wenu. Miji ya Negebu imefungwa malango yake, wala hapana mtu wa kuyafungua; Yuda amechukuliwa hali ya kufungwa; amechukuliwa kabisa hali ya kufungwa. Inua macho yako, Ee Yerusalemu, ukawatazame hawa wanaokuja kutoka kaskazini; liko wapi kundi lako ulilopewa, kundi lile zuri? Utasema nini wewe, atakapowaweka rafiki zako kuwa kichwa juu yako, ikiwa wewe mwenyewe umewafundisha kuwa juu yako? Je! Huzuni haitakushika, kama utungu wa mwanamke aliye katika kuzaa? Nawe ukisema moyoni mwako, Mbona mambo haya yamenipata mimi? Ni kwa sababu ya wingi wa uovu wako, marinda yako yamefunuliwa, na visigino vya miguu yako vimeumia. Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya. Kwa sababu hiyo nitawatawanya, kama makapi yapitayo, kwa upepo wa jangwani. Hiyo ndiyo kura yako, fungu lako ulilopimiwa na mimi, asema BWANA; kwa kuwa umenisahau, na kuutumainia uongo. Kwa ajili ya hayo, mimi nami nitayafunua marinda yako mbele ya uso wako, na aibu yako itaonekana. Nimeona machukizo yako, naam, uzinifu wako, na ubembe wako, na uasherati wa ukahaba wako, juu ya milima katika mashamba. Ole wako, Ee Yerusalemu! Hutaki kutakaswa; mambo hayo yataendelea hata lini?
Yeremia 13:1-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hili ndilo BWANA aliloniambia: “Nenda ununue mkanda wa kitani, ujivike kiunoni mwako, lakini usiuache uguse maji.” Kwa hiyo nikanunua mkanda, kama BWANA alivyoniagiza, nikajivika kiunoni. Ndipo neno la BWANA likanijia kwa mara ya pili: “Chukua mkanda ulionunua ambao umeuvaa kiunoni mwako, uende sasa Frati uufiche ndani ya ufa mdogo kwenye mwamba.” Ndipo nikaenda na kuuficha ule mkanda huko Frati, kama BWANA alivyoniamuru. Baada ya siku nyingi BWANA akaniambia, “Nenda sasa Frati ukauchukue ule mkanda niliokuambia uufiche huko.” Hivyo nikaenda Frati na kuuchimbua ule mkanda kutoka pale nilipokuwa nimeuficha, lakini sasa ulikuwa umeharibika na haufai tena kabisa. Ndipo neno la BWANA likanijia: “Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Vivyo hivyo ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikuu cha Yerusalemu. Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wafuatao ukaidi wa mioyo yao na kufuata miungu mingine wakiitumikia na kuiabudu, watakuwa kama mshipi huu ambao haufai kabisa! Kwa maana kama vile mshipi ufungwavyo kiunoni mwa mtu, ndivyo nilivyoifunga nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda,’ asema BWANA, ‘ili wawe watu wangu kwa ajili ya utukufu wangu, sifa na heshima yangu. Lakini hawajasikiliza.’ “Waambie: ‘Hili ndilo BWANA, Mungu wa Israeli, asemalo: kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo.’ Wakikuambia, ‘Kwani hatujui kwamba kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo?’ Uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: nitawajaza ulevi wote wanaoishi katika nchi hii, pamoja na wafalme wanaoketi kwenye kiti cha ufalme cha Daudi, makuhani, manabii na wakaaji wote wa Yerusalemu. Nitawagombanisha kila mmoja na mwenzake, baba na wana wao, asema BWANA. Sitawarehemu wala kuwahurumia ili niache kuwaangamiza.’ ” Sikieni na mzingatie, msiwe na kiburi, kwa kuwa BWANA amenena. Mpeni utukufu BWANA Mungu wenu, kabla hajaleta giza, kabla miguu yenu haijajikwaa juu ya vilima vitakavyotiwa giza. Mlitarajia nuru, lakini ataifanya kuwa giza nene na kuibadili kuwa huzuni kubwa. Lakini kama hamtasikiliza, nitalia sirini kwa ajili ya kiburi chenu; macho yangu yatalia kwa uchungu, yakitiririka machozi, kwa sababu kundi la kondoo la BWANA litachukuliwa mateka. Mwambie mfalme na mama malkia, “Shukeni kutoka viti vyenu vya utawala, kwa kuwa taji zenu za utukufu zitaanguka kutoka vichwani mwenu.” Miji ya Negebu itafungwa, wala hapatakuwa na mtu wa kuifungua. Watu wa Yuda wote watapelekwa uhamishoni, wakichukuliwa kabisa waende mbali. Inua macho yako uone wale wanaokuja kutoka kaskazini. Liko wapi lile kundi ulilokabidhiwa, wale kondoo uliojivunia? Utasema nini BWANA atakapowaweka juu yako wale ulioungana nao kama rafiki zako maalum? Je, hutapatwa na uchungu kama mwanamke aliye katika uchungu wa kuzaa? Nawe ukijiuliza, “Kwa nini haya yamenitokea?” Ni kwa sababu ya dhambi zako nyingi marinda yako yameraruliwa na mwili wako umetendewa vibaya. Je, Mkushi aweza kubadili ngozi yake au chui kubadili madoadoa yake? Vivyo hivyo, wewe uliyezoea kutenda mabaya huwezi kufanya mema. “Nitawatawanya kama makapi yapeperushwayo na upepo wa jangwani. Hii ndiyo kura yako, fungu nililokuamulia,” asema BWANA, “kwa sababu umenisahau mimi na kuamini miungu ya uongo. Nitayafunua marinda yako juu ya uso wako ili aibu yako ionekane, yaani uzinzi wako na kulia kwako kulikojaa tamaa kama farasi, na ukahaba wako usio na aibu! Nimeyaona matendo yako ya machukizo juu ya vilima na mashambani. Ole wako, ee Yerusalemu! Utaendelea kuwa najisi hadi lini?”