Yeremia 13:1-11
Yeremia 13:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Nenda ukajinunulie kikoi cha kitani, ukajifunge kiunoni; lakini usikitie majini.” Basi, nikaenda, nikanunua kikoi kama alivyoniagiza Mwenyezi-Mungu, nikajifunga kiunoni. Kisha, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili: “Kichukue kikoi ulichonunua na ambacho umejifunga kiunoni, uende kwenye mto Eufrate na kukificha katika pango mwambani.” Basi, nikaenda na kukificha kikoi hicho karibu na mto Eufrate, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniamuru. Ikawa, baada ya siku nyingi, Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Nenda kwenye mto Eufrate, ukakichukue kile kikoi nilichokuamuru ukifiche huko.” Basi, nikaenda kwenye mto Eufrate, nikachimbua na kukitoa kile kikoi mahali nilipokuwa nimekificha. Nilipokitoa, nilishangaa kukiona kuwa kilikuwa kimeharibika kabisa; kilikuwa hakifai tena. Ndipo neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hivi ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikubwa cha Yerusalemu. Watu hawa waovu wanakataa kusikia maneno yangu, na badala yake wanakuwa wakaidi na kufuata mawazo yao wenyewe. Wanaifuata miungu mingine, wanaitumikia na kuiabudu. Hao watakuwa kama kikoi hiki ambacho hakifai kitu. Kama vile kikoi kinavyoshikamana na kiuno cha mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami watu wa Israeli na watu wa Yuda, ili wajulikane kwa jina langu, wanisifu na kunitukuza. Lakini wao hawakunisikiliza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Yeremia 13:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akaniambia hivi, Nenda ukajinunulie kitambaa cha kitani, ukajifunge kiunoni, wala usikitie majini. Basi nikanunua kitambaa cha kitani sawasawa na neno la BWANA, nikajivika viunoni. Nalo neno la BWANA likanijia mara ya pili, kusema, Twaa kitambaa kile ulichonunua, kilicho viunoni mwako, kisha ondoka, nenda mpaka mto Frati, ukaufiche huko katika pango la jabali. Basi nikaenda, nikakificha karibu na mto Frati, kama BWANA alivyoniamuru. Hata ikawa, baada ya siku nyingi, BWANA akaniambia, Ondoka, nenda mpaka mto Frati, ukakitwae kile kitambaa, nilichokuamuru kukificha huko. Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikakitwaa kile kitambaa katika mahali pale nilipokificha; na tazama, kitambaa kilikuwa kimeharibika, hakikufaa tena kwa lolote. Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema, BWANA asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu. Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na kitambaa hiki kisichofaa kwa lolote. Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na kiuno cha mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli; na nyumba yote ya Yuda, asema BWANA; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia.
Yeremia 13:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akaniambia hivi, Enenda, ukajinunulie mshipi wa kitani, ukajivike viuno, wala usiutie majini. Basi nikanunua mshipi sawasawa na neno la BWANA, nikajivika viunoni. Nalo neno la BWANA likanijia mara ya pili, kusema, Twaa mshipi ule ulioununua, ulio viunoni mwako, kisha ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukaufiche huko katika pango la jabali. Basi nikaenda, nikauficha karibu na mto Frati, kama BWANA alivyoniamuru. Hata ikawa, baada ya siku nyingi, BWANA akaniambia, Ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukautwae ule mshipi, niliokuamuru kuuficha huko. Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikautwaa ule mshipi katika mahali pale nilipouficha; na tazama, mshipi ulikuwa umeharibika, haukufaa tena kwa lo lote. Ndipo neno la BWANA likanijia, kusema, BWANA asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu. Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na mshipi huu, usiofaa kwa lo lote. Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na viuno vya mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli; na nyumba yote ya Yuda, asema BWANA; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia.
Yeremia 13:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hili ndilo BWANA aliloniambia: “Nenda ununue mkanda wa kitani, ujivike kiunoni mwako, lakini usiuache uguse maji.” Kwa hiyo nikanunua mkanda, kama BWANA alivyoniagiza, nikajivika kiunoni. Ndipo neno la BWANA likanijia kwa mara ya pili: “Chukua mkanda ulionunua ambao umeuvaa kiunoni mwako, uende sasa Frati uufiche ndani ya ufa mdogo kwenye mwamba.” Ndipo nikaenda na kuuficha ule mkanda huko Frati, kama BWANA alivyoniamuru. Baada ya siku nyingi BWANA akaniambia, “Nenda sasa Frati ukauchukue ule mkanda niliokuambia uufiche huko.” Hivyo nikaenda Frati na kuuchimbua ule mkanda kutoka pale nilipokuwa nimeuficha, lakini sasa ulikuwa umeharibika na haufai tena kabisa. Ndipo neno la BWANA likanijia: “Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Vivyo hivyo ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikuu cha Yerusalemu. Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wafuatao ukaidi wa mioyo yao na kufuata miungu mingine wakiitumikia na kuiabudu, watakuwa kama mshipi huu ambao haufai kabisa! Kwa maana kama vile mshipi ufungwavyo kiunoni mwa mtu, ndivyo nilivyoifunga nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda,’ asema BWANA, ‘ili wawe watu wangu kwa ajili ya utukufu wangu, sifa na heshima yangu. Lakini hawajasikiliza.’