Yeremia 1:4-14
Yeremia 1:4-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu aliniambia neno lake: “Kabla hujachukuliwa mimba, mimi nilikujua, kabla hujazaliwa, mimi nilikuweka wakfu; nilikuteua uwe nabii kwa mataifa.” Nami nikajibu, Aa! Bwana Mwenyezi-Mungu, mimi sijui kusema, kwa kuwa bado ningali kijana. Lakini Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Usiseme kwamba wewe ni kijana bado. Utakwenda kwa watu wote nitakaokutuma kwao, na yote nitakayokuamuru utayasema. Wewe usiwaogope watu hao, kwa maana niko pamoja nawe kukulinda. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Kisha Mwenyezi-Mungu akaunyosha mkono wake, akagusa kinywa changu, akaniambia, “Tazama nimeyatia maneno yangu kinywani mwako. Leo nimekupa mamlaka juu ya mataifa na falme, uwe na mamlaka ya kungoa na kubomoa, mamlaka ya kuharibu na kuangamiza, mamlaka ya kujenga na ya kupanda.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Yeremia, unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona tawi la mlozi unaochanua.” Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Umeona vizuri, maana niko macho kulitekeleza neno langu.” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili: “Unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona chungu kinatokota kimeinama upande wangu kutoka kaskazini.” Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Maangamizi yataanzia kutoka kaskazini na kuwapata wakazi wote wa nchi hii.
Yeremia 1:4-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nilikujua, na kabla hujatoka tumboni, nilikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini BWANA akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA. Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda. Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa mlozi. Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize. Neno la BWANA likanijia mara ya pili, kusema, Waona nini? Nikasema, Naona sufuria lenye maji yatokotayo, na mdomo wake unaelekea toka upande wa kaskazini. Ndipo BWANA akaniambia, Toka kaskazini mabaya yatatokea, na kuwapata watu wote wakaao katika nchi hii.
Yeremia 1:4-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini BWANA akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA. Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda. Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa mlozi. Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize. Neno la BWANA likanijia mara ya pili, kusema, Waona nini? Nikasema, Naona sufuria lenye maji yatokotayo, na mdomo wake unaelekea toka upande wa kaskazini. Ndipo BWANA akaniambia, Toka kaskazini mabaya yatatokea, na kuwapata watu wote wakaao katika nchi hii.
Yeremia 1:4-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno la BWANA lilinijia, kusema, “Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua; kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum; nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.” Nami nikasema, “Aa, BWANA Mwenyezi, sijui kusema, kwani mimi ni mtoto mdogo tu.” Lakini BWANA akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utaenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza. Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asema BWANA. Kisha BWANA akaunyoosha mkono wake na kugusa kinywa changu, akaniambia, “Sasa nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako. Tazama, leo nimekuweka juu ya mataifa na falme ili kungʼoa na kubomoa, kuharibu na kuangamiza, kujenga na kupanda.” Neno la BWANA likanijia kusema, “Je, Yeremia unaona nini?” Nami nikajibu, “Naona tawi la mti wa mlozi.” BWANA akaniambia, “Umeona vyema kwa maana ninaliangalia neno langu ili kuona kwamba limetimizwa.” Neno la BWANA likanijia tena, “Unaona nini?” Nikajibu, “Naona chungu kinachochemka, kikiwa kimeinama kutoka kaskazini.” BWANA akaniambia, “Kutoka kaskazini maafa yatamwagwa kwa wote wanaoishi katika nchi.