Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 8:1-29

Waamuzi 8:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)

Watu wa kabila la Efraimu wakamwuliza Gideoni, “Kwa nini umetutendea hivyo? Kwa nini hukutuita ulipokwenda kupigana na Wamidiani?” Wakamlaumu kwa ukali. Lakini Gideoni akawajibu, “Mambo niliyofanya mimi si kitu kabisa kama yakilinganishwa na yale mliyoyafanya nyinyi. Walichookota watu wa Efraimu baada ya mavuno ni chema na kizuri kuliko mavuno ya jamaa yangu ya Abiezeri. Mungu amewatia mikononi mwenu wakuu wa Midiani, Orebu, na Zeebu. Je, mimi nimefanya nini nikilinganishwa nanyi?” Gideoni alipokwisha sema hivyo, hasira yao dhidi yake ikatulia. Gideoni na wenzake 300 wakafika Yordani, wakavuka. Ingawa walikuwa wamechoka sana, waliendelea kuwafuatia adui zao. Basi, akawaambia watu wa Sukothi, “Tafadhali wapeni wenzangu hawa mikate maana wamechoka sana; nami bado ninaendelea kuwafuatia wafalme Zeba na Salmuna wa Midiani.” Lakini viongozi wa Sukothi wakamwuliza, “Kwa nini tuwape mikate nanyi bado hamjamshinda Zeba na Salmuna?” Gideoni akawaambia, “Sawa, lakini Mwenyezi-Mungu atakapowatia Zeba na Salmuna mikononi mwangu, nitaichanachana miili yenu kwa miiba na mbigili za jangwani.” Kutoka huko akawaendea watu wa Penueli, akawaomba namna ileile. Nao watu wa Penueli wakamjibu kama walivyomjibu watu wa Sukothi. Gideoni akawaambia, “Nitakaporudi kwa amani nitaubomoa mnara huu.” Zeba na Salmuna walikuwa huko Karkori pamoja na jeshi lao la watu 15,000 ambao ndio tu waliobaki kutoka jeshi la mashariki, maana wenzao 120,000 waliuawa. Gideoni akafuata njia ya magharibi iliyo mashariki mwa Noba na Yogbeha, akalishambulia jeshi hilo ambalo halikuwa tayari. Wafalme wa Midiani, Zeba na Salmuna walitoroka wakakimbia, lakini Gideoni aliwafuatia, akawakamata na kulitia jeshi lote hofu kubwa. Kisha, Gideoni, mwana wa Yoashi, akarudi kutoka vitani akipitia kwenye mteremko wa Heresi. Akamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumhoji. Kijana huyo akamwandikia majina ya viongozi na wazee mashuhuri wa Sukothi, jumla yao watu sabini na saba. Gideoni akarudi kwa watu wa Sukothi, akawaambia, “Si mtakumbuka mlivyonitukana mliposema, ‘Kwa nini tuwape mikate watu wako waliochoka sana nanyi bado hamjamshinda Zeba na Salmuna?’ Haya basi, Zeba na Salmuna ndio hawa.” Basi, akawachukua wazee wa Sukothi na kuwapa funzo wanaume wote kwa kuichana miili yao kwa miiba na mbigili. Vilevile akaubomoa mnara wa Penueli na kuwaua wakazi wa mji huo. Kisha, akawauliza Zeba na Salmuna, “Watu wale mliowaua huko Tabori walikuwaje?” Wakamjibu, “Walifanana na wewe, maana walionekana kama wana wa mfalme.” Naye akawaambia, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu mzazi. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kama msingewaua, hata mimi nisingewaua.” Kisha akamwambia Yetheri, mzaliwa wake wa kwanza, “Simama, uwaue.” Lakini Yetheri aliogopa kuchukua upanga wake maana alikuwa bado kijana. Hapo Zeba na Salmuna wakasema, “Tuue wewe mwenyewe, maana hii ni kazi ya mtu mzima.” Gideoni akawaua yeye mwenyewe na kuchukua mapambo yao yaliyokuwa shingoni mwa ngamia wao. Kisha, Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Wewe na uwe mtawala wetu, na baada yako watutawale wazawa wako, kwa kuwa wewe umetukomboa kutoka kwa Wamidiani.” Gideoni akawajibu, “Mimi sitakuwa mtawala wenu wala mwanangu hatakuwa mtawala wenu. Mwenyezi-Mungu ndiye atakayekuwa mtawala wenu.” Kisha akawaambia, “Ningependa kuwaomba kitu kimoja; naomba kila mmoja wenu anipe vipuli mlivyoteka nyara.” Wale Wamidiani kwa vile walikuwa Waishmaeli, walivaa vipuli vya dhahabu. Watu wakamjibu, “Tutakupa kwa hiari.” Wakatandaza nguo na kila mmoja akatupa humo vipuli walivyokuwa wameteka nyara. Uzito wa vipuli vyote alivyowataka wampe ulikuwa kilo ishirini. Zaidi ya hivyo, alipokea pia herini, mavazi ya urujuani yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani na mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia wao. Gideoni akazitumia kutengenezea kizibao ambacho alikiweka kwenye mji wake wa Ofra. Waisraeli wote wakaenda huko kukiabudu. Kizibao hicho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake. Basi, Wamidiani walishindwa kabisa wasiwe tishio kwa Israeli; na nchi ya Israeli ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini. Gideoni, yaani Yerubaali, mwana wa Yoashi akarudi nyumbani kwake na kukaa huko.

Shirikisha
Soma Waamuzi 8

Waamuzi 8:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi watu wa Efraimu wakamwambia, Kwa nini umetutendea haya? Hata usituite hapo ulipokwenda kupigana na Wamidiani? Nao wakamshutumu vikali. Lakini akawaambia, Je! Niliyoyafanya ni nini yakilinganishwa na yale mliyofanya ninyi? Hayo masazo ya zabibu za Efraimu si mema kuliko mavuno ya Abiezeri? Mungu amewatia hao wakuu wa Midiani, Orebu na Zeebu, mikononi mwenu; na mimi nilipata kufanya nini kama mlivyofanya ninyi? Ndipo hasira zao walizokuwa nazo juu yake zikatulia aliposema maneno hayo. Basi Gideoni akafika Yordani, akauvuka, yeye na hao watu mia tatu waliokuwa pamoja naye, walikuwa wamechoka, lakini waliendelea kuwafuatilia adui. Naye akawaambia watu wa Sukothi, Tafadhali wapeni mikate hao watu waniandamao; kwa maana wameishiwa na nguvu, nami ni katika kuwafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani. Hao wakuu wa Sukothi wakasema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna iko mkononi mwako sasa, hata sisi tukawape jeshi lako mikate? Ndipo Gideoni akasema, Kwa sababu hii, hapo BWANA atakapokuwa amewatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, ndipo nitaipura miili yenu kwa miiba ya nyikani, na kwa michongoma. Basi kutoka hapo alikwea kwenda Penieli, akasema na watu wa mahali hapo maneno kama hayo; watu wa Penieli nao wakamjibu kama vile watu wa Sukothi walivyomjibu. Naye akawaambia hao watu wa Penieli nao, akisema, Nitakapokuja tena kwa amani, nitaubomoa mnara huu. Basi hao kina Zebu na Salmuna walikuwa katika Karkori, na majeshi yao walikuwa pamoja nao, watu kama elfu kumi na tano hesabu yao, ni wote waliobaki wa hilo jeshi lote la hao wana wa mashariki; kwa sababu walianguka wapiganaji elfu mia moja na ishirini waliokuwa wakitumia upanga. Basi Gideoni alikwea kwa njia iliyotumiwa na misafara, ambayo ilikuwa mashariki mwa Noba na Yogbeha, akalishambulia hilo jeshi; kwa maana lile jeshi halikuwa na hadhari. Zeba na Salmuna walikimbia; naye akawaandamia; akawakamata hao wafalme wawili wa Midiani Zeba na Salmuna, akalitapanyatapanya hilo jeshi lote. Kisha huyo Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani, kutoka kwenye makweleo ya Heresi. Ndipo akamshika kijana mmoja mwanamume katika watu wa Sukothi, akamwuliza; naye akamwandikia majina ya hao wakuu wa Sukothi, na wazee wa mji, watu sabini na saba. Kisha akaufikia wale watu wa Sukothi, akawaambia, Tazama, Zeba na Salmuna, ambao ninyi mlinisimanga kwa ajili yao, mliposema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna iko sasa mikononi mwako wewe, hata tuwape watu wako waliochoka mikate? Basi akawatwaa hao wazee wa mji, na miiba ya nyikani na michongoma, akawafunza hao watu wa Sukothi kwayo. Kisha akaubomoa mnara wa Penieli, na kuwaua watu wa mji huo. Ndipo akawaambia hao Zeba na Salmuna, Hao watu mliowaua huko Tabori walikuwa watu wa namna gani? Wakamjibu, Walikuwa kama wewe ulivyo; kila mmoja alikuwa anafanana na wana wa mfalme. Naye akasema, Watu hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu; kama yeye BWANA aishivyo, kama mngaliwaokoa hai watu hao, nami nisingewaua ninyi. Kisha akamwambia Yetheri mwanawe mzaliwa wa kwanza, Haya, simama, uwaue hawa. Lakini huyo kijana hakutoa upanga wake; maana, akaogopa, kwa sababu alikuwa ni kijana tu. Ndipo hapo Zeba na Salmuna wakasema, Simama wewe utuue sisi; kwa maana kama mtu alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake. Basi Gideoni akasimama, akawaua Zeba na Salmuna, akazitwaa koja zilizokuwa katika shingo za ngamia wao. Ndipo watu wa Israeli wakamwambia Gideoni, Tawala wewe juu yetu, wewe, na mwanao, na mjukuu wako pia; kwa kuwa wewe umetuokoa na mikono ya Midiani. Gideoni akawaambia, Mimi sitatawala juu yenu wala mwanangu hatatawala juu yenu; yeye BWANA atatawala juu yenu. Kisha Gideoni akawaambia, Mimi nina haja yangu niitakayo kwenu, ni ya kila mtu kunipa hizo herini za mateka wake. (Kwa maana walikuwa na herini za dhahabu, kwa sababu walikuwa ni Waishmaeli.) Wakajibu, Tutakupa kwa moyo mweupe. Basi wakatandika nguo chini, wakatia humo kila mtu herini za mateka yake. Na uzani wa hizo herini za dhahabu alizozitaka ulipata shekeli za dhahabu elfu moja na mia saba; mbali na makoja na vidani, na mavazi ya rangi ya zambarau waliyokuwa wameyavaa hao wafalme wa Midiani, tena mbali na mikufu iliyokuwa katika shingo za ngamia wao. Basi Gideoni akafanya naivera kwa vitu vile, akaiweka katika mji wake, mji huo wa Ofra; nao Israeli wote wakaenda na kuiandama kwa ukahaba huko; nayo ilikuwa ni tanzi kwa Gideoni na kwa nyumba yake. Ndipo Midiani walishindwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arubaini katika siku za Gideoni. Kisha huyo Yerubaali, mwana wa Yoashi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe.

Shirikisha
Soma Waamuzi 8

Waamuzi 8:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi watu wa Efraimu wakamwambia, Kwa nini wewe kututendea sisi kama haya? Hata usituite, hapo ulipokwenda kupigana na Midiani? Nao wakateta naye sana. Lakini akawaambia, Je! Mimi nimefanya nini sasa kama mlivyofanya ninyi? Hayo masazo ya zabibu za Efraimu si mema kuliko mavuno ya Abiezeri? Mungu amewatia hao wakuu wa Midiani, Orebu na Zeebu, mikononi mwenu; na mimi nilipata kufanya nini kama mlivyofanya ninyi? Ndipo hasira zao walizokuwa nazo juu yake zikatulia aliposema maneno hayo. Basi Gideoni akafika Yordani, akauvuka, yeye na hao watu mia tatu waliokuwa pamoja naye, walikuwa wamepungukiwa na nguvu, lakini wawafuatia vivyo. Naye akawaambia watu wa Sukothi, Tafadhali wapeni mikate hao watu waniandamao; kwa maana wanapungukiwa na nguvu, nami ni katika kuwafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani. Hao wakuu wa Sukothi wakasema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna i mkononi mwako sasa, hata sisi tukawape jeshi lako mikate? Ndipo Gideoni akasema, Kwa sababu hii, hapo BWANA atakapokuwa amewatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, ndipo nitaipura nyama ya miili yenu kwa miiba ya nyikani, na kwa michongoma. Basi kutoka hapo alikwea kwenda Penieli, akasema na watu wa mahali hapo maneno kama hayo; watu wa Penieli nao wakamjibu kama vile watu wa Sukothi walivyomjibu. Naye akawaambia hao watu wa Penieli nao, akisema, Nitakapokuja tena kwa amani, nitauvunja mnara huu. Basi hao kina Zebu na Salmuna walikuwa katika Karkori, na majeshi yao walikuwa pamoja nao, watu kama kumi na tano elfu hesabu yao, ni wote waliobaki wa hilo jeshi lote la hao wana wa mashariki; kwa sababu walianguka watu mia na ishirini elfu waliokuwa wenye kutumia upanga. Basi Gideoni alikwea kwa njia ya hao waliokuwa wenye kukaa hemani upande wa mashariki wa Noba na Yogbeha, akalipiga hilo jeshi; kwa maana lile jeshi lilikuwa salama. Zeba na Salmuna walikimbia; naye akawaandamia; akawakamata hao wafalme wawili wa Midiani Zeba na Salmuna, akalitapanya-tapanya hilo jeshi lote. Kisha huyo Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani, kutoka kwenye makweleo ya Heresi. Ndipo akamshika mtu mmoja hirimu katika watu wa Sukothi, akamwuliza; naye akamwandikia majina ya hao wakuu wa Sukothi, na wazee wa mji, watu sabini na saba. Kisha akawafikilia wale watu wa Sukothi, akawaambia, Tazama, Zeba na Salmuna, ambao ninyi mlinisimanga kwa ajili yao, mliposema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna iko sasa mikononi mwako wewe, hata tuwape watu wako waliochoka mikate? Basi akawatwaa hao wazee wa mji, na miiba ya nyikani na michongoma, akawafunza hao watu wa Sukothi kwayo. Kisha akaupomosha mnara wa Penieli, na kuwaua watu wa mji huo. Ndipo akawaambia hao Zeba na Salmuna, Hao watu mliowaua huko Tabori walikuwa watu wa namna gani? Wakamjibu, Walikuwa kama wewe ulivyo; kila mmoja alikuwa anafanana na wana wa mfalme. Naye akasema, Watu hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mamaangu mimi; kama yeye BWANA alivyo hai, kwamba mliwaokoa hai watu hao, mimi nisingewaua ninyi. Kisha akamwambia Yetheri mwanawe mzaliwa wa kwanza, Haya, simama, uwaue hawa. Lakini huyo kijana hakutoa upanga wake; maana, akacha, kwa sababu alikuwa ni kijana tu. Ndipo hapo Zeba na Salmuna wakasema, Simama wewe ukatuangukie sisi; kwa maana kama mtu alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake. Basi Gideoni akasimama, akawaua Zeba na Salmuna, akazitwaa koja zilizokuwa katika shingo za ngamia zao. Ndipo watu wa Israeli wakamwambia Gideoni, Tawala wewe juu yetu, wewe, na mwanao, na mjukuu wako pia; kwa kuwa wewe umetuokoa na mikono ya Midiani. Gideoni akawaambia, Mimi sitatawala juu yenu wala mwanangu hatatawala juu yenu; yeye BWANA atatawala juu yenu. Kisha Gideoni akawaambia, Mimi nina haja yangu niitakayo kwenu, ni ya kila mtu kunipa hizo pete za masikio ya mateka yake. (Kwa maana walikuwa na pete za masikio za dhahabu, kwa sababu walikuwa ni Waishmaeli.) Wakajibu, Tutakupa kwa mioyo. Basi wakatandika nguo chini, wakatia humo kila mtu pete za masikio ya mateka yake. Na uzani wa hizo pete za dhahabu alizozitaka ulipata shekeli za dhahabu elfu moja na mia saba; mbali na makoja na vidani, na mavazi ya rangi ya zambarau waliyokuwa wameyavaa hao wafalme wa Midiani, tena mbali na mikufu iliyokuwa katika shingo za ngamia zao. Basi Gideoni akafanya naivera kwa vitu vile, akaiweka katika mji wake, mji huo wa Ofra; nao Israeli wote wakaenda na kuiandama kwa ukahaba huko; nayo ilikuwa ni tanzi kwa Gideoni na kwa nyumba yake. Hivyo Midiani walishindwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arobaini katika siku za Gideoni. Kisha huyo Yerubaali, mwana wa Yoashi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe.

Shirikisha
Soma Waamuzi 8

Waamuzi 8:1-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi Waefraimu wakamuuliza Gideoni, “Mbona umetutenda hivi? Kwa nini hukutuita ulipoenda kupigana na Wamidiani?” Wakamlaumu kwa ukali sana. Gideoni akawajibu, “Nilichofanya mimi ni nini kulinganisha na kile ninyi mlichofanya? Je, kuokoa masazo ya zabibu za Efraimu si bora kuliko mavuno kamili ya zabibu ya Abiezeri? Mungu amewatia Orebu na Zeebu, hao viongozi wa Wamidiani, mikononi mwenu. Je, mimi niliweza kufanya nini kulinganisha na mlichofanya ninyi?” Aliposema hili, hasira yao dhidi yake ikatulia. Gideoni pamoja na watu wake mia tatu, wakiwa wamechoka sana lakini bado wakiwafuatia, wakafika Yordani na kuuvuka. Akawaambia wanaume wa Sukothi, “Tafadhali lipatieni jeshi langu mikate, kwa maana wamechoka, nami ningali ninawafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani.” Lakini viongozi wa Sukothi wakasema, “Je, tayari umewakamata Zeba na Salmuna ili tulipatie jeshi lako mikate?” Gideoni akajibu, “Kwa ajili ya hilo tu, BWANA atakapowatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, nitaichana nyama ya miili yenu kwenye miiba ya nyikani na kwenye michongoma.” Kutoka hapo alikwea hadi Penieli na kutoa ombi lile lile, lakini nao wanaume wa Penieli wakamjibu kama wanaume wa Sukothi walivyokuwa wamemjibu. Hivyo akawaambia wanaume wa Penieli, “Nitakaporudi kwa ushindi, nitaubomoa mnara huu.” Wakati huu Zeba na Salmuna walikuwa Karkori, wakiwa na jeshi la watu wapatao elfu kumi na tano waliokuwa wamesalia wa mataifa ya mashariki, kwa kuwa watu wapatao elfu mia moja na ishirini wenye panga walikuwa wameuawa. Basi Gideoni akakwea kwa njia ya wafugaji wahamaji mashariki mwa Noba na Yogbeha, na kulishambulia jeshi ambalo halikushuku lolote. Zeba na Salmuna, hao wafalme wawili wa Midiani, wakakimbia lakini yeye Gideoni akawafuata na kuwakamata, akalishinda hilo jeshi lao lote kabisa. Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani kupitia Mwinuko wa Heresi. Akamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumuuliza maswali, naye yule kijana akamwandikia majina ya viongozi sabini na saba wa Sukothi, ambao ni wazee wa mji. Ndipo Gideoni akaja na kuwaambia wanaume wa Sukothi, “Tazameni Zeba na Salmuna mlionisimanga kwa ajili yao mkisema, ‘Je, tayari umewakamata Zeba na Salmuna ili tulipatie jeshi lako mikate?’ ” Akawachukua hao wazee wa mji, na kuwaadhibu wanaume wa Sukothi kwa kuwachapa kwa miiba na michongoma ya nyikani. Pia akaubomoa mnara wa Penieli na kuwaua wanaume wa huo mji. Kisha akawauliza Zeba na Salmuna, “Ni wanaume wa aina gani mliowaua huko Tabori?” Wakajibu, “Ni wanaume kama wewe, kila mmoja wao akiwa anafanana na mwana wa mfalme.” Gideoni akajibu, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu hasa. Hakika kama BWANA aishivyo, kama mngekuwa mmewaacha hai, mimi nisingewaua ninyi.” Akamgeukia Yetheri, mwanawe mzaliwa wa kwanza, akasema, “Waue hawa!” Lakini Yetheri hakuufuta upanga wake, kwa sababu aliogopa, kwa kuwa alikuwa bado kijana mdogo tu. Zeba na Salmuna wakasema, “Njoo ufanye hivyo wewe mwenyewe. ‘Alivyo mwanaume, ndivyo zilivyo nguvu zake.’ ” Hivyo, Gideoni akajitokeza na kuwaua, naye akayaondoa mapambo kwenye shingo za ngamia wao. Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Ututawale, wewe, mwanao, na mjukuu wako, kwa kuwa umetuokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani.” Lakini Gideoni akawaambia, “Mimi sitawatawala ninyi, wala mwanangu hatawatawala. BWANA ndiye atakayewatawala ninyi.” Naye akasema, “Ninalo ombi moja, kwamba kila mmoja wenu anipatie kipuli kutoka fungu lake la nyara.” (Ilikuwa desturi ya Waishmaeli kuvaa vipuli vya dhahabu.) Wakajibu, “Tutafurahi kuvitoa.” Hivyo wakatanda vazi chini na kila mwanaume akatupia juu yake pete kutoka fungu lake la nyara. Uzito wa pete za dhahabu alizoomba ulikuwa shekeli elfu moja na mia saba, bila kuhesabu mapambo mengine, vidani, na mavazi ya zambarau yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani, au mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia wao. Gideoni akatengeneza kizibau kwa kutumia ile dhahabu, ambacho alikiweka katika mji wake, yaani Ofra. Waisraeli wote wakafanya uasherati kwa kukiabudu huko, nacho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake. Hivyo Midiani wakashindwa mbele ya Waisraeli, nao hawakuinua vichwa vyao tena. Wakati wa siku za uhai wa Gideoni, nchi ikafurahia amani miaka arobaini. Yerub-Baali mwana wa Yoashi akarudi kwenda kuishi katika nyumba yake.

Shirikisha
Soma Waamuzi 8