Waamuzi 7:9-15
Waamuzi 7:9-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Usiku huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Nenda ukawashambulie kambini mwao, maana nimewatia mikononi mwako. Lakini kama unaogopa, nenda pamoja na mtumishi wako Pura. Huko utasikia wanayosema, nawe utapata nguvu za kuweza kwenda kuwashambulia.” Basi, Gideoni akaenda pamoja na mtumishi wake Pura mpaka kwenye vituo vya walinda zamu wa kambi ya Wamidiani. Wamidiani, Waamaleki na watu wote wa Mashariki walilala bondeni, wengi kama nzige, na ngamia wao wasiohesabika, wengi kama mchanga wa pwani. Gideoni alipofika, akamsikia mtu mmoja akimsimulia mwenzake ndoto yake hivi: “Niliota ndoto. Niliona mkate wa shayiri ukivingirika hadi kambini mwa Wamidiani, ukalipiga hema na kulipindua chini juu. Hema likalala chini.” Mwenzake akamjibu, “Hiyo inamaanisha tu upanga wa yule Mwisraeli Gideoni mwana wa Yoashi ambaye mikononi mwake Mungu amewatia Wamidiani pamoja na jeshi lote.” Gideoni aliposikia masimulizi hayo ya ndoto na tafsiri yake, alimwabudu Mungu. Kisha alirudi kwenye kambi ya Waisraeli, akasema, “Amkeni twende; maana Mwenyezi-Mungu amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.”
Waamuzi 7:9-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako. Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini; nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya, mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hadi katika vituo vya walinda zamu wa kambi ya Wamidiani. Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia wao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi. Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, niliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika katika hema moja, ukaipiga hadi ikaanguka, ukaipindua, hadi ikalala chini. Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake. Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana BWANA amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu.
Waamuzi 7:9-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako. Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini; nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hata kufikilia mwisho wa watu wenye silaha waliokuwa kambini. Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia zao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi. Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini. Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake. Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana BWANA amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu.
Waamuzi 7:9-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Usiku ule ule BWANA akamwambia Gideoni, “Ondoka, ushuke ushambulie kambi, kwa kuwa nimeitia mkononi mwako. Lakini kama unaogopa kushambulia, shuka kambini pamoja na mtumishi wako Pura, nawe sikiliza wanayosema. Hatimaye, utatiwa moyo kushambulia kambi.” Basi yeye na Pura, mtumishi wake, wakashuka na kuwafikia walinzi wa mbele wa kambi. Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine yote ya mashariki walikaa bondeni, nao walikuwa mfano wa nzige kwa wingi wao. Ngamia wao hawangehesabika, wingi wao ulikuwa kama mchanga wa ufuoni mwa bahari. Gideoni alifika mara tu mtu mmoja alipokuwa akimweleza mwenzake ndoto yake, akisema, “Tazama, niliota ndoto, mkate wa shayiri ulioviringana ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukaipiga hema kwa nguvu, na kusababisha hema hilo kupinduka na kuporomoka.” Rafiki yake akamjibu, “Habari hii si kitu kingine isipokuwa upanga wa Gideoni mwana wa Yoashi, Mwisraeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote mkononi mwake.” Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akasujudu na kuabudu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni! BWANA amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.”