Waamuzi 7:13-25
Waamuzi 7:13-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Gideoni alipofika, akamsikia mtu mmoja akimsimulia mwenzake ndoto yake hivi: “Niliota ndoto. Niliona mkate wa shayiri ukivingirika hadi kambini mwa Wamidiani, ukalipiga hema na kulipindua chini juu. Hema likalala chini.” Mwenzake akamjibu, “Hiyo inamaanisha tu upanga wa yule Mwisraeli Gideoni mwana wa Yoashi ambaye mikononi mwake Mungu amewatia Wamidiani pamoja na jeshi lote.” Gideoni aliposikia masimulizi hayo ya ndoto na tafsiri yake, alimwabudu Mungu. Kisha alirudi kwenye kambi ya Waisraeli, akasema, “Amkeni twende; maana Mwenyezi-Mungu amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.” Basi akawagawa wale watu 300 katika makundi matatu, akawapa tarumbeta na magudulia yenye mienge. Akawaambia, “Mniangalie na kufanya sawa kama nitakavyofanya wakati nitakapofika kambini. Nitakapopiga tarumbeta, mimi pamoja na kundi langu, nyote pigeni tarumbeta kutoka kila upande na kusema kwa sauti kubwa, ‘Kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kwa ajili ya Gideoni!’” Ilipokaribia usiku wa manane, Gideoni na kundi lake la watu mia moja mara tu baada ya kufika mwisho wa kambi, mwanzoni mwa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu walikaribia kambi ya adui. Wakapiga tarumbeta na kuvunja magudulia waliyokuwa nayo. Makundi yote matatu kwa pamoja yakapiga tarumbeta na kuvunja magudulia yao. Katika mikono yao ya kushoto walishika mienge na kwa mikono yao ya kulia tarumbeta na kuzipiga, huku wakisema kwa sauti kubwa, “Upanga kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kwa ajili ya Gideoni!” Wakasimama kila mmoja mahali pake kuizunguka kambi. Jeshi lote la adui likatawanyika huku likipiga mayowe. Watu wa Gideoni walipopiga tarumbeta zao 300, Mwenyezi-Mungu aliwafanya Wamidiani waanze kuuana wao kwa wao kambini. Waliosalia wakatoroka hadi Serera panapoelekea Beth-shita, hadi mpakani mwa Abel-mehola karibu na Tabathi. Waisraeli wa kabila la Naftali, Asheri, na Manase, wote waliitwa, wakawafuatia Wamidiani. Gideoni akatuma wajumbe kote katika nchi ya milima ya Efraimu watangaze: “Teremkeni kuwakabili Wamidiani na kuwazuia kwa kuteka vijito na mto Yordani mpaka Beth-bara.” Basi, wanaume wote wa Efraimu wakaja na kuuteka mto Yordani mpaka Beth-bara. Wakachukua mateka viongozi wawili wa Midiani, yaani Orebu na Zeebu. Wakamuua Orebu katika mwamba wa Orebu, naye Zeebu wakamuua katika shinikizo la Zeebu, wakiwa wanawafuatia Wamidiani. Wakamletea Gideoni vichwa vya Orebu na Zeebu, ngambo ya mto Yordani.
Waamuzi 7:13-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, niliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika katika hema moja, ukaipiga hadi ikaanguka, ukaipindua, hadi ikalala chini. Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake. Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana BWANA amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu. Kisha akawapanga wale watu mia tatu wawe vikosi vitatu, akatia tarumbeta katika mikono ya watu wote, na mitungi isiyo na maji, na mienge ndani ya hiyo mitungi. Akawaambia, Nitazameni, mkafanye kama nifanyavyo mimi; angalieni, nitakapofika mwisho wa kambi, itakuwa, nifanyavyo mimi nanyi fanyeni vivyo hivyo. Nitakapopiga tarumbeta, mimi na wote walio pamoja nami, basi ninyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi, mkaseme, Kwa BWANA, na kwa Gideoni. Basi Gideoni, na wale watu mia moja waliokuwa pamoja naye, wakafika mwisho wa kambi, mwanzo wa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu; wakazipiga hizo tarumbeta, wakaivunja vipande vipande ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. Vile vikosi vitatu wakapiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kulia ili kuzipiga; wakapiga kelele, Upanga wa BWANA na wa Gideoni. Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele, wakawakimbiza. Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye BWANA akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuelekea Serera, hadi mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi. Wanaume wa Israeli walikuwa wamekusanyika kutoka Naftali, na kutoka Asheri, na kutoka Manase yote, wakawafuata Midiani. Kisha Gideoni akatuma wajumbe katika nchi yote ya vilima vilima ya Efraimu, akisema, Haya, teremkeni juu ya Midiani, na kuyatwaa hayo maji mbele yao, mpaka Bethbara, maana huo mto wa Yordani. Basi wanaume wote wa Efraimu walitokeza wakayatwaa maji mpaka Bethbara, yaani, huo mto wa Yordani. Wakawashika hao wakuu wawili wa Midiani, Orebu na Zeebu; wakamwua huyo Orebu pale penye jabali la Orebu, na huyo Zeebu wakamwua hapo penye shinikizo la divai la Zeebu, kisha wakawaandamia Wamidiani; vichwa vya Orebu na Zeebu wakamletea Gideoni huko ng'ambo ya pili ya Yordani.
Waamuzi 7:13-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini. Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake. Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana BWANA amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu. Kisha akawapanga wale watu mia tatu wawe vikosi vitatu, akatia tarumbeta katika mikono ya watu wote, na mitungi isiyo maji, na mienge ndani ya hiyo mitungi. Akawaambia, Nitazameni, mkafanye kama nifanyavyo mimi; angalieni, nitakapofika mwisho wa kambi, itakuwa, nifanyavyo mimi nanyi fanyeni kadhalika. Nitakapopiga tarumbeta, mimi na wote walio pamoja nami, basi ninyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi, mkaseme, Kwa BWANA, na kwa Gideoni. Basi Gideoni, na wale watu mia waliokuwa pamoja naye, wakafika mwisho wa kambi, mwanzo wa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu; wakazipiga hizo tarumbeta, wakaivunja vipande vipande ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. Vile vikosi vitatu wakapiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga; wakapiga kelele, Upanga wa BWANA na wa Gideoni. Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele, wakawakimbiza. Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye BWANA akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuendelea Serera, hata mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi. Wanaume wa Israeli walikuwa wamekusanyika kutoka Naftali, na kutoka Asheri, na kutoka Manase yote, wakawafuata Midiani. Kisha Gideoni akapeleka wajumbe katika nchi yote ya vilima vilima ya Efraimu, akisema, Haya, telemkeni juu ya Midiani, na kuyashika hayo maji mbele yao, mpaka Bethbara, maana, huo mto wa Yordani. Basi watu waume wote wa Efraimu walikutana pamoja, wakayashika maji mpaka Bethbara, maana, huo mto wa Yordani. Wakawashika hao wakuu wawili wa Midiani, Orebu na Zeebu; wakamwua huyo Orebu pale penye jabali la Orebu, na huyo Zeebu wakamwua hapo penye shinikizo la divai la Zeebu, kisha wakawaandamia Wamidiani; vichwa vya Orebu na Zeebu wakamletea Gideoni huko ng’ambo ya pili ya Yordani.
Waamuzi 7:13-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Gideoni alifika mara tu mtu mmoja alipokuwa akimweleza mwenzake ndoto yake, akisema, “Tazama, niliota ndoto, mkate wa shayiri ulioviringana ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukaipiga hema kwa nguvu, na kusababisha hema hilo kupinduka na kuporomoka.” Rafiki yake akamjibu, “Habari hii si kitu kingine isipokuwa upanga wa Gideoni mwana wa Yoashi, Mwisraeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote mkononi mwake.” Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akasujudu na kuabudu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni! BWANA amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.” Akawagawa wale watu mia tatu katika makundi matatu, akawakabidhi tarumbeta mikononi mwao wote, na mitungi mitupu, na mienge ikawekwa ndani yake. Akawaambia, “Nitazameni, fanyeni kama nitakavyofanya. Nitakapofika mwisho wa kambi, mfanye kama nitakavyofanya. Mimi na wote walio pamoja nami tutakapopiga tarumbeta zetu, ninyi nanyi pigeni tarumbeta pande zote za kambi na mpige kelele, mseme, ‘Upanga wa BWANA na wa Gideoni.’ ” Gideoni na wale watu mia moja waliokuwa pamoja naye wakafika mwisho wa kambi usiku mwanzoni mwa zamu ya kati, mara tu walipokuwa wamebadili zamu. Wakapiga zile tarumbeta zao, na kuvunja ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. Yale makundi matatu wakapiga tarumbeta na kuvunja mitungi. Wakashika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga. Wakapaza sauti zao, wakisema, “Upanga wa BWANA, na wa Gideoni!” Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote, Wamidiani wote wakakimbia, huku wakipiga kelele. Walipozipiga zile tarumbeta mia tatu, BWANA akafanya watu katika kambi yote kugeukiana kila mmoja na mwenziwe kwa upanga. Jeshi likakimbia hadi Beth-Shita kuelekea Serera, hadi mpakani mwa Abel-Mehola karibu na Tabathi. Wanaume Waisraeli wakaitwa kutoka Naftali, Asheri na Manase yote, nao wakawafuatia Wamidiani. Gideoni akatuma wajumbe katika nchi yote ya vilima ya Efraimu, akisema, “Teremkeni dhidi ya Wamidiani na mkazuie vivuko vya maji mbele yao hadi Beth-Bara na pia Yordani.” Hivyo wanaume wote wa Efraimu wakakutanika pamoja na kuzingira vivuko vya maji mbele yao hadi Beth-Bara na pia Yordani. Wakawakamata Orebu na Zeebu, wakuu wawili wa Midiani. Wakamuua Orebu pale penye mwamba wa Orebu, na Zeebu wakamuua pale penye shinikizo la kukamulia zabibu la Zeebu. Wakawafuatia Wamidiani na kuleta vichwa vya Orebu na Zeebu kwa Gideoni, huko ngʼambo ya Yordani.