Waamuzi 7:1-8
Waamuzi 7:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Yerubaali, yaani Gideoni na watu wote waliokuwa pamoja naye waliamka mapema, wakapiga kambi yao bondeni karibu na chemchemi ya Harodi; kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini mwao bondeni karibu na mlima More. Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Watu ulio nao ni wengi mno kwangu mimi kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Waisraeli wasije wakajisifu mbele yangu na kusema kwamba wamejiokoa kwa nguvu zao wenyewe. Sasa watangazie watu wote kwamba mtu yeyote aliye mwoga au anayetetemeka arudi nyumbani kwake.” Basi, Gideoni aliwajaribu, na watu 22,000 wakarudi nyumbani akabaki na watu 10,000. Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Watu hao bado ni wengi mno. Sasa wapeleke mtoni, nami nitawajaribu huko. Mtu yeyote nitakayekuambia, ‘Huyu atakwenda nawe, huyo aende nawe. Lakini mtu yeyote nitakayekuambia hatakwenda nawe, huyo asiende nawe.’” Basi, Gideoni akawapeleka watu mtoni na Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Watu watakaoramba maji kama mbwa, utawatenganisha na wale watakaopiga magoti kunywa maji.” Idadi ya waliokunywa maji kwa kuchota kwa mikono yao na kuramba kama mbwa ilikuwa 300. Lakini wengine wote waliobaki walipiga magoti kunywa maji. Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Kwa hao watu 300 waliokunywa kwa kuramba kama mbwa, nitawaokoa Waisraeli na kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Lakini wale wengine wote warudi makwao.” Basi, Gideoni akachukua vyakula vya wale waliokuwa wanaondoka na tarumbeta, akawaaga waende makwao. Yeye akabaki na wale watu 300. Kambi ya Wamidiani ilikuwa bondeni upande wao wa chini.
Waamuzi 7:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka asubuhi na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni. BWANA akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno kwangu kuwatia Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa. Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu yeyote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu elfu ishirini na mbili wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi. BWANA akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; walete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda. Basi akawaleta watu chini majini. BWANA akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa. Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji. BWANA akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake. Basi Gideoni akachukua vyakula vyao na tarumbeta zao, kisha akawaaga watu wote wa Israeli, kila mtu hemani mwake; akabaki na watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni.
Waamuzi 7:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni. BWANA akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa. Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu awaye yote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu ishirini na mbili elfu wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi. BWANA akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; uwalete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda. Basi akawaleta watu chini majini. BWANA akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa. Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji. BWANA akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake. Basi wale watu wakachukua vyakula vyao mikononi mwao, na tarumbeta zao; naye akawapeleka watu wote wa Israeli, kila mtu hemani kwake; bali aliwazuia wale watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni.
Waamuzi 7:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Yerub-Baali (yaani Gideoni) na lile jeshi lililokuwa pamoja naye, wakaondoka asubuhi na mapema na kupiga kambi kando ya chemchemi ya Harodi. Kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini mwao katika bonde, karibu na kilima cha More. BWANA akamwambia Gideoni, “Jeshi lililo pamoja nawe ni kubwa sana kwangu kuwatia Wamidiani mikononi mwao, Israeli asije akajisifu juu yangu, akisema, ‘Mkono wangu ndio uliniokoa.’ Kwa hiyo sasa tangaza jeshi lote likiwa linasikia, kwamba: ‘Yeyote anayeogopa na kutetemeka, yeye na arudi nyumbani, aondoke katika Mlima Gileadi.’ ” Hivyo, watu elfu ishirini na mbili wakarudi nyumbani, wakabaki elfu kumi. Lakini BWANA akamwambia Gideoni, “Idadi ya jeshi bado ni kubwa. Wapeleke kwenye maji, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako. Nikikuambia, ‘Huyu ataenda pamoja nawe,’ yeye ataenda; lakini nikisema, ‘Huyu hataenda pamoja nawe,’ yeye hataenda.” Gideoni akalipeleka lile jeshi kwenye maji, naye BWANA akamwambia Gideoni, “Watenganishe watakaoramba maji kwa ulimi kama mbwa, na wale watakaopiga magoti ili kunywa.” Waliokunywa kwa kuramba maji kutoka mikononi mwao walikuwa watu mia tatu. Wengine wote walipiga magoti ili kunywa. BWANA akamwambia Gideoni, “Kupitia hao watu mia tatu walioramba maji nitawaokoa ninyi, nami nitawatia Wamidiani mkononi mwako. Waache hao watu wengine wote warudi kila mmoja nyumbani mwake.” Hivyo Gideoni akawaruhusu wale Waisraeli wengine kila mmoja aende kwenye hema lake. Akabakia na wale mia tatu, nao wakachukua vyakula na tarumbeta za wenzao. Basi kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake bondeni.