Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 7:1-22

Waamuzi 7:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Yerubaali, yaani Gideoni na watu wote waliokuwa pamoja naye waliamka mapema, wakapiga kambi yao bondeni karibu na chemchemi ya Harodi; kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini mwao bondeni karibu na mlima More. Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Watu ulio nao ni wengi mno kwangu mimi kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Waisraeli wasije wakajisifu mbele yangu na kusema kwamba wamejiokoa kwa nguvu zao wenyewe. Sasa watangazie watu wote kwamba mtu yeyote aliye mwoga au anayetetemeka arudi nyumbani kwake.” Basi, Gideoni aliwajaribu, na watu 22,000 wakarudi nyumbani akabaki na watu 10,000. Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Watu hao bado ni wengi mno. Sasa wapeleke mtoni, nami nitawajaribu huko. Mtu yeyote nitakayekuambia, ‘Huyu atakwenda nawe, huyo aende nawe. Lakini mtu yeyote nitakayekuambia hatakwenda nawe, huyo asiende nawe.’” Basi, Gideoni akawapeleka watu mtoni na Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Watu watakaoramba maji kama mbwa, utawatenganisha na wale watakaopiga magoti kunywa maji.” Idadi ya waliokunywa maji kwa kuchota kwa mikono yao na kuramba kama mbwa ilikuwa 300. Lakini wengine wote waliobaki walipiga magoti kunywa maji. Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Kwa hao watu 300 waliokunywa kwa kuramba kama mbwa, nitawaokoa Waisraeli na kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Lakini wale wengine wote warudi makwao.” Basi, Gideoni akachukua vyakula vya wale waliokuwa wanaondoka na tarumbeta, akawaaga waende makwao. Yeye akabaki na wale watu 300. Kambi ya Wamidiani ilikuwa bondeni upande wao wa chini. Usiku huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Nenda ukawashambulie kambini mwao, maana nimewatia mikononi mwako. Lakini kama unaogopa, nenda pamoja na mtumishi wako Pura. Huko utasikia wanayosema, nawe utapata nguvu za kuweza kwenda kuwashambulia.” Basi, Gideoni akaenda pamoja na mtumishi wake Pura mpaka kwenye vituo vya walinda zamu wa kambi ya Wamidiani. Wamidiani, Waamaleki na watu wote wa Mashariki walilala bondeni, wengi kama nzige, na ngamia wao wasiohesabika, wengi kama mchanga wa pwani. Gideoni alipofika, akamsikia mtu mmoja akimsimulia mwenzake ndoto yake hivi: “Niliota ndoto. Niliona mkate wa shayiri ukivingirika hadi kambini mwa Wamidiani, ukalipiga hema na kulipindua chini juu. Hema likalala chini.” Mwenzake akamjibu, “Hiyo inamaanisha tu upanga wa yule Mwisraeli Gideoni mwana wa Yoashi ambaye mikononi mwake Mungu amewatia Wamidiani pamoja na jeshi lote.” Gideoni aliposikia masimulizi hayo ya ndoto na tafsiri yake, alimwabudu Mungu. Kisha alirudi kwenye kambi ya Waisraeli, akasema, “Amkeni twende; maana Mwenyezi-Mungu amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.” Basi akawagawa wale watu 300 katika makundi matatu, akawapa tarumbeta na magudulia yenye mienge. Akawaambia, “Mniangalie na kufanya sawa kama nitakavyofanya wakati nitakapofika kambini. Nitakapopiga tarumbeta, mimi pamoja na kundi langu, nyote pigeni tarumbeta kutoka kila upande na kusema kwa sauti kubwa, ‘Kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kwa ajili ya Gideoni!’” Ilipokaribia usiku wa manane, Gideoni na kundi lake la watu mia moja mara tu baada ya kufika mwisho wa kambi, mwanzoni mwa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu walikaribia kambi ya adui. Wakapiga tarumbeta na kuvunja magudulia waliyokuwa nayo. Makundi yote matatu kwa pamoja yakapiga tarumbeta na kuvunja magudulia yao. Katika mikono yao ya kushoto walishika mienge na kwa mikono yao ya kulia tarumbeta na kuzipiga, huku wakisema kwa sauti kubwa, “Upanga kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kwa ajili ya Gideoni!” Wakasimama kila mmoja mahali pake kuizunguka kambi. Jeshi lote la adui likatawanyika huku likipiga mayowe. Watu wa Gideoni walipopiga tarumbeta zao 300, Mwenyezi-Mungu aliwafanya Wamidiani waanze kuuana wao kwa wao kambini. Waliosalia wakatoroka hadi Serera panapoelekea Beth-shita, hadi mpakani mwa Abel-mehola karibu na Tabathi.

Shirikisha
Soma Waamuzi 7

Waamuzi 7:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka asubuhi na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni. BWANA akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno kwangu kuwatia Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa. Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu yeyote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu elfu ishirini na mbili wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi. BWANA akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; walete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda. Basi akawaleta watu chini majini. BWANA akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa. Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji. BWANA akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake. Basi Gideoni akachukua vyakula vyao na tarumbeta zao, kisha akawaaga watu wote wa Israeli, kila mtu hemani mwake; akabaki na watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni. Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako. Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini; nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya, mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hadi katika vituo vya walinda zamu wa kambi ya Wamidiani. Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia wao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi. Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, niliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika katika hema moja, ukaipiga hadi ikaanguka, ukaipindua, hadi ikalala chini. Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake. Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana BWANA amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu. Kisha akawapanga wale watu mia tatu wawe vikosi vitatu, akatia tarumbeta katika mikono ya watu wote, na mitungi isiyo na maji, na mienge ndani ya hiyo mitungi. Akawaambia, Nitazameni, mkafanye kama nifanyavyo mimi; angalieni, nitakapofika mwisho wa kambi, itakuwa, nifanyavyo mimi nanyi fanyeni vivyo hivyo. Nitakapopiga tarumbeta, mimi na wote walio pamoja nami, basi ninyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi, mkaseme, Kwa BWANA, na kwa Gideoni. Basi Gideoni, na wale watu mia moja waliokuwa pamoja naye, wakafika mwisho wa kambi, mwanzo wa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu; wakazipiga hizo tarumbeta, wakaivunja vipande vipande ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. Vile vikosi vitatu wakapiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kulia ili kuzipiga; wakapiga kelele, Upanga wa BWANA na wa Gideoni. Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele, wakawakimbiza. Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye BWANA akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuelekea Serera, hadi mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi.

Shirikisha
Soma Waamuzi 7

Waamuzi 7:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni. BWANA akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa. Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu awaye yote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu ishirini na mbili elfu wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi. BWANA akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; uwalete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda. Basi akawaleta watu chini majini. BWANA akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa. Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji. BWANA akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake. Basi wale watu wakachukua vyakula vyao mikononi mwao, na tarumbeta zao; naye akawapeleka watu wote wa Israeli, kila mtu hemani kwake; bali aliwazuia wale watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni. Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako. Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini; nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hata kufikilia mwisho wa watu wenye silaha waliokuwa kambini. Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia zao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi. Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini. Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake. Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana BWANA amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu. Kisha akawapanga wale watu mia tatu wawe vikosi vitatu, akatia tarumbeta katika mikono ya watu wote, na mitungi isiyo maji, na mienge ndani ya hiyo mitungi. Akawaambia, Nitazameni, mkafanye kama nifanyavyo mimi; angalieni, nitakapofika mwisho wa kambi, itakuwa, nifanyavyo mimi nanyi fanyeni kadhalika. Nitakapopiga tarumbeta, mimi na wote walio pamoja nami, basi ninyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi, mkaseme, Kwa BWANA, na kwa Gideoni. Basi Gideoni, na wale watu mia waliokuwa pamoja naye, wakafika mwisho wa kambi, mwanzo wa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu; wakazipiga hizo tarumbeta, wakaivunja vipande vipande ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. Vile vikosi vitatu wakapiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga; wakapiga kelele, Upanga wa BWANA na wa Gideoni. Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele, wakawakimbiza. Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye BWANA akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuendelea Serera, hata mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi.

Shirikisha
Soma Waamuzi 7

Waamuzi 7:1-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ndipo Yerub-Baali (yaani Gideoni) na lile jeshi lililokuwa pamoja naye, wakaondoka asubuhi na mapema na kupiga kambi kando ya chemchemi ya Harodi. Kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini mwao katika bonde, karibu na kilima cha More. BWANA akamwambia Gideoni, “Jeshi lililo pamoja nawe ni kubwa sana kwangu kuwatia Wamidiani mikononi mwao, Israeli asije akajisifu juu yangu, akisema, ‘Mkono wangu ndio uliniokoa.’ Kwa hiyo sasa tangaza jeshi lote likiwa linasikia, kwamba: ‘Yeyote anayeogopa na kutetemeka, yeye na arudi nyumbani, aondoke katika Mlima Gileadi.’ ” Hivyo, watu elfu ishirini na mbili wakarudi nyumbani, wakabaki elfu kumi. Lakini BWANA akamwambia Gideoni, “Idadi ya jeshi bado ni kubwa. Wapeleke kwenye maji, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako. Nikikuambia, ‘Huyu ataenda pamoja nawe,’ yeye ataenda; lakini nikisema, ‘Huyu hataenda pamoja nawe,’ yeye hataenda.” Gideoni akalipeleka lile jeshi kwenye maji, naye BWANA akamwambia Gideoni, “Watenganishe watakaoramba maji kwa ulimi kama mbwa, na wale watakaopiga magoti ili kunywa.” Waliokunywa kwa kuramba maji kutoka mikononi mwao walikuwa watu mia tatu. Wengine wote walipiga magoti ili kunywa. BWANA akamwambia Gideoni, “Kupitia hao watu mia tatu walioramba maji nitawaokoa ninyi, nami nitawatia Wamidiani mkononi mwako. Waache hao watu wengine wote warudi kila mmoja nyumbani mwake.” Hivyo Gideoni akawaruhusu wale Waisraeli wengine kila mmoja aende kwenye hema lake. Akabakia na wale mia tatu, nao wakachukua vyakula na tarumbeta za wenzao. Basi kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake bondeni. Usiku ule ule BWANA akamwambia Gideoni, “Ondoka, ushuke ushambulie kambi, kwa kuwa nimeitia mkononi mwako. Lakini kama unaogopa kushambulia, shuka kambini pamoja na mtumishi wako Pura, nawe sikiliza wanayosema. Hatimaye, utatiwa moyo kushambulia kambi.” Basi yeye na Pura, mtumishi wake, wakashuka na kuwafikia walinzi wa mbele wa kambi. Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine yote ya mashariki walikaa bondeni, nao walikuwa mfano wa nzige kwa wingi wao. Ngamia wao hawangehesabika, wingi wao ulikuwa kama mchanga wa ufuoni mwa bahari. Gideoni alifika mara tu mtu mmoja alipokuwa akimweleza mwenzake ndoto yake, akisema, “Tazama, niliota ndoto, mkate wa shayiri ulioviringana ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukaipiga hema kwa nguvu, na kusababisha hema hilo kupinduka na kuporomoka.” Rafiki yake akamjibu, “Habari hii si kitu kingine isipokuwa upanga wa Gideoni mwana wa Yoashi, Mwisraeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote mkononi mwake.” Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akasujudu na kuabudu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni! BWANA amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.” Akawagawa wale watu mia tatu katika makundi matatu, akawakabidhi tarumbeta mikononi mwao wote, na mitungi mitupu, na mienge ikawekwa ndani yake. Akawaambia, “Nitazameni, fanyeni kama nitakavyofanya. Nitakapofika mwisho wa kambi, mfanye kama nitakavyofanya. Mimi na wote walio pamoja nami tutakapopiga tarumbeta zetu, ninyi nanyi pigeni tarumbeta pande zote za kambi na mpige kelele, mseme, ‘Upanga wa BWANA na wa Gideoni.’ ” Gideoni na wale watu mia moja waliokuwa pamoja naye wakafika mwisho wa kambi usiku mwanzoni mwa zamu ya kati, mara tu walipokuwa wamebadili zamu. Wakapiga zile tarumbeta zao, na kuvunja ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. Yale makundi matatu wakapiga tarumbeta na kuvunja mitungi. Wakashika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga. Wakapaza sauti zao, wakisema, “Upanga wa BWANA, na wa Gideoni!” Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote, Wamidiani wote wakakimbia, huku wakipiga kelele. Walipozipiga zile tarumbeta mia tatu, BWANA akafanya watu katika kambi yote kugeukiana kila mmoja na mwenziwe kwa upanga. Jeshi likakimbia hadi Beth-Shita kuelekea Serera, hadi mpakani mwa Abel-Mehola karibu na Tabathi.

Shirikisha
Soma Waamuzi 7