Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 6:11-24

Waamuzi 6:11-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Malaika wa Mwenyezi-Mungu akaenda, akaketi chini ya mwaloni wa Yoashi, Mwabiezeri, huko Ofra. Gideoni mwana wa Yoashi, alikuwa anapura ngano ndani ya shinikizo la kusindikia zabibu ili Wamidiani wasimwone. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nawe, ewe shujaa.” Gideoni akamwambia, “Ee Bwana wangu, ikiwa Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu ambayo wazee wetu walitusimulia, wakisema: ‘Mwenyezi-Mungu ndiye aliyetutoa nchini Misri.’ Lakini sasa Mwenyezi-Mungu ametutupa na kututia mikononi mwa Wamidiani!” Mwenyezi-Mungu akamgeukia, akamwambia, “Nenda kwa uwezo ulio nao, ukaikomboe Israeli kutoka Wamidiani. Ni mimi ninayekutuma.” Gideoni akamjibu, “Tafadhali Bwana, nitawezaje kuikomboa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu zaidi katika kabila la Manase, na mimi mwenyewe ni mdogo kabisa katika jamaa yetu!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nitakuwa pamoja nawe; nawe utawaangamiza Wamidiani kana kwamba wangekuwa mtu mmoja.” Gideoni akamwambia, “Basi, ikiwa nimepata fadhili kwako, nioneshe ishara ili nijue kuwa ni wewe kweli uliyezungumza nami. Nakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea zawadi yangu na kuiweka mbele yako.” Naye akamjibu, “Nitakaa hapa mpaka utakaporudi.” Gideoni akaenda nyumbani mwake, akatayarisha mwanambuzi na mikate isiyotiwa chachu kutoka debe la unga; akatia nyama ndani ya kikapu na mchuzi ndani ya chungu, kisha akampelekea chini ya mwaloni, akampa. Malaika wa Mungu akamwambia, “Chukua nyama na mikate isiyotiwa chachu uviweke juu ya mwamba huu. Halafu tia mchuzi juu ya mikate na nyama.” Naye akafanya hivyo. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akanyosha fimbo yake, akagusa nyama na mikate kwa ncha ya fimbo. Ghafla, moto ukatoka mwambani, ukateketeza nyama na mikate. Mara malaika wa Mwenyezi-Mungu akatoweka mbele yake. Ndipo Gideoni akatambua kwamba huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu; akasema, “Ole wangu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu, maana nimemwona malaika wako uso kwa uso.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Amani iwe nawe! Usiogope, hutakufa.” Gideoni akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu huko na kuyaita, “Mwenyezi-Mungu ni Amani.” Madhabahu hiyo iko huko Ofra, mji wa Wabiezeri, mpaka leo.

Shirikisha
Soma Waamuzi 6

Waamuzi 6:11-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Malaika wa BWANA akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwaabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. Malaika wa BWANA akamtokea, akamwambia, BWANA yuko pamoja nawe, Ee shujaa. Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. BWANA akamtazama, akasema, Nenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. BWANA akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja. Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unioneshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami. Tafadhali, usiondoke hapa hadi nikujie, nikatoe zawadi yangu, na kuiweka mbele zako. Akasema, Nitangoja hadi utakaporudi. Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa. Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo. Ndipo malaika wa BWANA akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa BWANA akaondoka mbele ya macho yake. Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa BWANA; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona BWANA uso kwa uso. BWANA akamwambia “Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa”. Ndipo Gideoni akamjengea BWANA madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri.

Shirikisha
Soma Waamuzi 6

Waamuzi 6:11-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Malaika wa BWANA akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. Malaika wa BWANA akamtokea, akamwambia, BWANA yu pamoja nawe, Ee shujaa. Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. BWANA akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. BWANA akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja. Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unionyeshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami. Tafadhali, usiondoke hapa hata nikujie, nikatoe zawadi yangu, na kuiweka mbele zako. Akasema, Nitangoja hata utakaporudi. Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa. Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo. Ndipo malaika wa BWANA akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa BWANA akaondoka mbele ya macho yake. Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa BWANA; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona BWANA uso kwa uso. BWANA akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa. Ndipo Gideoni akamjengea BWANA madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri.

Shirikisha
Soma Waamuzi 6

Waamuzi 6:11-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Malaika wa BWANA akaja akaketi chini ya mwaloni ulio Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi Mwabiezeri, pale Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione. Malaika wa BWANA alipomtokea Gideoni, akamwambia, “BWANA yu pamoja nawe, ewe shujaa mwenye nguvu.” Gideoni akajibu, “Nisamehe, Ee Bwana wangu. Kama BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi yale matendo yake makuu ambayo baba zetu walitusimulia juu yake waliposema, ‘Je, BWANA hakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasa BWANA ametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.” BWANA akamgeukia na kusema “Nenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?” Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.” BWANA akamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.” Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonesha kuwa kweli ni wewe unayesema nami. Tafadhali nakuomba usiondoke hapa hadi nitakaporudi, nilete sadaka yangu na kuiweka mbele yako.” Naye BWANA akamwambia, “Nitangoja hadi utakaporudi.” Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa moja ya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mwaloni, akampa. Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo. Malaika wa BWANA akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa BWANA akatoweka machoni pake. Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa BWANA, akapaza sauti, akasema, “Ole wangu, BWANA Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa BWANA uso kwa uso!” Lakini BWANA akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.” Hivyo Gideoni akamjengea BWANA madhabahu mahali pale na kupaita Yehova-Shalomu. Hata leo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri.

Shirikisha
Soma Waamuzi 6