Waamuzi 6:1-6
Waamuzi 6:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; naye akawatia mikononi mwa Wamidiani kwa muda wa miaka saba. Wamidiani waliwakandamiza sana Waisraeli, mpaka wakajichimbia mashimo na mapango milimani kuwa ngome zao. Kila mara Waisraeli walipopanda mbegu mashambani, Wamidiani, Waamaleki na watu wengine wa huko mashariki walikuja kuwashambulia. Mataifa hayo yaliweka kambi nchini, yakawashambulia na kuharibu mazao yote nchini hadi mpakani mwa Gaza, wasiwaachie Waisraeli chochote, awe kondoo, ng'ombe au punda. Adui waliozoea kuja kwa wingi kama nzige, pamoja na ng'ombe na ngamia wao na kufanya makao yao nchini Israeli, waliharibu nchi ya Israeli kwa vile walikuwa wengi mno wasiohesabika. Waisraeli walidhoofishwa sana na Wamidiani hata wakamlilia Mwenyezi-Mungu awasaidie.
Waamuzi 6:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA; BWANA akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakawavamia; wakapiga kambi juu yao, na kuyaharibu hayo mavuno ya nchi, hadi kufika Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki zozote; kondoo, wala ng'ombe, wala punda. Kwa maana walikwea na ng'ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia BWANA.
Waamuzi 6:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA; BWANA akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakakwea juu yao; wakapanga marago juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo, wala ng’ombe, wala punda. Kwa maana walikwea na ng’ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia BWANA.
Waamuzi 6:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele za BWANA, naye BWANA akawatia mikononi mwa Wamidiani kwa muda wa miaka saba. Kwa kuwa Wamidiani walikuwa na nguvu juu yao, Waisraeli walijitengenezea maficho milimani, kwenye mapango, na katika ngome. Kila wakati Waisraeli walipopanda mazao mashambani, Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki walivamia nchi yao. Wakapiga kambi katika mashamba yao na kuharibu mazao ya nchi yote hadi kufikia Gaza, wala hawakuacha kiumbe chochote kilicho hai kwa Waisraeli, iwe kondoo au ngʼombe au punda. Walipanda na mifugo yao na mahema yao, mfano wa makundi ya nzige. Ilikuwa haiwezekani kuwahesabu watu na ngamia wao; wakavamia nchi ili kuiharibu. Wamidiani wakaifanya Israeli kuwa maskini sana, hata Waisraeli wakamlilia BWANA kumwomba msaada.