Waamuzi 6:1-40
Waamuzi 6:1-40 Biblia Habari Njema (BHN)
Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; naye akawatia mikononi mwa Wamidiani kwa muda wa miaka saba. Wamidiani waliwakandamiza sana Waisraeli, mpaka wakajichimbia mashimo na mapango milimani kuwa ngome zao. Kila mara Waisraeli walipopanda mbegu mashambani, Wamidiani, Waamaleki na watu wengine wa huko mashariki walikuja kuwashambulia. Mataifa hayo yaliweka kambi nchini, yakawashambulia na kuharibu mazao yote nchini hadi mpakani mwa Gaza, wasiwaachie Waisraeli chochote, awe kondoo, ng'ombe au punda. Adui waliozoea kuja kwa wingi kama nzige, pamoja na ng'ombe na ngamia wao na kufanya makao yao nchini Israeli, waliharibu nchi ya Israeli kwa vile walikuwa wengi mno wasiohesabika. Waisraeli walidhoofishwa sana na Wamidiani hata wakamlilia Mwenyezi-Mungu awasaidie. Waisraeli walipomlilia Mwenyezi-Mungu awaondolee taabu walizopata kwa Wamidiani, Mwenyezi-Mungu aliwapelekea nabii, naye akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Niliwatoa nchini Misri ambako mlikuwa watumwa, nikawakomboa mikononi mwa Wamisri wote waliowakandamiza. Nikawafukuza watu mbele yenu na kuwapa nyinyi nchi yao. Kisha nikawakumbusheni kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; na kwamba msiiheshimu miungu ya Waamori, ambao nchi yao mmeichukua, lakini hamkuisikiliza sauti yangu.’” Malaika wa Mwenyezi-Mungu akaenda, akaketi chini ya mwaloni wa Yoashi, Mwabiezeri, huko Ofra. Gideoni mwana wa Yoashi, alikuwa anapura ngano ndani ya shinikizo la kusindikia zabibu ili Wamidiani wasimwone. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nawe, ewe shujaa.” Gideoni akamwambia, “Ee Bwana wangu, ikiwa Mwenyezi-Mungu yuko pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu ambayo wazee wetu walitusimulia, wakisema: ‘Mwenyezi-Mungu ndiye aliyetutoa nchini Misri.’ Lakini sasa Mwenyezi-Mungu ametutupa na kututia mikononi mwa Wamidiani!” Mwenyezi-Mungu akamgeukia, akamwambia, “Nenda kwa uwezo ulio nao, ukaikomboe Israeli kutoka Wamidiani. Ni mimi ninayekutuma.” Gideoni akamjibu, “Tafadhali Bwana, nitawezaje kuikomboa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu zaidi katika kabila la Manase, na mimi mwenyewe ni mdogo kabisa katika jamaa yetu!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nitakuwa pamoja nawe; nawe utawaangamiza Wamidiani kana kwamba wangekuwa mtu mmoja.” Gideoni akamwambia, “Basi, ikiwa nimepata fadhili kwako, nioneshe ishara ili nijue kuwa ni wewe kweli uliyezungumza nami. Nakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea zawadi yangu na kuiweka mbele yako.” Naye akamjibu, “Nitakaa hapa mpaka utakaporudi.” Gideoni akaenda nyumbani mwake, akatayarisha mwanambuzi na mikate isiyotiwa chachu kutoka debe la unga; akatia nyama ndani ya kikapu na mchuzi ndani ya chungu, kisha akampelekea chini ya mwaloni, akampa. Malaika wa Mungu akamwambia, “Chukua nyama na mikate isiyotiwa chachu uviweke juu ya mwamba huu. Halafu tia mchuzi juu ya mikate na nyama.” Naye akafanya hivyo. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akanyosha fimbo yake, akagusa nyama na mikate kwa ncha ya fimbo. Ghafla, moto ukatoka mwambani, ukateketeza nyama na mikate. Mara malaika wa Mwenyezi-Mungu akatoweka mbele yake. Ndipo Gideoni akatambua kwamba huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu; akasema, “Ole wangu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu, maana nimemwona malaika wako uso kwa uso.” Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Amani iwe nawe! Usiogope, hutakufa.” Gideoni akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu huko na kuyaita, “Mwenyezi-Mungu ni Amani.” Madhabahu hiyo iko huko Ofra, mji wa Wabiezeri, mpaka leo. Usiku huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Chukua fahali mmoja wa baba yako, fahali yule wa pili wa umri wa miaka saba. Bomoa madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako na kuvunja sanamu ya Ashera iliyo karibu nayo. Halafu, unijengee mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, madhabahu nzuri juu ya mwinuko huu. Kisha unitolee sadaka ya kuteketezwa ya yule fahali wa pili ukitumia kuni za ile sanamu ya Ashera uliyoivunja.” Basi, Gideoni akachukua watumishi wake kumi, akafanya kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu. Lakini kwa kuwa aliiogopa jamaa yake na watu wa mjini, badala ya kufanya hayo mchana, alifanya wakati wa usiku. Wakazi wa mji walipoamka asubuhi na mapema waliona madhabahu ya Baali na sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo vimeharibiwa. Yule fahali wa pili alikuwa ameteketezwa juu ya madhabahu iliyokuwa imejengwa mahali hapo. Wakaulizana, “Nani amefanya jambo hili?” Walipofanya uchunguzi wakagundua kwamba Gideoni mwana wa Yoashi ndiye aliyekuwa amefanya hayo. Wakazi wa mji wakamjia Yoashi, wakamwambia, “Mtoe mwanao tumuue, maana ameharibu madhabahu ya Baali na kuivunja sanamu ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.” Yoashi akawaambia wale wote waliomkabili, “Je, mnamtetea Baali? Je, mtamwokoa? Yeyote atakayemtetea atauawa kabla ya mapambazuko. Kama Baali ni mungu, basi, na ajitetee mwenyewe maana madhabahu yake imebomolewa.” Siku hiyo wakamwita Gideoni “Yerubaali” maana yake, “Baali na ajitetee mbele yake”, maana aliibomoa madhabahu ya Baali. Wamidiani, Waamaleki na watu wote wanaokaa kando ya mto Yordani wakapiga kambi zao katika bonde la Yezreeli. Lakini roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Gideoni. Gideoni akapiga tarumbeta kuwaita Wabiezeri waje kumfuata. Akatuma wajumbe katika nchi yote ya Manase waje kumfuata. Wajumbe wengine akawatuma kuwaita watu wa makabila ya Asheri, Zebuluni na Naftali, nao wakaja kujiunga naye. Gideoni akamwambia Mungu, “Ikiwa utaikomboa Israeli kwa mkono wangu kama ulivyosema, sasa naweka ngozi ya kondoo kwenye sakafu ya kupuria ngano. Ikiwa kutakuwa na umande juu ya ngozi tu, na sakafu inayoizunguka ikawa kavu, basi, nitajua kuwa utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu kama ulivyosema.” Ikawa hivyo, kwa maana alipoamka asubuhi kesho yake, alikamua umande uliokuwa juu ya ile ngozi, akajaza bakuli. Gideoni akamwambia Mungu, “Tafadhali usinikasirikie. Nakuomba niseme mara moja tena. Nakuomba uniruhusu nitumie ngozi hii kufanya jaribio lingine. Nakuomba juu ya ngozi kuwe kukavu, lakini kwenye sakafu kuwe na umande.” Mungu akafanya hivyo usiku huo, maana, juu ya ngozi kulikuwa kukavu na kwenye sakafu kulikuwa na umande.
Waamuzi 6:1-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA; BWANA akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakawavamia; wakapiga kambi juu yao, na kuyaharibu hayo mavuno ya nchi, hadi kufika Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki zozote; kondoo, wala ng'ombe, wala punda. Kwa maana walikwea na ng'ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia BWANA. Kisha ikawa, hapo wana wa Israeli walipomlilia BWANA kwa sababu ya Midiani, BWANA akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli; naye akawaambia, BWANA, yeye Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa; nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri, na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, nami niliwapa ninyi nchi yao; kisha niliwaambia, Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu; msiiche miungu ya Waamori, ambayo mnakaa katika nchi yao; lakini hamkuitii sauti yangu. Malaika wa BWANA akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwaabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. Malaika wa BWANA akamtokea, akamwambia, BWANA yuko pamoja nawe, Ee shujaa. Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. BWANA akamtazama, akasema, Nenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. BWANA akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja. Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unioneshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami. Tafadhali, usiondoke hapa hadi nikujie, nikatoe zawadi yangu, na kuiweka mbele zako. Akasema, Nitangoja hadi utakaporudi. Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa. Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo. Ndipo malaika wa BWANA akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa BWANA akaondoka mbele ya macho yake. Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa BWANA; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona BWANA uso kwa uso. BWANA akamwambia “Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa”. Ndipo Gideoni akamjengea BWANA madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri. Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; ukamjengee BWANA, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata. Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama BWANA alivyomwambia; lakini kwa kuwa aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku. Hata wakazi wa mji walipoamka asubuhi na mapema, wakaona madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa. Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili. Ndipo wakazi wa mji wakamwambia Yoashi, Mlete mwanao, afe; kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali na kwa sababu ameikata ile Ashera iliyokuwa karibu nayo. Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe kabla ya mapambazuko; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake. Basi Yoashi akamwita Gideoni, Yerubaali siku hiyo, akisema, Baali na atete naye kwa ajili ya nafsi yake, kwa sababu ameibomoa madhabahu yake. Wakati huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli. Lakini Roho ya BWANA ikamjia juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata. Kisha akatuma wajumbe waende kati ya Manase yote; wao nao walikutana pamoja ili kumfuata; kisha akatuma wajumbe waende kwa Asheri, na kwa Zabuloni, na kwa Naftali; nao wakakwea ili kumlaki. Gideoni akamwambia Mungu, Ikiwa wewe utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema, Tazama, nitaweka ngozi ya kondoo katika kiwanja cha kupuria; na kama ukiwapo umande juu ya ngozi tu, na nchi yote ikiwa kavu, basi, hapo ndipo nitakapojua ya kuwa utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema. Ikawa hivyo; kwa maana aliondoka asubuhi na mapema, akaikamua ile ngozi, akautoa ule umande katika ile ngozi, bakuli zima la maji. Gideoni akamwambia Mungu, Hasira yako isiwake juu yangu, nami nitasema mara hii tu; nakuomba, nijaribu kwa ngozi hii mara hii tu; sasa ngozi tu na iwe kavu, na uwe umande juu ya nchi yote. Mungu akafanya hivyo usiku ule; maana ile ngozi tu ilikuwa kavu, napo palikuwa na umande juu ya nchi yote.
Waamuzi 6:1-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA; BWANA akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakakwea juu yao; wakapanga marago juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo, wala ng’ombe, wala punda. Kwa maana walikwea na ng’ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia BWANA. Kisha ikawa, hapo wana wa Israeli walipomlilia BWANA kwa sababu ya Midiani, BWANA akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli; naye akawaambia, BWANA, yeye Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa; nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri, na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, nami niliwapa ninyi nchi yao; kisha niliwaambia, Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu; msiiche miungu ya Waamori, ambayo mwaketi katika nchi yao; lakini hamkuitii sauti yangu. Malaika wa BWANA akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. Malaika wa BWANA akamtokea, akamwambia, BWANA yu pamoja nawe, Ee shujaa. Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. BWANA akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. BWANA akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja. Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unionyeshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami. Tafadhali, usiondoke hapa hata nikujie, nikatoe zawadi yangu, na kuiweka mbele zako. Akasema, Nitangoja hata utakaporudi. Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa. Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo. Ndipo malaika wa BWANA akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa BWANA akaondoka mbele ya macho yake. Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa BWANA; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona BWANA uso kwa uso. BWANA akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa. Ndipo Gideoni akamjengea BWANA madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri. Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Mtwae ng’ombe wa baba yako, yaani ng’ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; ukamjengee BWANA, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng’ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata. Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama BWANA alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku. Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng’ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa. Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili. Ndipo watu wa mji wakamwambia Yoashi Mlete mwanao, afe; kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali na kwa sababu ameikata ile Ashera iliyokuwa karibu nayo. Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake. Basi akamwita Yerubaali siku hiyo, akisema, Baali na atete naye kwa ajili ya nafsi yake, kwa sababu ameibomoa madhabahu yake. Wakati huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli. Lakini roho ya BWANA ikaja juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata. Kisha akatuma wajumbe waende kati ya Manase yote; wao nao walikutana pamoja ili kumfuata; kisha akatuma wajumbe waende kwa Asheri, na kwa Zabuloni, na kwa Naftali; nao wakakwea ili kumlaki. Gideoni akamwambia Mungu, Ikiwa wewe utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema, tazama, nitaweka ngozi ya kondoo katika kiwanja cha kupuria; na kama ukiwapo umande juu ya ngozi tu, na nchi yote ikiwa kavu, basi, hapo ndipo nitakapojua ya kuwa utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema. Ikawa hivyo; kwa maana aliondoka asubuhi na mapema, akaikamua ile ngozi, akautoa ule umande katika ile ngozi, bakuli zima la maji. Gideoni akamwambia Mungu, Hasira yako isiwake juu yangu, nami nitasema mara hii tu; nakuomba, nijaribu kwa ngozi hii mara hii tu; sasa ngozi tu na iwe kavu, na uwe umande juu ya nchi yote. Mungu akafanya hivyo usiku ule; maana ile ngozi tu ilikuwa kavu, napo palikuwa na umande juu ya nchi yote.
Waamuzi 6:1-40 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele za BWANA, naye BWANA akawatia mikononi mwa Wamidiani kwa muda wa miaka saba. Kwa kuwa Wamidiani walikuwa na nguvu juu yao, Waisraeli walijitengenezea maficho milimani, kwenye mapango, na katika ngome. Kila wakati Waisraeli walipopanda mazao mashambani, Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki walivamia nchi yao. Wakapiga kambi katika mashamba yao na kuharibu mazao ya nchi yote hadi kufikia Gaza, wala hawakuacha kiumbe chochote kilicho hai kwa Waisraeli, iwe kondoo au ngʼombe au punda. Walipanda na mifugo yao na mahema yao, mfano wa makundi ya nzige. Ilikuwa haiwezekani kuwahesabu watu na ngamia wao; wakavamia nchi ili kuiharibu. Wamidiani wakaifanya Israeli kuwa maskini sana, hata Waisraeli wakamlilia BWANA kumwomba msaada. Waisraeli walipomlilia BWANA kwa sababu ya Wamidiani, BWANA akawapelekea nabii, ambaye aliwaambia, “Hili ndilo BWANA, Mungu wa Israeli, asemalo: Niliwapandisha mtoke Misri, toka nchi ya utumwa. Nikawaokoa kutoka mikononi mwa Wamisri na kutoka mikononi mwa watesi wenu wote. Nikawafukuza watoke mbele yenu, nami nikawapa ninyi nchi yao. Nikawaambia, ‘Mimi ndimi BWANA Mungu wenu; msiiabudu miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao!’ Lakini ninyi hamkuitii sauti yangu.” Malaika wa BWANA akaja akaketi chini ya mwaloni ulio Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi Mwabiezeri, pale Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione. Malaika wa BWANA alipomtokea Gideoni, akamwambia, “BWANA yu pamoja nawe, ewe shujaa mwenye nguvu.” Gideoni akajibu, “Nisamehe, Ee Bwana wangu. Kama BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi yale matendo yake makuu ambayo baba zetu walitusimulia juu yake waliposema, ‘Je, BWANA hakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasa BWANA ametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.” BWANA akamgeukia na kusema “Nenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?” Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.” BWANA akamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.” Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonesha kuwa kweli ni wewe unayesema nami. Tafadhali nakuomba usiondoke hapa hadi nitakaporudi, nilete sadaka yangu na kuiweka mbele yako.” Naye BWANA akamwambia, “Nitangoja hadi utakaporudi.” Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa moja ya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mwaloni, akampa. Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo. Malaika wa BWANA akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa BWANA akatoweka machoni pake. Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa BWANA, akapaza sauti, akasema, “Ole wangu, BWANA Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa BWANA uso kwa uso!” Lakini BWANA akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.” Hivyo Gideoni akamjengea BWANA madhabahu mahali pale na kupaita Yehova-Shalomu. Hata leo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri. Usiku ule ule BWANA akamwambia, “Mchukue ngʼombe dume wa baba yako, yule wa pili mwenye miaka saba, ubomoe madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako, na ukaikate nguzo ya Ashera iliyo karibu nayo. Kisha mjengee BWANA Mungu wako madhabahu kwa taratibu zake juu ya mwamba katika ngome hii. Kwa kutumia kuni za hiyo nguzo ya Ashera uliyoikatakata, mtoe sadaka huyo dume wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa.” Basi Gideoni akawachukua watumishi wake kumi na kufanya kama BWANA alivyomwambia. Lakini kwa kuwa aliwaogopa jamaa yake na watu wa mji, akafanya haya usiku badala ya mchana. Watu wa mji walipoamka asubuhi, tazama madhabahu ya Baali imebomolewa, na nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwakatwa, na yule ngʼombe wa pili ametolewa sadaka juu ya madhabahu iliyojengwa upya! Wakaulizana, “Ni nani aliyetenda mambo haya?” Walipochunguza kwa makini, wakaambiwa, “Ni Gideoni mwana wa Yoashi, ndiye alitenda hivi.” Watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mlete mwanao hapa. Ni lazima afe, kwa sababu amebomoa madhabahu ya Baali na kukatakata nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.” Lakini Yoashi akaambia umati wa watu waliomzunguka wakiwa kinyume naye, “Je, ninyi mtamtetea Baali? Mnajaribu kumwokoa? Yeyote mwenye kumpigania atauawa kufikia kesho asubuhi! Kama Baali ni mungu kweli, anaweza kujitetea mwenyewe wakati mtu anapobomoa madhabahu yake.” Basi siku ile wakamwita Gideoni “Yerub-Baali,” yaani “Baali na ashindane naye,” kwa sababu alibomoa madhabahu yake. Basi Wamidiani wote, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki wakaunganisha majeshi yao, wakavuka ngʼambo ya Yordani na kupiga kambi katika Bonde la Yezreeli. Ndipo Roho wa BWANA akamjia Gideoni, naye Gideoni akapiga tarumbeta kuwaita Waabiezeri ili wamfuate. Akatuma wajumbe waende katika Manase yote, akiwataka wachukue silaha na pia katika Asheri, Zabuloni na Naftali, nao wakakwea ili kukutana nao. Gideoni akamwambia Mungu, “Kama utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu, kama ulivyoahidi: tazama, nitaweka manyoya ya kondoo kwenye sakafu ya kupuria nafaka, na kama utakuwepo umande juu ya manyoya tu, na ardhi yote ikiwa kavu, ndipo nitakapojua kuwa utaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.” Hivyo ndivyo ilivyotokea. Gideoni akaamka asubuhi na mapema kesho yake, akayakamua yale manyoya yenye umande, yakatoka maji kiasi cha kujaa bakuli. Kisha Gideoni akamwambia BWANA, “Usinikasirikie. Ninaomba nifanye ombi moja lingine. Niruhusu nifanye jaribio jingine moja kwa manyoya haya. Wakati huu uyafanye manyoya kuwa kavu, na ardhi yote ifunikwe na umande.” Usiku ule Mungu akafanya hivyo. Manyoya yakawa kavu, na ardhi yote ikafunikwa na umande.