Waamuzi 20:1-48
Waamuzi 20:1-48 Biblia Habari Njema (BHN)
Watu wote wa Israeli, kutoka Dani hadi Beer-sheba, pamoja na watu wa nchi ya Gileadi, jumuiya nzima, walikusanyika huko Mizpa, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Viongozi wote wa makabila ya Israeli wakajitokeza mbele ya mkusanyiko wa watu wa Mungu. Wote, jumla walikuwa askari wa miguu wenye silaha 400,000. Nao watu wa kabila la Benyamini, wakapata habari kwamba watu wale wengine wa Israeli walikuwa wamekusanyika huko Mizpa. Basi Waisraeli wakamwuliza yule mwanamume Mlawi “Tueleze, uovu huo ulifanyikaje?” Yule Mlawi, mume wa yule suria, akawajibu, “Mimi na suria wangu tulifika mjini Gibea, mji wa kabila la Benyamini ili tulale huko usiku. Lakini watu wa mji wa Gibea wakaja usiku wakaizingira nyumba nilimokuwa nimelala. Walitaka kuniua, wakambaka suria wangu mpaka akafa. Mimi nikachukua maiti yake, nikamkatakata vipandevipande na kuvipeleka kwa makabila yote ya Israeli, maana wamefanya jambo la kuchukiza na potovu katika Israeli. Sasa enyi Waisraeli, shaurianeni na toeni uamuzi wenu.” Watu wote kwa pamoja, wakasimama na kusema, “Hakuna yeyote kati yetu atakayerudi hemani kwake au nyumbani kwake. Hivi ndivyo tutakavyofanya kuhusu Gibea: Tutapiga kura namna ya kuwashambulia. Tutachagua watu kumi katika kila watu mia moja wa Israeli, watu mia moja katika kila watu elfu moja, watu elfu moja katika kila watu elfu kumi. Hao watakuwa na jukumu la kuwaletea chakula wenzao watakaokuwa na kazi ya kuuadhibu mji wa Gibea katika nchi ya Benyamini kwa uhalifu wao na upotovu walioufanya katika Israeli.” Hivyo wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa moyo mmoja dhidi ya mji wa Gibea. Watu wa makabila ya Israeli wakatuma wajumbe mpaka kila sehemu ya kabila la Benyamini, wakisema, “Je, ni uovu gani huu uliotukia miongoni mwenu? Sasa tupeni hao watu mabaradhuli wa Gibea ili tuwaue na kutokomeza uovu huu kutoka Israeli.” Lakini watu wa kabila la Benyamini hawakuwasikiliza ndugu zao, Waisraeli. Basi walikusanyika huko Gibea kutoka katika kila mji wao, ili kupigana na Waisraeli. Watu wa kabila la Benyamini walikusanya kutoka miji yao jeshi la watu 26,000 wenye kutumia silaha, nao wakazi wa mji wa Gibea wakakusanya watu 700 waliochaguliwa. Kati ya watu hao waliochaguliwa kulikuwa na watu 700 waliotumia mkono wa kushoto; kila mmoja aliweza kurusha jiwe kwa kombeo na kulenga unywele bila kukosea. Waisraeli, licha ya wa kabila la Benyamini, walikusanya watu 400,000 wawezao kutumia silaha. Wote walikuwa hodari wa vita. Waisraeli wakaenda Betheli kutaka shauri kwa Mungu, wapate kujua kabila ambalo litakwenda kwanza kupigana na watu wa kabila la Benyamini. Mwenyezi-Mungu alitaja kabila la Yuda liende kwanza. Basi, Waisraeli wakaenda asubuhi, wakapiga kambi yao karibu na mji wa Gibea. Waisraeli wakatoka kupigana na watu wa kabila la Benyamini karibu na Gibea. Watu wa kabila la Benyamini wakatoka nje ya mji wa Gibea wakapigana na Waisraeli, wakawaangusha chini siku hiyo, watu wa Israeli 22,000. Lakini Waisraeli wakajipa moyo, wakajipanga tena kwa vita mahali pale walipojipanga kwa mara ya kwanza. Basi Waisraeli wakaenda juu, wakamlilia Mwenyezi-Mungu mpaka jioni. Kisha wakaomba shauri kwa Mwenyezi-Mungu: “Je, twende tena kupigana na ndugu zetu, wa kabila la Benyamini?” Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Nendeni mkapigane nao.” Hivyo siku ya pili Waisraeli wakakaribia kupigana na watu wa kabila la Benyamini. Siku hiyo ya pili watu wa kabila la Benyamini walitoka Gibea na kuwashambulia Waisraeli, wakawaangusha chini Waisraeli 18,000. Watu wote wa jeshi la Waisraeli wakaenda Betheli. Walikaa huko mbele ya Mwenyezi-Mungu wakiomboleza na kufunga mpaka jioni. Wakamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Waisraeli wakamwomba Mwenyezi-Mungu awape shauri. Wakati huo sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilikuwa huko Betheli. Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Aroni alikuwa na wajibu wa kuhudumu mbele yake. Waisraeli wakamwuliza Mwenyezi-Mungu, “Je, twende tena kupigana na ndugu zetu, watu wa kabila la Benyamini?” Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Nendeni. Kesho nitawatia mikononi mwenu.” Hivyo, Waisraeli wakaweka watu mafichoni kuuzunguka mji wa Gibea. Waisraeli wakaenda kupigana na watu wa kabila la Benyamini katika siku ya tatu. Wakajipanga dhidi ya mji wa Gibea kama walivyofanya nyakati za hapo awali. Kisha watu wa kabila la Benyamini walipotoka mjini kuanza kupigana na Waisraeli, walivutwa kutoka nje ya mji. Ilitokea tena kama walivyofanya nyakati za hapo awali wakawaua baadhi ya watu wa Israeli kwenye njia kuu zielekeazo miji ya Betheli na Gibea, mpaka mbugani. Waliua Waisraeli wapatao thelathini. Watu wa Benyamini wakafikiri, “Tumewapiga kama nyakati zilizopita.” Lakini Waisraeli wakasema, “Sisi tukimbie ili tuwavute mbali na mji hadi kwenye njia kuu.” Hivyo watu wote wa Israeli wakatoka kwenye sehemu yao na kujipanga tena huko Baal-tamari. Wenzao waliokuwa wanaotea wakatoka haraka mahali pao upande wa magharibi wa mji wa Gibea. Askari hodari waliochaguliwa kutoka makabila yote ya Israeli wakawasili hapo mbele ya mji wa Gibea. Vita vya siku hiyo vilikuwa vikali. Lakini watu wa Benyamini hawakufahamu kwamba kuangamia kwao kulikuwa karibu. Mwenyezi-Mungu aliwashinda watu wa Benyamini mbele ya Waisraeli. Waisraeli wakawaua watu wa Benyamini 25,100. Hao wote waliouawa walikuwa askari walioweza kutumia silaha. Hivyo watu wa kabila la Benyamini wakaona kwamba wameshindwa. Waisraeli walirudi nyuma kana kwamba wanawakimbia watu wa kabila la Benyamini, kwani walitegemea wenzao waliokuwa wamewekwa kuotea mji wa Gibea. Wale waliowekwa kuuotea mji walitoka haraka na kuushambulia mji wa Gibea na kuwaua wote waliokuwamo kwa upanga. Walikuwa wamekubaliana na wale watu wengine wa Israeli juu ya ishara moja. Walikubaliana kwamba wale waliokuwa wanaotea watakapoona moshi mkubwa unapanda juu kutoka mjini, basi, waushambulie mji. Wakati huo, watu wa kabila la Benyamini walikuwa tayari wameua watu wapatao thelathini wa Israeli na kuambiana, “Tumewapiga kama hapo awali.” Lakini ile ishara ya mnara wa moshi ilipoanza kutokea katika mji, watu wa kabila la Benyamini walipotazama nyuma yao, wakashangaa kuona kwamba mji wao ulikuwa unateketezwa moto. Ndipo Waisraeli wakageuka, na watu wa kabila la Benyamini wakakumbwa na fadhaa kwani sasa waliona kuwa kuangamia kwao kulikuwa kumekaribia. Kwa hiyo wakageuka, wakawakimbia Waisraeli kuelekea jangwani, lakini vita vikawakumba; wakajikuta wako katikati ya majeshi mawili ya Israeli, na askari waliotoka wakawaangamiza. Waisraeli waliwazingira watu wa kabila la Benyamini, wakawafuatia kutoka Noha hadi mashariki ya mji wa Gibea wakiwaua wengi wao. Siku hiyo watu 18,000 wa kabila la Benyamini, wote askari hodari, waliuawa. Watu wengine wa kabila la Benyamini waligeuka, wakakimbia kuelekea jangwani hadi mwamba wa Rimoni. Wengine 5,000 waliuawa kwenye njia kuu walipokuwa wanakimbia. Waisraeli waliendelea kuwafuatia vikali watu wa kabila la Benyamini hadi mji wa Gidomu wakawaua watu 2,000. Jumla ya watu wote wa kabila la Benyamini waliouawa siku hiyo ilikuwa 25,000, askari hodari wa kutumia silaha. Lakini wanaume 600 wa kabila la Benyamini walifaulu kukimbilia jangwani hadi kwenye mwamba wa Rimoni, wakakaa huko kwa muda wa miezi minne. Waisraeli wakawageukia watu wengine wa kabila la Benyamini, wakawaua wote: Wanaume, wanawake, watoto na wanyama. Na miji yote waliyoikuta huko wakaiteketeza moto.
Waamuzi 20:1-48 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo wana wa Israeli walipotoka; na mkutano ukakutanika kama mtu mmoja, kutoka Dani hadi Beer-sheba, pamoja na nchi ya Gileadi wakamkutanikia BWANA huko Mispa. Wakuu wote wa makabila yote ya Israeli, wakahudhuria huo mkutano wa watu wa Mungu, wanaume elfu mia nne waendao kwa miguu, walio na silaha. Basi wana wa Benyamini walipata habari ya kuwa wana wa Israeli wamekwea kwenda Mispa. Wana wa Israeli wakasema, Tuambieni huo uovu ulitendekaje? Huyo Mlawi, huyo mume wa mwanamke aliyeuawa, akajibu na kusema, Mimi nilifika Gibea ulio wa Benyamini mimi na suria yangu, ili tulale. Nao wanaume wa Gibea wakaniondokea, na kuizingira hiyo nyumba pande zote juu yangu wakati wa usiku; walitaka kuniua, na suria wangu wakambaka nguvu, hata amekufa. Basi nikamtwaa huyo suria wangu, na kumkata vipande, na kumpeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli; kwa sababu wametenda maovu makuu na upumbavu katika Israeli. Angalieni, ninyi wana wa Israeli nyote, sasa toeni maneno na mashauri yenu. Basi watu hao wote waliinuka sawia, wakisema, Hatutakwenda, hata mmoja, hemani kwake, wala hatutaondoka, hata mmoja, kwenda nyumbani kwake. Lakini jambo tutakalowatenda watu wa Gibea ni hili; tutakwea kuushambulia kwa kupiga kura; nasi tutatwaa watu kumi katika mia moja katika kabila zote za Israeli, na watu mia moja katika elfu, na watu elfu katika elfu kumi, ili waende kuwatwalia watu vyakula, ili hapo watakapofika Gibea ya Benyamini wapate kutenda mfano wa upumbavu huo wote walioutenda wao katika Israeli. Basi wanaume wote wa Israeli walikutana pamoja juu ya mji huo, walikuwa wanashikamana pamoja kama mtu mmoja. Kisha makabila ya Israeli wakatuma watu waende katika kabila yote ya Benyamini, wakasema, Je! Ni uovu gani huu uliokuwa kati yenu? Basi sasa watoeni watu hao, hao mabaradhuli walio katika Gibea, ili tuwaue, na kuuondoa uovu katika Israeli. Lakini Benyamini hawakukubali kuisikia sauti ya ndugu zao wana wa Israeli. Lakini wana wa Benyamini wakakutanika huko Gibea kutoka katika miji yao, ili watoke kwenda kupigana na wana wa Israeli. Hao wana wa Benyamini walihesabiwa siku ile kutoka hiyo miji, wanaume elfu ishirini na sita waliokuwa na silaha, mbali na hao waliokaa Gibea, ambao walihesabiwa watu wateule mia saba. Katika watu hao wote walikuwako wanaume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa kombeo, wala asikose. Nao watu wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, walihesabiwa kuwa ni wanaume elfu mia nne, wenye silaha; hao wote walikuwa ni watu wa vita. Basi wana wa Israeli wakainuka, wakakwea kwenda Betheli, nao wakataka shauri kwa Mungu; wakasema, Ni nani atakayekwea kwenda vitani kwanza kwa ajili yetu juu ya wana wa Benyamini? BWANA akawaambia, Yuda atakwea kwanza. Basi wana wa Israeli waliondoka asubuhi, wakapanga hema zao ili kuvamia Gibea. Watu wa Israeli waliondoka ili wapigane na Benyamini; nao watu wa Israeli wakaviandaa vita juu yao huko Gibea. Wana wa Benyamini wakatoka Gibea, wakawaua watu elfu ishirini na mbili katika Israeli siku hiyo. Lakini watu hao, watu wa Israeli, walijitia nguvu, wakaviandaa vile vita mara ya pili mahali pale walipojiandaa siku ya kwanza. Wana wa Israeli wakakwea juu na kulia mbele za BWANA hadi jioni; wakamwuliza BWANA, wakisema, Je! Niende nikaribie tena kupiga vita juu ya wana wa Benyamini ndugu yangu? BWANA akasema, Haya, kweeni, mwende kupigana naye. Basi wana wa Israeli wakakaribia juu ya wana wa Benyamini siku ya pili. Benyamini alitoka kupigana nao kutoka Gibea siku ya pili, wakawaua watu elfu kumi na nane tena katika watu wa Israeli; hao wote walikuwa wamejihami. Ndipo wana wa Israeli wote, na hao watu wote, wakakwea, wakaenda Betheli, na kulia, wakaketi hapo mbele za BWANA, wakafunga siku hiyo hadi jioni; nao wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za BWANA. Kisha wana wa Israeli wakauliza kwa BWANA (kwa sababu sanduku la Agano la Mungu lilikuwako huko siku hizo, na Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anasimama mbele ya hilo sanduku siku hizo), wakasema, Je! Nitoke tena niende kupigana na wana wa Benyamini ndugu yangu, au niache? BWANA akawaambia, Haya, kweeni; kwa kuwa kesho nitamtoa na kumtia mkononi mwako. Basi Israeli akaweka watu wavizie kinyume cha Gibea kuuzunguka pande zote. Basi wana wa Israeli wakakwea kwenda kupigana na wana wa Benyamini siku ya tatu, wakajipanga ili kupigana na Gibea, kama walivyofanya hapo awali. Nao wana wa Benyamini wakatoka waende kupigana nao, wakavutwa waende mbali na huo mji; kisha wakaanza kuwapiga na kuwaua Waisraeli wapatao thelathini, kama walivyofanya hapo awali, kwa kuwaua katika hizo njia kuu, zielekeazo Betheli, na Gibea, na katika nchi tambarare. Wana wa Benyamini wakasema, Wamepigwa mbele yetu kama wali. Lakini wana wa Israeli wakasema, Haya, na tukimbie, na kuwavuta wauache mji waende katika njia kuu. Basi hao watu wote wa Israeli wakaondoka mahali pao wakajipanga huko Baal-tamari; na hao wenye kuvizia wa Israeli wakatoka mahali hapo walipokuwa, hata Maare-geba. Kisha watu elfu kumi waliochaguliwa katika Israeli wote wakavamia Gibea, na vile vita vilikuwa vikali sana; lakini Benyamini hawakujua ya kuwa maafa yalikuwa karibu nao. BWANA akampiga Benyamini mbele ya Israeli; na wana wa Israeli waliangamiza wanaume elfu ishirini na tano na mia moja, wa Benyamini siku hiyo; wote hao waliokuwa wenye kutumia upanga. Basi wana wa Benyamini waliona kuwa wamepigwa; kwa kuwa watu wa Israeli wakaondoka mbele ya Benyamini, kwa sababu walikuwa wanawatumaini hao wenye kuvizia waliokuwa wamewaweka kinyume cha Gibea. Hao wenye kuvizia wakafanya haraka, wakaurukia Gibea; na kuushambulia mji wote kwa makali ya upanga. Basi hiyo ishara iliyoaganwa kati ya watu wa Israeli na hao wenye kuvizia ilikuwa ni hii, kwamba wafanye lipande wingu kubwa la moshi kutoka katika huo mji. Nao watu wa Israeli walipogeuka katika ile vita, Benyamini naye akaanza kupiga na kuwaua watu wa Israeli kama watu thelathini; kwani walisema, Hakika yetu wamepigwa mbele yetu, vile vile kama katika ile vita ya kwanza. Lakini hapo hilo wingu lilipoanza kupanda kutoka katika mji, kama nguzo ya moshi, ndipo Wabenyamini wakaangalia nyuma, na tazama, moshi ulikuwa umetanda mji mzima kwenda mbinguni. Ndipo watu wa Israeli wakageuka, na watu wa Benyamini walishtushwa; kwa kuwa waliona ya kwamba wamefikiwa na maafa. Kwa hiyo wakageuza maungo yao mbele ya wana wa Israeli kuelekea njia ya kwenda nyikani; lakini ile vita ikawaandamia kwa kasi; na hao waliotoka katika ile miji wakawaangamiza katikati yake. Waliwazingira Wabenyamini pande zote na kuwafukuza, na kuwakanyagakanyaga hapo walipopumzika, hadi upande wa mashariki mwa Gibea. Wakauawa Wabenyamini elfu kumi na nane, hao wote walikuwa ni wapiganaji hodari. Kisha wakageuka na kukimbilia upande wa nyika hadi katika jabali la Rimoni; nao wakaokota katika watu hao katika njia kuu wanaume elfu tano; wakawaandamia kwa kasi mpaka Gidomu, nako wakawaua wengine wao watu elfu mbili. Basi jumla ya watu wa Benyamini waliouawa siku ile walikuwa ni watu elfu ishirini na tano waliokuwa wapiganaji vita; wote hao walikuwa ni mashujaa. Lakini wanaume mia sita wakageuka, wakakimbilia upande wa nyikani hadi katika jabali la Rimoni, wakakaa kwenye hilo jabali la Rimoni muda wa miezi minne. Kisha watu wa Israeli wakageuka tena kuwaendea wana wa Benyamini, wakawapiga kwa makali ya upanga, huo mji mzima, na hao wanyama wa mji, na kila kitu walichokiona; tena miji yote waliyoiona wakaiteketeza kwa moto.
Waamuzi 20:1-48 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo wana wa Israeli walipotoka; na mkutano ukakutanika kama mtu mmoja, kutoka Dani hata Beer-sheba, pamoja na nchi ya Gileadi wakamkutanikia BWANA huko Mispa. Hao wakuu wa watu, maana wakuu wa kabila zote za Israeli, wakajihudhurisha katika huo mkutano wa watu wa Mungu, watu waume mia nne elfu waendao kwa miguu, wenye kutumia upanga. Basi wana wa Benyamini walipata habari ya kuwa wana wa Israeli wamekwea kwenda Mispa. Wana wa Israeli wakasema, Tuambieni huo uovu ulikuwaje kutendeka? Huyo Mlawi, huyo mume wa mwanamke aliyeuawa, akajibu na kusema, Mimi nilifikilia Gibea ulio wa Benyamini mimi na suria yangu, ili tulale. Nao watu waume wa Gibea wakaniondokea, na kuizingira hiyo nyumba pande zote juu yangu wakati wa usiku; walidhani kuniua, na suria wangu wakamtenza nguvu, hata amekufa. Basi nikamtwaa huyo suria yangu, na kumkata vipande, na kumpeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli; kwa sababu wametenda maovu makuu na upumbavu katika Israeli. Angalieni, ninyi wana wa Israeli nyote, sasa toeni maneno na mashauri yenu. Basi watu hao wote waliinuka kama mtu mmoja, wakisema, Hatutakwenda, hata mmoja, hemani kwake, wala hatutaondoka, hata mmoja, kwenda nyumbani kwake. Lakini jambo tutakalowatenda watu wa Gibea ni hili; tutakwea kwa kura kwenda kuupiga; nasi tutatwaa watu kumi katika mia katika kabila zote za Israeli, na watu mia katika elfu, na watu elfu katika elfu kumi, ili waende kuwatwalia watu vyakula, ili kwamba, hapo watakapofika Gibea ya Benyamini wapate kutenda mfano wa upumbavu huo wote walioutenda wao katika Israeli. Basi waume wote wa Israeli walikutana pamoja juu ya mji huo, walikuwa wanashikamana pamoja kama mtu mmoja. Kisha kabila za Israeli wakatuma watu waende katika kabila yote ya Benyamini, wakasema, Je! Ni uovu gani huu uliokuwa kati yenu? Basi sasa watoeni watu hao, hao mabaradhuli walio katika Gibea, ili kwamba tupate kuwaua, na kuuondoa uovu katika Israeli. Lakini Benyamini hawakukubali kuisikia sauti ya ndugu zao wana wa Israeli. Lakini wana wa Benyamini wakakutanika huko Gibea kutoka katika miji yao, ili watoke kwenda kupiga vita juu ya wana wa Israeli. Hao wana wa Benyamini walihesabiwa siku ile kutoka hiyo miji, watu waume ishirini na sita elfu waliotumia upanga, zaidi ya hao waliokaa Gibea, ambao walihesabiwa watu wateule mia saba. Katika watu hao wote walikuwako watu waume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa teo, wala asikose. Nao watu wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, walihesabiwa kuwa ni watu waume mia nne elfu, wenye kutumia upanga; hao wote walikuwa ni watu wa vita. Basi wana wa Israeli wakainuka, wakakwea kwenda Betheli, nao wakataka shauri kwa Mungu; wakasema, Ni nani atakayekwea kwenda vitani kwanza kwa ajili yetu juu ya wana wa Benyamini? BWANA akawaambia, Yuda atakwea kwanza. Basi wana wa Israeli waliondoka asubuhi, wakapanga hema zao juu ya Gibea. Watu wa Israeli walitoka ili wapigane na Benyamini; nao watu wa Israeli wakaviandaa vita juu yao huko Gibea. Wana wa Benyamini wakatoka Gibea, wakaangamiza hata nchi watu ishirini na mbili elfu katika Israeli siku hiyo. Lakini watu hao, watu wa Israeli, walijitia nguvu, wakaviandaa vile vita mara ya pili mahali pale walipojiandaa siku ya kwanza. Wana wa Israeli wakakwea juu na kulia mbele za BWANA hata jioni; wakamwuliza BWANA, wakisema, Je! Niende nikaribie tena kupiga vita juu ya wana wa Benyamini ndugu yangu? BWANA akasema, Haya, kweeni, mwende kupigana naye. Basi wana wa Israeli wakakaribia juu ya wana wa Benyamini siku ya pili. Benyamini alitoka kupigana nao kutoka Gibea siku ya pili, wakaangamiza hata nchi watu kumi na nane elfu tena katika watu wa Israeli; hao wote walikuwa wenye kutumia upanga. Ndipo wana Israeli wote, na hao watu wote, wakakwea, wakaenda Betheli, na kulia, wakaketi hapo mbele za BWANA, wakafunga siku hiyo hata jioni; nao wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za BWANA. Kisha wana wa Israeli wakauliza kwa BWANA (kwa sababu sanduku la agano la Mungu lilikuwako huko siku hizo, na Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anasimama mbele ya hilo sanduku siku hizo), wakasema, Je! Nitoke tena niende kupigana na wana wa Benyamini ndugu yangu, au niache? BWANA akawaambia, Haya, kweeni; kwa kuwa kesho nitamtoa na kumtia mkononi mwako. Basi Israeli akaweka watu wavizie kinyume cha Gibea kuuzunguka pande zote. Basi wana wa Israeli wakakwea kwenda kupigana na wana wa Benyamini siku ya tatu, wakajipanga ili kupigana na Gibea, kama walivyofanya nyakati nyingine. Nao wana wa Benyamini wakatoka waende kupigana nao, wakavutwa waende mbali na huo mji; kisha wakaanza kupiga na kuua katika hao watu, wapata kama watu thelathini wa Israeli, kama walivyofanya nyakati nyingine, katika hizo njia kuu, ambazo njia mojawapo huendelea Betheli, na njia ya pili huendelea Gibea, katika shamba. Wana wa Benyamini wakasema, Wamepigwa mbele yetu kama kwanza. Lakini wana wa Israeli wakasema, Haya, na tukimbie, na kuwavuta wauache mji waende katika njia kuu. Basi hao watu wote wa Israeli wakaondoka mahali pao wakajipanga huko Baal-tamari; na hao wenye kuvizia wa Israeli wakatoka mahali hapo walipokuwa, hata Maare-geba. Kisha watu elfu kumi waliochaguliwa katika Israeli wote wakaja juu ya Gibea, na vile vita vilikuwa vikali sana; lakini hawakujua ya kuwa uovu ulikuwa karibu nao. BWANA akampiga Benyamini mbele ya Israeli; na wana wa Israeli waliangamiza watu waume ishirini na tano elfu na mia moja, wa Benyamini siku hiyo; wote hao waliokuwa wenye kutumia upanga. Basi wana wa Benyamini waliona kuwa wamepigwa; kwa kuwa watu wa Israeli wakaondoka mbele ya Benyamini, kwa sababu walikuwa wanawatumaini hao wenye kuvizia waliokuwa wamewaweka kinyume cha Gibea. Hao wenye kuvizia wakafanya haraka, wakaurukia Gibea; na hao wenye kuvizia wakaenda wakaupiga huo mji wote kwa makali ya upanga. Basi hiyo ishara iliyoaganwa kati ya watu wa Israeli na hao wenye kuvizia ilikuwa ni hii, kwamba wafanye lipande wingu kubwa la moshi kutoka katika huo mji. Nao watu wa Israeli walipogeuka katika vile vita, Benyamini naye akaanza kupiga na kuwaua watu wa Israeli kama watu thelathini; kwani walisema, Hakika yetu wamepigwa mbele yetu, vile vile kama katika vile vita vya kwanza. Lakini hapo hilo wingu lilipoanza kupanda kutoka katika mji, kama nguzo ya moshi, ndipo Wabenyamini wakaangalia nyuma, na tazama, huo mji mzima ulikuwa wapaa juu katika moshi kwenda mbinguni. Ndipo watu wa Israeli wakageuka, na watu wa Benyamini walisitushwa; kwa kuwa waliona ya kwamba wamefikiliwa na uovu. Kwa hiyo wakageuza maungo yao mbele ya wana wa Israeli kuelekea njia ya kwenda nyikani; lakini vile vita vikawaandamia kwa kasi; na hao waliotoka katika ile miji wakawaangamiza katikati yake. Waliwazingira Wabenyamini pande zote na kuwafukuza, na kuwakanyaga-kanyaga hapo walipopumzika, hata kufikilia Gibea upande wa maawio ya jua. Wakaanguka watu wa Benyamini watu kumi na nane elfu, hao wote walikuwa ni watu waume mashujaa. Kisha wakageuka na kukimbia upande wa nyika hata kulifikilia jabali la Rimoni; nao wakaokota katika watu hao katika njia kuu watu waume elfu tano; wakawaandamia kwa kasi mpaka Gidomu, nako wakawapiga wengine wao watu elfu mbili. Basi jumla ya watu wa Benyamini walioanguka siku ile walikuwa ni watu ishirini na tano elfu waliokuwa wanatumia upanga; wote hao walikuwa ni watu mashujaa. Lakini watu waume mia sita wakageuka, wakakimbia upande wa nyikani mpaka jabali la Rimoni, wakakaa kwenye hilo jabali la Rimoni muda wa miezi minne. Kisha watu wa Israeli wakageuka tena kuwaendea wana wa Benyamini, wakawapiga kwa makali ya upanga, huo mji mzima, na hao wanyama wa mji, na kila kitu walichokiona; tena miji yote waliyoiona wakaitia moto.
Waamuzi 20:1-48 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Waisraeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na wa kutoka nchi ya Gileadi wakatoka kama mtu mmoja, wakakusanyika mbele za BWANA huko Mispa. Viongozi wote wa makabila ya Israeli wakakaa kwenye nafasi zao katika kusanyiko la watu wa Mungu, ambao walikuwa askari elfu mia nne walioenda kwa miguu wenye panga. (Wabenyamini wakasikia kuwa Waisraeli wamepanda kwenda Mispa.) Ndipo Waisraeli wakasema, “Tuelezeni jinsi jambo hili ovu lilivyotendeka.” Hivyo yule Mlawi, mume wa yule mwanamke aliyeuawa, akasema, “Mimi na suria wangu tulifika Gibea ya Benyamini ili tulale huko. Wakati wa usiku wanaume wa Gibea wakanijia na kuizingira nyumba, wakitaka kuniua. Wakambaka suria wangu hata akafa. Ndipo nikamchukua suria wangu, nikamkatakata vipande vipande na kuvipeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli, kwa kuwa wametenda uasherati mkubwa na jambo la aibu katika Israeli. Sasa, ninyi Waisraeli wote, semeni na mtoe uamuzi wenu.” Watu wote wakainuka wakasema, kama mtu mmoja, “Hakuna hata mmoja wetu atakayeenda nyumbani. Hakuna hata mmoja wetu atakayerudi nyumbani kwake. Sasa hili ndilo tutakaloitendea Gibea: Tutaikabili jinsi kura itakavyotuongoza. Tutatoa watu kumi katika kila mia moja kutoka kwenye makabila yote ya Israeli, watu mia moja katika kila elfu moja, na watu elfu moja katika kila elfu kumi, ili waende wakalete mahitaji kwa ajili ya jeshi. Basi wakati jeshi litakapofika Gibea ya Benyamini, watawatendea yale wanayostahili, kwa ajili ya uovu huu walioutenda katika Israeli.” Hivyo wanaume wote wa Israeli wakakutanika pamoja na kujiunga kama mtu mmoja dhidi ya huo mji. Makabila ya Israeli yakatuma watu kwenda katika kabila la Benyamini lote na kuwaambia, “Ni uovu gani huu wa kutisha uliotendeka kati yenu? Basi watoeni hao wanaume waovu wa Gibea, ili tupate kuwaua na kuuondoa uovu katika Israeli.” Lakini Wabenyamini hawakuwasikia ndugu zao, Waisraeli. Wakatoka katika miji yao, wakakutanika Gibea ili kupigana na Waisraeli. Siku ile Wabenyamini wakakusanya watu elfu ishirini na sita kutoka miji yao waliojifunga panga, mbali na hao vijana wenye uwezo mia saba kutoka wale walioishi Gibea. Miongoni mwa askari hao, palikuwa na askari mia saba waliochaguliwa waliotumia mkono wa kushoto; kila mmoja wao angetupa jiwe kwa kombeo na kulenga unywele bila kukosa. Nao wanaume wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, wakakusanya wanaume elfu mia nne hodari wenye panga. Waisraeli wakapanda Betheli na kumuuliza Mungu, “Ni nani miongoni mwetu atakayetangulia mbele yetu ili kupigana na Wabenyamini?” BWANA akawajibu, “Yuda ndiye atakayetangulia.” Kesho yake asubuhi, Waisraeli wakaamka na kupiga kambi karibu na Gibea. Waisraeli wakaondoka ili kupigana na Wabenyamini, nao Waisraeli wakachukua nafasi zao katika vita huko Gibea. Wabenyamini wakatoka Gibea na kuwaua Waisraeli elfu ishirini na mbili siku hiyo. Lakini Waisraeli wakatiana moyo kila mmoja na mwenzake, nao wakachukua tena nafasi zao katika vile vita mahali pale walipokuwa siku ya kwanza. Waisraeli wakapanda mbele za BWANA na kulia mbele zake hadi jioni. Nao wakamuuliza BWANA, “Je, tupande tena kupigana vita na Wabenyamini, ndugu zetu?” BWANA akajibu, “Pandeni mkapigane nao.” Ndipo Waisraeli wakawakaribia Wabenyamini siku ya pili. Wakati huu, Wabenyamini walipotoka Gibea ili kupigana na Waisraeli, wakawaua wanaume elfu kumi na nane wenye panga. Ndipo jeshi lote, na Waisraeli wote, wakapanda Betheli, na huko wakakaa mbele za BWANA wakilia. Wakafunga siku hiyo hadi jioni na kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya amani kwa BWANA. Nao Waisraeli wakauliza ushauri kwa BWANA. (Katika siku hizo Sanduku la Agano la Mungu lilikuwa huko, na Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anahudumu mbele za hilo Sanduku.) Wakauliza, “Je, tupande tena kwenda vitani kupigana na Wabenyamini, ndugu zetu, au la?” BWANA akajibu, “Nendeni, kwa kuwa kesho nitawatia mikononi mwenu.” Basi Waisraeli wakaweka waviziaji kuizunguka Gibea. Kisha Waisraeli wakapanda kupigana na Wabenyamini katika siku ya tatu na kuchukua nafasi zao dhidi ya Gibea kama walivyokuwa wamefanya hapo awali. Wabenyamini wakatoka ili kukabiliana na Waisraeli, ambao waliwavuta Wabenyamini watoke katika mji. Wakaanza kupigana na wakawaua watu wapatao thelathini wa Israeli, kama walivyofanya nyakati nyingine, katika uwanja na katika njia kuu, moja iendayo Betheli na nyingine Gibea. Wabenyamini walipokuwa wakiambiana, “Wanapigwa mbele yetu kama hapo awali,” nao Waisraeli waliambiana, “Turudini nyuma ili tuwavute wauache mji, waende kuelekea barabarani.” Wanaume wote wa Israeli wakaondoka kwenye nafasi zao na kujipanga huko Baal-Tamari, nao wale waviziaji wa Waisraeli wakatoka ghafula walipokuwa kwenye uwanda wa magharibi mwa Gibea. Ndipo vijana wenye uwezo elfu kumi katika Israeli wakaja kuishambulia Gibea. Vita vilikuwa vikali sana, hata Wabenyamini hawakutambua kuwa maangamizi yalikuwa karibu nao. BWANA akawashinda Wabenyamini mbele ya Waisraeli, na siku hiyo Waisraeli wakawaua Wabenyamini elfu ishirini na tano na mia moja wenye panga. Hivyo Wabenyamini wakaona kuwa wameshindwa. Basi Waisraeli walikuwa wamewaondokea Wabenyamini, kwa sababu Waisraeli waliwategemea hao waviziaji waliokuwa wamewaweka karibu na Gibea. Wale waviziaji wakafanya haraka kuingia Gibea, wakasambaa na kuwaua watu wote wa mji kwa upanga. Waisraeli walikuwa wamekubaliana na hao waviziaji kuwa wangesababisha wingu kubwa la moshi lipande kutoka huo mji, ndipo Waisraeli wangegeuka kupigana. Wabenyamini walikuwa wameanza kuwapiga na kuwaua Waisraeli (wapatao thelathini), hivyo wakasema, “Hakika tunawashinda kama tulivyowashinda katika vita hapo awali.” Lakini nguzo ya moshi ilipoanza kupanda kutoka mji ule, Wabenyamini wakageuka, na tazama: katika mji mzima, moshi ulikuwa ukipaa angani. Ndipo Waisraeli wakawageukia, nao Wabenyamini wakatiwa hofu, kwa kuwa walitambua kwamba maafa yamewajia. Basi wakakimbia mbele ya Waisraeli kuelekea nyikani, lakini hawakuweza kukwepa vile vita. Nao Waisraeli waliotoka katika ile miji wakawaua huko. Wakawazingira Wabenyamini pande zote, wakawafuatia na kuwafikia karibu na Gibea upande wa mashariki. Wakaanguka Wabenyamini elfu kumi na nane, wote wapiganaji hodari. Walipogeuka na kukimbia kuelekea nyikani hata kufikia mwamba wa Rimoni, Waisraeli wakawaua watu elfu tano huko njiani. Wakawafuatia kwa karibu hadi Gidomu, na huko wakawaua wanaume wengine elfu mbili. Siku hiyo wakawaua Wabenyamini elfu ishirini na tano wenye panga, wapiganaji hodari. Lakini watu mia sita wakakimbia kuelekea nyikani katika mwamba wa Rimoni, na kukaa huko muda wa miezi minne. Waisraeli wakarudi na kuwaua kwa upanga Wabenyamini wote, pamoja na wanyama na kila walichokipata. Pia kila mji waliouona wakauchoma kwa moto.