Waamuzi 2:8-15
Waamuzi 2:8-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Yoshua mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alifariki akiwa na umri wa miaka 110. Wakamzika katika sehemu aliyogawiwa iwe yake huko Timnath-heresi, katika nchi ya milima ya Efraimu kaskazini ya mlima Gaashi. Kisha watu wote wa kizazi chake walifariki, kikafuata kizazi kingine ambacho hakikumjua Mwenyezi-Mungu wala matendo aliyowatendea watu wa Israeli. Basi, Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu Mabaali. Walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao, ambaye aliwatoa katika nchi ya Misri, wakaifuata miungu mingine, miungu iliyoabudiwa na watu walioishi kandokando yao. Waliisujudia miungu hiyo, wakamkasirisha sana Mwenyezi-Mungu. Walimwacha Mwenyezi-Mungu, wakatumikia Mabaali na Maashtarothi. Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya Israeli, naye akawaacha wanyanganyi wapore mali zao. Aliwakabidhi kwa adui zao waliowazunguka hata wasiweze tena kuwapinga. Kila walipokwenda kupigana, mkono wa Mwenyezi-Mungu uliwakabili kuwaletea balaa, kama alivyokuwa amewaonya na kuapa. Nao wakawa katika huzuni kubwa.
Waamuzi 2:8-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, naye alikuwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua BWANA, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Wana wa Israeli walifanya mambo maovu mbele za macho ya BWANA, na wakawatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika. Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda mkono wa BWANA ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama BWANA alivyosema, na kama BWANA alivyowaapia; nao wakafadhaika sana.
Waamuzi 2:8-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, naye alipata umri wa miaka mia na kumi. Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua BWANA, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakawatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika. Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda mkono wa BWANA ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama BWANA alivyosema, na kama BWANA alivyowaapia; nao wakafadhaika sana.
Waamuzi 2:8-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Heresi katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini mwa Mlima Gaashi. Baada ya kizazi kile chote kukusanywa pamoja na baba zao, kikainuka kizazi kingine baada yao ambacho hakikumjua BWANA, wala matendo yale aliyokuwa ametenda kwa ajili ya Waisraeli. Kwa hiyo Waisraeli wakatenda maovu machoni pa BWANA na kuwatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyekuwa amewatoa katika nchi ya Misri. Wakaifuata na kuiabudu miungu mbalimbali ya mataifa yaliyowazunguka. Wakamkasirisha BWANA, kwa sababu walimwacha na kutumikia Baali na Maashtorethi. Hivyo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa wavamizi waliowateka nyara. Akawauza katika mikono ya adui zao pande zote, hivyo hawakuweza tena kuwazuia adui zao. Wakati wowote Israeli walipotoka kwenda kupigana, mkono wa BWANA ulikuwa kinyume nao ili awashinde, kama vile alivyokuwa amewaapia. Nao wakawa katika taabu kubwa.