Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 2:11-23

Waamuzi 2:11-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu Mabaali. Walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao, ambaye aliwatoa katika nchi ya Misri, wakaifuata miungu mingine, miungu iliyoabudiwa na watu walioishi kandokando yao. Waliisujudia miungu hiyo, wakamkasirisha sana Mwenyezi-Mungu. Walimwacha Mwenyezi-Mungu, wakatumikia Mabaali na Maashtarothi. Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya Israeli, naye akawaacha wanyanganyi wapore mali zao. Aliwakabidhi kwa adui zao waliowazunguka hata wasiweze tena kuwapinga. Kila walipokwenda kupigana, mkono wa Mwenyezi-Mungu uliwakabili kuwaletea balaa, kama alivyokuwa amewaonya na kuapa. Nao wakawa katika huzuni kubwa. Ndipo Mwenyezi-Mungu akawapa waamuzi ambao waliwaokoa mikononi mwa watu waliopora mali zao. Hata hivyo, Waisraeli hawakuwasikiliza waamuzi wao, maana walifanya kama wazinzi kwa kufuata miungu mingine na kuisujudia. Waliacha upesi nyayo walizofuata babu zao ambao walitii amri za Mwenyezi-Mungu; bali wao hawakufanya hivyo. Kila mara Mwenyezi-Mungu alipowapelekea mwamuzi, yeye mwenyewe alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa mikononi mwa adui zao muda wote wa uhai wa mwamuzi huyo. Aghalabu, Mwenyezi-Mungu aliwaonea huruma aliposikia kilio chao kutokana na mateso na dhuluma walizofanyiwa. Lakini kila mara mwamuzi alipofariki walirudia mienendo yao ya zamani, wakaishi vibaya kuliko babu zao. Waliifuata miungu mingine, wakaitumikia na kuisujudia, wala hawakuyaacha matendo yao wala ukaidi wao. Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akawaka hasira dhidi ya Waisraeli, akasema, “Kwa kuwa watu hawa wamevunja agano nililofanya na babu zao, wakakataa kutii sauti yangu, sitayafukuza tena mataifa ambayo Yoshua aliyabakiza, wakati alipofariki. Nitayatumia mataifa hayo kuwajaribu Waisraeli nione kama watairudia njia yangu kama babu zao au sivyo.” Basi, Mwenyezi-Mungu akayaacha mataifa hayo, wala hakuyafukuza mara moja, wala hakumpa Yoshua ushindi juu ya mataifa hayo!

Shirikisha
Soma Waamuzi 2

Waamuzi 2:11-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wana wa Israeli walifanya mambo maovu mbele za macho ya BWANA, na wakawatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika. Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda mkono wa BWANA ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama BWANA alivyosema, na kama BWANA alivyowaapia; nao wakafadhaika sana. Kisha BWANA akawainua waamuzi, waliowaokoa mikononi mwa watu hao waliowateka nyara. Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za BWANA bali wao hawakufanya hivyo. Na kila wakati BWANA alipowainulia waamuzi, ndipo BWANA alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana BWANA alisikitishwa na kilio chao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua. Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi. Basi hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili limelivunja agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu; mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa; ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kama wataifuata njia ya BWANA kwenda katika njia hiyo, au sivyo. Basi BWANA akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.

Shirikisha
Soma Waamuzi 2

Waamuzi 2:11-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakawatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika. Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda mkono wa BWANA ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama BWANA alivyosema, na kama BWANA alivyowaapia; nao wakafadhaika sana. Kisha BWANA akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara. Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za BWANA bali wao hawakufanya hivyo. Na wakati BWANA alipowainulia waamuzi, ndipo BWANA alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana BWANA alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua. Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi. Basi hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu; mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa; ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kwamba wataishika njia ya BWANA kwenda katika njia hiyo, au sivyo. Basi BWANA akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.

Shirikisha
Soma Waamuzi 2

Waamuzi 2:11-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kwa hiyo Waisraeli wakatenda maovu machoni pa BWANA na kuwatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyekuwa amewatoa katika nchi ya Misri. Wakaifuata na kuiabudu miungu mbalimbali ya mataifa yaliyowazunguka. Wakamkasirisha BWANA, kwa sababu walimwacha na kutumikia Baali na Maashtorethi. Hivyo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa wavamizi waliowateka nyara. Akawauza katika mikono ya adui zao pande zote, hivyo hawakuweza tena kuwazuia adui zao. Wakati wowote Israeli walipotoka kwenda kupigana, mkono wa BWANA ulikuwa kinyume nao ili awashinde, kama vile alivyokuwa amewaapia. Nao wakawa katika taabu kubwa. Ndipo BWANA akawainua waamuzi, ambao waliwaokoa kutoka mikononi mwa hao wavamizi. Lakini hawakuwasikiliza hata waamuzi wao, bali walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine na kuiabudu. Waligeuka upesi na kuiacha njia ambayo baba zao waliiendea, yaani njia ya kutii amri za BWANA. Kila mara BWANA alipowainulia mwamuzi, BWANA alikuwa pamoja na huyo mwamuzi, naye aliwaokoa kutoka mikononi mwa adui zao kwa kipindi chote alichoishi yule mwamuzi. Kwa kuwa BWANA aliwahurumia kwa sababu ya kilio chao cha huzuni kwa ajili ya wale waliokuwa wakiwatesa na kuwataabisha. Lakini kila mara mwamuzi alipofariki, watu walirudia katika hali mbaya ya uovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine, ili kuitumikia na kuiabudu. Walikataa kuacha matendo yao maovu na njia zao za ukaidi. Kwa hiyo BWANA akawakasirikia sana Israeli na kusema, “Kwa kuwa taifa hili limevunja agano lile nililofanya na baba zao na hawakunisikiliza, mimi nami sitafukuza taifa lolote ambalo Yoshua aliliacha alipofariki. Nitawatumia mataifa hao ili nipate kuwapima Israeli, nione kama wataishika njia ya BWANA na kuenenda kwa njia hiyo jinsi baba zao walivyofanya.” BWANA alikuwa ameyaacha hayo mataifa yabaki; hakuyaondoa mara moja kwa kuyatia mikononi mwa Yoshua.

Shirikisha
Soma Waamuzi 2