Waamuzi 2:1-6
Waamuzi 2:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Malaika wa Mwenyezi-Mungu aliondoka Gilgali, akaenda Bokimu, akawaambia Waisraeli, “Niliwatoa nchini Misri na kuwaleta katika nchi ambayo niliwaahidi kwa kiapo babu zenu. Nilisema kwamba sitalivunja agano langu nanyi kamwe. Na kwa upande wenu niliwaamuru msifanye agano na wenyeji wa nchi hii na kwamba madhabahu zao mtazibomoa. Lakini nyinyi hamkuitii amri yangu. Kwa nini mambo haya? Kwa hiyo sasa nasema: Sitawafukuza tena wakazi wa nchi hii bali watawataabisha, nayo miungu yao itakuwa mtego kwenu.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu alipowaambia watu wote wa Israeli maneno haya, walipaza sauti zao na kulia. Wakapaita mahali hapo Bokimu. Hapo wakamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu. Baada ya Yoshua kuwaaga Waisraeli, kila mmoja alikwenda kwenye eneo lake alilogawiwa ili kuimiliki nchi.
Waamuzi 2:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha malaika wa BWANA alikwea kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hadi nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi; nanyi msifanye agano lolote na hawa wenyeji wa nchi hii; yabomoeni madhabahu yao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani? Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni mtego kwenu. Ikawa, hapo huyo malaika wa BWANA alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia. Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia BWANA sadaka huko. Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi.
Waamuzi 2:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha malaika wa BWANA alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi; nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani? Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu. Ikawa, hapo huyo malaika wa BWANA alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia. Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia BWANA sadaka huko. Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi.
Waamuzi 2:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Malaika wa BWANA akakwea kutoka Gilgali hadi Bokimu, naye akasema, “Niliwapandisha kutoka Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyoapa kuwapa baba zenu. Nikasema, ‘Kamwe sitalivunja agano langu nanyi. Msifanye agano na watu wa nchi hii, bali mtabomoa madhabahu yao.’ Lakini ninyi hamkunitii mimi. Kwa nini mmefanya jambo hili? Sasa basi ninawaambia kuwa sitawafukuza watoke kati yenu, ila watakuwa mitego kwenu, nayo miungu yao itakuwa tanzi kwenu.” Malaika wa BWANA alipomaliza kusema mambo haya kwa Waisraeli wote, watu wakalia kwa sauti kuu. Wakapaita mahali pale Bokimu. Nao wakamtolea BWANA sadaka. Baada ya Yoshua kuwapa watu ruhusa waende zao, Waisraeli wakaenda kwenye urithi wao wenyewe ili kumiliki nchi yao.