Waamuzi 2:1-23
Waamuzi 2:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Malaika wa Mwenyezi-Mungu aliondoka Gilgali, akaenda Bokimu, akawaambia Waisraeli, “Niliwatoa nchini Misri na kuwaleta katika nchi ambayo niliwaahidi kwa kiapo babu zenu. Nilisema kwamba sitalivunja agano langu nanyi kamwe. Na kwa upande wenu niliwaamuru msifanye agano na wenyeji wa nchi hii na kwamba madhabahu zao mtazibomoa. Lakini nyinyi hamkuitii amri yangu. Kwa nini mambo haya? Kwa hiyo sasa nasema: Sitawafukuza tena wakazi wa nchi hii bali watawataabisha, nayo miungu yao itakuwa mtego kwenu.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu alipowaambia watu wote wa Israeli maneno haya, walipaza sauti zao na kulia. Wakapaita mahali hapo Bokimu. Hapo wakamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu. Baada ya Yoshua kuwaaga Waisraeli, kila mmoja alikwenda kwenye eneo lake alilogawiwa ili kuimiliki nchi. Waisraeli walimtumikia Mwenyezi-Mungu siku zote za maisha ya Yoshua na baada ya kifo chake muda wote walioishi wale wazee waliosalia ambao waliyaona matendo makuu ambayo Mwenyezi-Mungu aliwatendea Waisraeli. Yoshua mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alifariki akiwa na umri wa miaka 110. Wakamzika katika sehemu aliyogawiwa iwe yake huko Timnath-heresi, katika nchi ya milima ya Efraimu kaskazini ya mlima Gaashi. Kisha watu wote wa kizazi chake walifariki, kikafuata kizazi kingine ambacho hakikumjua Mwenyezi-Mungu wala matendo aliyowatendea watu wa Israeli. Basi, Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu Mabaali. Walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao, ambaye aliwatoa katika nchi ya Misri, wakaifuata miungu mingine, miungu iliyoabudiwa na watu walioishi kandokando yao. Waliisujudia miungu hiyo, wakamkasirisha sana Mwenyezi-Mungu. Walimwacha Mwenyezi-Mungu, wakatumikia Mabaali na Maashtarothi. Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya Israeli, naye akawaacha wanyanganyi wapore mali zao. Aliwakabidhi kwa adui zao waliowazunguka hata wasiweze tena kuwapinga. Kila walipokwenda kupigana, mkono wa Mwenyezi-Mungu uliwakabili kuwaletea balaa, kama alivyokuwa amewaonya na kuapa. Nao wakawa katika huzuni kubwa. Ndipo Mwenyezi-Mungu akawapa waamuzi ambao waliwaokoa mikononi mwa watu waliopora mali zao. Hata hivyo, Waisraeli hawakuwasikiliza waamuzi wao, maana walifanya kama wazinzi kwa kufuata miungu mingine na kuisujudia. Waliacha upesi nyayo walizofuata babu zao ambao walitii amri za Mwenyezi-Mungu; bali wao hawakufanya hivyo. Kila mara Mwenyezi-Mungu alipowapelekea mwamuzi, yeye mwenyewe alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa mikononi mwa adui zao muda wote wa uhai wa mwamuzi huyo. Aghalabu, Mwenyezi-Mungu aliwaonea huruma aliposikia kilio chao kutokana na mateso na dhuluma walizofanyiwa. Lakini kila mara mwamuzi alipofariki walirudia mienendo yao ya zamani, wakaishi vibaya kuliko babu zao. Waliifuata miungu mingine, wakaitumikia na kuisujudia, wala hawakuyaacha matendo yao wala ukaidi wao. Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akawaka hasira dhidi ya Waisraeli, akasema, “Kwa kuwa watu hawa wamevunja agano nililofanya na babu zao, wakakataa kutii sauti yangu, sitayafukuza tena mataifa ambayo Yoshua aliyabakiza, wakati alipofariki. Nitayatumia mataifa hayo kuwajaribu Waisraeli nione kama watairudia njia yangu kama babu zao au sivyo.” Basi, Mwenyezi-Mungu akayaacha mataifa hayo, wala hakuyafukuza mara moja, wala hakumpa Yoshua ushindi juu ya mataifa hayo!
Waamuzi 2:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha malaika wa BWANA alikwea kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hadi nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi; nanyi msifanye agano lolote na hawa wenyeji wa nchi hii; yabomoeni madhabahu yao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani? Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni mtego kwenu. Ikawa, hapo huyo malaika wa BWANA alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia. Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia BWANA sadaka huko. Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi. Watu hao wakamtumikia BWANA siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioendelea siku zao baada ya Yoshua, hao waliokuwa wameiona hiyo kazi kubwa ya BWANA yote, aliyokuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, naye alikuwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua BWANA, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Wana wa Israeli walifanya mambo maovu mbele za macho ya BWANA, na wakawatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika. Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda mkono wa BWANA ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama BWANA alivyosema, na kama BWANA alivyowaapia; nao wakafadhaika sana. Kisha BWANA akawainua waamuzi, waliowaokoa mikononi mwa watu hao waliowateka nyara. Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za BWANA bali wao hawakufanya hivyo. Na kila wakati BWANA alipowainulia waamuzi, ndipo BWANA alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana BWANA alisikitishwa na kilio chao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua. Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi. Basi hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili limelivunja agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu; mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa; ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kama wataifuata njia ya BWANA kwenda katika njia hiyo, au sivyo. Basi BWANA akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.
Waamuzi 2:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha malaika wa BWANA alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi; nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani? Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu. Ikawa, hapo huyo malaika wa BWANA alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia. Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia BWANA sadaka huko. Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi. Watu hao wakamtumikia BWANA siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioendelea siku zao baada ya Yoshua, hao waliokuwa wameiona hiyo kazi kubwa ya BWANA yote, aliyokuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, naye alipata umri wa miaka mia na kumi. Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua BWANA, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakawatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika. Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. Kila walikokwenda mkono wa BWANA ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama BWANA alivyosema, na kama BWANA alivyowaapia; nao wakafadhaika sana. Kisha BWANA akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara. Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za BWANA bali wao hawakufanya hivyo. Na wakati BWANA alipowainulia waamuzi, ndipo BWANA alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana BWANA alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua. Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi. Basi hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu; mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa; ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kwamba wataishika njia ya BWANA kwenda katika njia hiyo, au sivyo. Basi BWANA akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.
Waamuzi 2:1-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Malaika wa BWANA akakwea kutoka Gilgali hadi Bokimu, naye akasema, “Niliwapandisha kutoka Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyoapa kuwapa baba zenu. Nikasema, ‘Kamwe sitalivunja agano langu nanyi. Msifanye agano na watu wa nchi hii, bali mtabomoa madhabahu yao.’ Lakini ninyi hamkunitii mimi. Kwa nini mmefanya jambo hili? Sasa basi ninawaambia kuwa sitawafukuza watoke kati yenu, ila watakuwa mitego kwenu, nayo miungu yao itakuwa tanzi kwenu.” Malaika wa BWANA alipomaliza kusema mambo haya kwa Waisraeli wote, watu wakalia kwa sauti kuu. Wakapaita mahali pale Bokimu. Nao wakamtolea BWANA sadaka. Baada ya Yoshua kuwapa watu ruhusa waende zao, Waisraeli wakaenda kwenye urithi wao wenyewe ili kumiliki nchi yao. Watu wakamtumikia BWANA siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, wale waliokuwa wameona mambo makuu ambayo BWANA alikuwa ametenda kwa ajili ya Israeli. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Heresi katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini mwa Mlima Gaashi. Baada ya kizazi kile chote kukusanywa pamoja na baba zao, kikainuka kizazi kingine baada yao ambacho hakikumjua BWANA, wala matendo yale aliyokuwa ametenda kwa ajili ya Waisraeli. Kwa hiyo Waisraeli wakatenda maovu machoni pa BWANA na kuwatumikia Mabaali. Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyekuwa amewatoa katika nchi ya Misri. Wakaifuata na kuiabudu miungu mbalimbali ya mataifa yaliyowazunguka. Wakamkasirisha BWANA, kwa sababu walimwacha na kutumikia Baali na Maashtorethi. Hivyo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa wavamizi waliowateka nyara. Akawauza katika mikono ya adui zao pande zote, hivyo hawakuweza tena kuwazuia adui zao. Wakati wowote Israeli walipotoka kwenda kupigana, mkono wa BWANA ulikuwa kinyume nao ili awashinde, kama vile alivyokuwa amewaapia. Nao wakawa katika taabu kubwa. Ndipo BWANA akawainua waamuzi, ambao waliwaokoa kutoka mikononi mwa hao wavamizi. Lakini hawakuwasikiliza hata waamuzi wao, bali walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine na kuiabudu. Waligeuka upesi na kuiacha njia ambayo baba zao waliiendea, yaani njia ya kutii amri za BWANA. Kila mara BWANA alipowainulia mwamuzi, BWANA alikuwa pamoja na huyo mwamuzi, naye aliwaokoa kutoka mikononi mwa adui zao kwa kipindi chote alichoishi yule mwamuzi. Kwa kuwa BWANA aliwahurumia kwa sababu ya kilio chao cha huzuni kwa ajili ya wale waliokuwa wakiwatesa na kuwataabisha. Lakini kila mara mwamuzi alipofariki, watu walirudia katika hali mbaya ya uovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine, ili kuitumikia na kuiabudu. Walikataa kuacha matendo yao maovu na njia zao za ukaidi. Kwa hiyo BWANA akawakasirikia sana Israeli na kusema, “Kwa kuwa taifa hili limevunja agano lile nililofanya na baba zao na hawakunisikiliza, mimi nami sitafukuza taifa lolote ambalo Yoshua aliliacha alipofariki. Nitawatumia mataifa hao ili nipate kuwapima Israeli, nione kama wataishika njia ya BWANA na kuenenda kwa njia hiyo jinsi baba zao walivyofanya.” BWANA alikuwa ameyaacha hayo mataifa yabaki; hakuyaondoa mara moja kwa kuyatia mikononi mwa Yoshua.