Waamuzi 2:1-10
Waamuzi 2:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Malaika wa Mwenyezi-Mungu aliondoka Gilgali, akaenda Bokimu, akawaambia Waisraeli, “Niliwatoa nchini Misri na kuwaleta katika nchi ambayo niliwaahidi kwa kiapo babu zenu. Nilisema kwamba sitalivunja agano langu nanyi kamwe. Na kwa upande wenu niliwaamuru msifanye agano na wenyeji wa nchi hii na kwamba madhabahu zao mtazibomoa. Lakini nyinyi hamkuitii amri yangu. Kwa nini mambo haya? Kwa hiyo sasa nasema: Sitawafukuza tena wakazi wa nchi hii bali watawataabisha, nayo miungu yao itakuwa mtego kwenu.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu alipowaambia watu wote wa Israeli maneno haya, walipaza sauti zao na kulia. Wakapaita mahali hapo Bokimu. Hapo wakamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu. Baada ya Yoshua kuwaaga Waisraeli, kila mmoja alikwenda kwenye eneo lake alilogawiwa ili kuimiliki nchi. Waisraeli walimtumikia Mwenyezi-Mungu siku zote za maisha ya Yoshua na baada ya kifo chake muda wote walioishi wale wazee waliosalia ambao waliyaona matendo makuu ambayo Mwenyezi-Mungu aliwatendea Waisraeli. Yoshua mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alifariki akiwa na umri wa miaka 110. Wakamzika katika sehemu aliyogawiwa iwe yake huko Timnath-heresi, katika nchi ya milima ya Efraimu kaskazini ya mlima Gaashi. Kisha watu wote wa kizazi chake walifariki, kikafuata kizazi kingine ambacho hakikumjua Mwenyezi-Mungu wala matendo aliyowatendea watu wa Israeli.
Waamuzi 2:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha malaika wa BWANA alikwea kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hadi nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi; nanyi msifanye agano lolote na hawa wenyeji wa nchi hii; yabomoeni madhabahu yao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani? Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni mtego kwenu. Ikawa, hapo huyo malaika wa BWANA alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia. Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia BWANA sadaka huko. Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi. Watu hao wakamtumikia BWANA siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioendelea siku zao baada ya Yoshua, hao waliokuwa wameiona hiyo kazi kubwa ya BWANA yote, aliyokuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, naye alikuwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua BWANA, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.
Waamuzi 2:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha malaika wa BWANA alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi; nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani? Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu. Ikawa, hapo huyo malaika wa BWANA alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia. Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia BWANA sadaka huko. Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi. Watu hao wakamtumikia BWANA siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioendelea siku zao baada ya Yoshua, hao waliokuwa wameiona hiyo kazi kubwa ya BWANA yote, aliyokuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, naye alipata umri wa miaka mia na kumi. Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua BWANA, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.
Waamuzi 2:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Malaika wa BWANA akakwea kutoka Gilgali hadi Bokimu, naye akasema, “Niliwapandisha kutoka Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyoapa kuwapa baba zenu. Nikasema, ‘Kamwe sitalivunja agano langu nanyi. Msifanye agano na watu wa nchi hii, bali mtabomoa madhabahu yao.’ Lakini ninyi hamkunitii mimi. Kwa nini mmefanya jambo hili? Sasa basi ninawaambia kuwa sitawafukuza watoke kati yenu, ila watakuwa mitego kwenu, nayo miungu yao itakuwa tanzi kwenu.” Malaika wa BWANA alipomaliza kusema mambo haya kwa Waisraeli wote, watu wakalia kwa sauti kuu. Wakapaita mahali pale Bokimu. Nao wakamtolea BWANA sadaka. Baada ya Yoshua kuwapa watu ruhusa waende zao, Waisraeli wakaenda kwenye urithi wao wenyewe ili kumiliki nchi yao. Watu wakamtumikia BWANA siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, wale waliokuwa wameona mambo makuu ambayo BWANA alikuwa ametenda kwa ajili ya Israeli. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Heresi katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini mwa Mlima Gaashi. Baada ya kizazi kile chote kukusanywa pamoja na baba zao, kikainuka kizazi kingine baada yao ambacho hakikumjua BWANA, wala matendo yale aliyokuwa ametenda kwa ajili ya Waisraeli.