Waamuzi 18:1-31
Waamuzi 18:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku hizo hakukuwa na mfalme katika Israeli. Basi kabila la Dani lilikuwa linatafuta eneo lake lenyewe la kuishi humo, kwani mpaka wakati huo, halikuwa limegawiwa sehemu yake lenyewe miongoni mwa makabila ya Israeli. Hivyo watu wa kabila la Dani walichagua miongoni mwao watu hodari wakawatuma kutoka huko Eshtaoli na Sora wakawaamuru waende kuipeleleza nchi. Basi watu hao wakafika katika nchi ya milima ya Efraimu, nyumbani kwa Mika, wakakaa humo. Walipokuwa nyumbani kwa Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi. Wakamgeukia na kumwuliza, “Nani amekuleta huku? Una shughuli gani hapa?” Yeye akawajibu, “Mika amefanya nami mpango; ameniajiri nami nimekuwa kuhani wake.” Nao wakamwambia, “Tafadhali utuulizie kwa Mwenyezi-Mungu kama tutafanikiwa katika safari yetu.” Yule kuhani akawaambia, “Nendeni kwa amani. Mwenyezi-Mungu anaichunga safari yenu.” Basi, watu hao watano wakaondoka, wakaenda Laishi. Waliwaona watu walioishi huko, na jinsi walivyokaa kwa usalama kama vile watu wa Sidoni. Walikuwa watu watulivu wasio na wasiwasi na hawakupungukiwa mahitaji yoyote nchini. Walikuwa mbali na watu wa Sidoni, na hawakuwa na shughuli yoyote na watu wengine. Basi hao wapelelezi walirudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, nao wakawauliza, “Mmetuletea taarifa gani?” Wao wakasema, “Inukeni twende na kuishambulia nchi hiyo. Tumeiona nchi hiyo, na kweli ni nchi yenye rutuba. Je, mtakaa hapa tu bila kufanya kitu? Msikawie kwenda kuimiliki nchi hiyo. Mtakapofika huko mtakuta watu wasio na wasiwasi wowote. Nchi hiyo ni kubwa, haikupungukiwa chochote na Mungu ameitia mikononi mwetu.” Basi, watu 600 wa kabila la Dani wakiwa na silaha zao za vita wakaondoka kutoka Sora na Eshtaoli wakaenda kupiga kambi yao huko Kiriath-yearimu katika nchi ya Yuda. Ndiyo maana mahali hapo, upande wa magharibi wa Kiriath-yearimu pameitwa Mahane-dani mpaka leo. Kutoka huko wakaelekea nchi ya milima ya Efraimu, wakafika nyumbani kwa Mika. Watu wale watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mnajua kwamba katika nyumba mojawapo ya hizi kuna kizibao, kinyago na sanamu ya kusubu? Basi, fikirini namna ya kufanya.” Basi wale wapelelezi wakaelekea kwenye nyumba ya Mika, wakaingia ndani na kumwuliza habari zake yule kijana Mlawi. Wakati huo, wale watu 600 wa kabila la Dani wakiwa na silaha zao za vita walisimama mlangoni. Wale watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi waliingia ndani, wakachukua ile sanamu mungu ya kusubu, kile kizibao na kinyago cha ibada. Wakati huo yule kuhani alikuwa amesimama mlangoni pamoja na wale watu 600 wenye silaha. Basi, alipowaona wale wapelelezi wameingia nyumbani mwa Mika wakachukua sanamu ya kuchonga, kifuko cha kauli, kinyago na sanamu ile ya kusubu, akawauliza, “Mnafanya nini?” Nao wakamwambia, “Nyamaza, funga mdomo wako, uje pamoja nasi, uwe kuhani wetu na kama baba yetu. Au waonaje? Je, yafaa kwako zaidi kuwa kuhani wa mtu mmoja ama kuwa kuhani wa kabila moja la Israeli?” Yule kuhani akafurahi sana akachukua kile kifuko, kile kinyago cha ibada, na ile sanamu ya mungu ya kusubu, akafuatana nao. Basi, wakaanza safari yao, huku wametanguliwa na watoto wao na mifugo na mali zao. Walipokuwa wamefika mbali na nyumbani kwa Mika, watu waliokuwa jirani na Mika wakaitwa, wakawafuatia watu wa kabila la Dani wakawafikia. Kisha wakawapigia kelele, nao watu wa kabila la Dani wakageuka, wakamwuliza Mika, “Una shida gani hata umetufuatia pamoja na kundi hili lote?” Mika akasema, “Nyinyi mmechukua miungu yangu niliyojitengenezea, mkamchukua na kuhani wangu, mkaniacha bila chochote. Mnawezaje basi kuniuliza nina shida gani?” Watu wa kabila la Dani wakamwambia, “Afadhali uache kelele zako, la sivyo wengine wetu wenye hasira wanaweza wakakuvamia, nawe ukapoteza maisha yako na maisha ya jamaa yako.” Mika alipoona kwamba wamemzidi nguvu, akageuka, akarudi nyumbani; nao watu wa kabila la Dani wakaenda zao. Hao watu wa kabila la Dani walivichukua vitu vile ambavyo Mika alikuwa amevitengeneza, wakamchukua na yule kuhani aliyemhudumia. Basi wakaenda kushambulia Laishi wakawaua wakazi wake ambao waliishi humo kwa utulivu na bila wasiwasi, wakauteketeza mji huo. Wakazi wa mji huo hawakuwa na mtu wa kuwaokoa kwa sababu walikuwa mbali na mji wa Sidoni, tena hawakuwa na uhusiano na watu wengine. Mji huo ulikuwa kwenye bonde la Beth-rehobu. Watu wa kabila la Dani wakaujenga upya, wakaishi humo. Walibadilisha jina la mji huo, wakauita Dani, kufuata jina la babu yao aliyekuwa mwana wa Israeli. Lakini mji huo hapo awali uliitwa Laishi. Watu wa kabila la Dani wakaisimika ile sanamu ya kuchonga, naye Yonathani, mwana wa Gershomu, mwana wa Mose, akawa kuhani wao. Wazawa wake pia walikuwa makuhani wa kabila la Dani mpaka wananchi wa nchi hiyo walipopelekwa uhamishoni. Wakati wote nyumba ya Mungu ilipokuwa huko Shilo, watu wa kabila la Dani waliiabudu sanamu ya kuchonga ambayo Mika aliitengeneza.
Waamuzi 18:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; tena katika siku hizo kabila la Wadani wakajitafutia urithi wapate mahali pa kukaa; maana hawakuwa wamepata urithi wao kati ya makabila ya Israeli. Basi wana wa Dani wakatuma watu watano kutoka kwa koo zao zote, watu mashujaa, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli, ili kuipeleleza hiyo nchi, kuikagua; wakawaambia, Haya, endeni mkaikague nchi hii; basi wakaifikia nchi ya vilima vilima ya Efraimu, hadi nyumba ya huyo Mika, Wakalala huko. Basi hapo walipokuwa karibu na nyumba ya Mika, wakatambua sauti yake huyo kijana Mlawi; ndipo wakageuka wakaenda kuko, na kumwuliza, Je! Ni nani aliyekuleta wewe huku? Unafanya nini mahali hapa? Una kazi gani hapa? Naye akawaambia, Hivi na hivi ndivyo alivyonifanyia Mika, ameniajiri, nami nimekuwa kuhani wake. Nao wakamwambia, Tafadhali tutakie shauri la Mungu, ili tupate kujua kama njia yetu tuiendeayo itafanikiwa. Kuhani akawaambia, Haya endeni na amani; njia mnayoiendea iko mbele za BWANA. Ndipo hao watu watano wakaenda zao, wakafika Laisha, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake, jinsi walivyokaa kwa amani, kama ilivyokuwa desturi ya Wasidoni, watu watulivu na wasioshuku, wasiopungukiwa na chochote duniani, na waliokuwa na miliki; Nao walikuwa mbali na hao Wasidoni, wala hawakutangamana na watu wengine. Kisha wakawarudia ndugu zao huko Sora na Eshtaoli; ndugu zao wakawauliza; Haya, mna habari gani? Wakasema, Haya, inukeni, twende tukapigane nao; kwa maana tumeiona hiyo nchi nayo ni nchi nzuri sana; nanyi, je! Hamtafanya chochote? Msiwe wavivu kwenda, na kuingia, ili mpate kuimiliki nchi hiyo. Hapo mtakapokwenda mtawafikia watu wakaao kwa amani, na hiyo nchi nayo ni kubwa; kwa kuwa Mungu ameitia mikononi mwenu; ni mahali ambapo hapapungukiwi na kitu chochote kilichoko duniani. Basi wakatoka hapo watu mia sita waliovaa silaha za vita, wa jamaa ya Wadani, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli. Wakakwea juu na kupiga kambi huko Kiriath-yearimu, katika Yuda; kwa sababu hiyo wakapaita mahali pale jina lake Mahane-dani hata hivi leo; tazama, ni hapo nyuma ya Kiriath-yearimu. Nao wakapita huko hadi hiyo nchi ya vilima vilima ya Efraimu, wakafikia nyumba ya huyo Mika. Ndipo hao watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisha wakawaambia ndugu zao, Je! Ninyi mwajua ya kwamba mna naivera ndani ya nyumba hizi, na kinyago na sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Basi sasa fikirini iwapasayo kufanya. Basi wakageuka wakaenda kuko, wakafika katika nyumba ya huyo kijana Mlawi, huko nyumbani kwa Mika, kumwamkia. Hao watu mia sita wenye kuvaa silaha zao za vita, waliokuwa ni wana wa Dani, wakasimama penye maingilio ya lango. Na hao watu watano waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi wakakwea juu, wakaingia ndani, na kuitwaa hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu; na huyo kuhani akasimama penye maingilio ya lango pamoja na hao wanaume mia sita waliojihami. Nao hapo walipoingia ndani ya nyumba ya Mika, na kuileta hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu, huyo kuhani akawauliza, Je! Mwafanya nini ninyi? Wao wakamwambia, Nyamaza wewe, weka mkono wako kinywani mwako, uende pamoja nasi, uwe kwetu baba, tena kuhani; je! Ni vema kwako kuwa kuhani kwa ajili ya nyumba ya mtu mmoja, au kuwa kuhani kwa ajili ya kabila na jamaa katika Israeli? Huyo kuhani moyo wake ukafurahi, naye akaitwaa hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kuchonga, akaenda katikati ya hao watu. Basi wakageuka wakaenda zao, lakini watoto wadogo na wanyama wao wa kufugwa, na vyombo vyao, wakawatanguliza mbele yao. Walipokuwa wamekwenda kitambo kizima kutoka nyumba ya Mika, wale watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na nyumba ya Mika walikutana, wakawaandama na kuwapata hao wana wa Dani. Wakawapigia kelele wana wa Dani. Nao wakageuza nyuso zao na kumwambia Mika, Una nini wewe, hata ukaja na mkutano namna hii? Akasema, Ninyi mmeichukua miungu niliyoifanya, na huyo kuhani, nanyi mmekwenda zenu, nami nina nini tena? Basi imekuwaje ninyi kuniuliza, Una nini wewe? Hao wana wa Dani wakamwambia, Hiyo sauti yako isisikike kati yetu, wasije walio na hasira wakakupiga, nawe ukapotewa na uhai wako, pamoja na uhai wa watu wa nyumbani mwako. Basi wana wa Dani wakaenda zao; naye Mika alipoona ya kuwa wanamzidi nguvu, akageuka akarudi nyumbani kwake. Nao wakakitwaa hicho alichokuwa amekifanya Mika, na kuhani aliyekuwa naye nao wakafika Laisha, kwa watu waliokuwa watulivu na wasioshuku, wakawapiga kwa makali ya upanga; wakauteketeza kwa moto mji wao. Wala hakukuwa na mwokozi, kwa sababu huo mji ulikuwa mbali sana na Sidoni, nao hawakutangamana na watu wowote wale; na mji huo ulikuwa katika hilo bonde lililo karibu na Bethrehobu. Nao wakaujenga huo mji na kukaa humo. Wakauita mji jina lake Dani, kwa kulifuata jina la baba yao Dani, aliyezaliwa na Israeli; lakini jina la mji huo hapo awali lilikuwa Laisha. Kisha wana wa Dani wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga; na Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, yeye na wanawe walikuwa ni makuhani katika kabila la Wadani hadi siku nchi hiyo ilipochukuliwa mateka. Basi wakaiabudu hiyo sanamu ya kuchonga aliyotengeneza Mika, wakati wote ile nyumba ya Mungu ilipokuwako huko Shilo.
Waamuzi 18:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; tena katika siku hizo kabila ya Wadani wakajitafutia urithi wapate mahali pa kukaa; maana hata siku hiyo urithi wao haujawaangukia kati ya kabila za Israeli. Basi wana wa Dani wakatuma watu wa jamaa zao, watu watano katika hesabu yao yote, watu mashujaa, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli, ili kuipeleleza hiyo nchi, kuiaua; wakawaambia, Haya, endeni mkaikague nchi hii; basi wakaifikilia nchi ya vilima vilima ya Efraimu, hata nyumba ya huyo Mika, Wakalala huko. Basi hapo walipokuwa karibu na nyumba ya Mika, wakatambua sauti yake huyo hirimu, huyo Mlawi; ndipo wakageuka wakaenda kuko, na kumwuliza, Je! Ni nani aliyekuleta wewe huku? Nawe wafanya nini mahali hapa? Una kazi gani hapa? Naye akawaambia, Hivi na hivi ndivyo alivyonifanyia Mika, ameniajiri, nami nimekuwa kuhani wake. Nao wakamwambia, Tafadhali tutakie shauri la Mungu, ili tupate kujua kwamba njia yetu tuiendeayo itafanikiwa. Kuhani akawaambia, Haya endeni na amani; njia mnayoiendea i mbele za BWANA. Ndipo hao watu watano wakaenda zao, wakafika Laisha, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake, jinsi walivyokaa salama salimini kwa mfano wa walivyokaa hao Wasidoni, wenye starehe na hifadhi, kwa maana hapakuwa na mtu katika nchi hiyo aliyekuwa na amri, aliyeweza kuwatweza katika neno lo lote, nao walikuwa wa mbali na hao Wasidoni, wala hawakuwa na shughuli na mtu ye yote. Kisha wakawarudia ndugu zao huko Sora na Eshtaoli; ndugu zao wakawauliza; Haya, mna habari gani? Wakasema, Haya, inukeni, twende tukapigane nao; kwa maana tumeiona hiyo nchi nayo ni nchi nzuri sana; nanyi, je! Mwanyamaa tu? Msiwe wavivu kwenda, na kuingia, ili mpate kuimiliki nchi hiyo. Hapo mtakapokwenda mtawafikilia watu wakaao salama salimini, na hiyo nchi nayo ni kubwa; kwa kuwa Mungu ameitia mikononi mwenu; ni mahali ambapo hapana kupungukiwa na kitu cho chote kilicho duniani. Basi wakatoka hapo watu mia sita waliovaa silaha za vita, wa jamaa ya Wadani, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli. Wakakwea juu na kupiga kambi huko Kiriath-yearimu, katika Yuda; kwa sababu hiyo wakapaita mahali pale jina lake Mahane-dani hata hivi leo; tazama, ni hapo nyuma ya Kiriath-yearimu. Nao wakapita huko hata hiyo nchi ya vilima vilima ya Efraimu, wakafikilia nyumba ya huyo Mika. Ndipo hao watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisha wakajibu, na kuwaambia ndugu zao Je! Ninyi mwajua ya kwamba mna naivera ndani ya nyumba hizi, na kinyago na sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Basi sasa fikirini iwapasayo kufanya. Basi wakageuka wakaenda kuko, wakafikilia nyumba ya huyo hirimu, Mlawi, hata hiyo nyumba ya Mika, nao wakamwuliza habari za hali yake. Hao watu mia sita wenye kuvaa silaha zao za vita, waliokuwa ni wana wa Dani, wakasimama penye maingilio ya lango. Na hao watu watano waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi wakakwea juu, wakaingia ndani, na kuitwaa hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu; na huyo kuhani akasimama penye maingilio ya lango pamoja na hao watu waume sita mia wenye kuvaa silaha za vita. Nao hapo walipoingia ndani ya nyumba ya Mika, na kuileta hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu, huyo kuhani akawauliza, Je! Mwafanya nini ninyi? Wao wakamwambia, Nyamaza wewe, weka mkono wako kinywani mwako, uende pamoja nasi, uwe kwetu baba, tena kuhani; je! Ni vema kwako kuwa kuhani kwa ajili ya nyumba ya mtu mmoja, au kuwa kuhani kwa ajili ya kabila na jamaa katika Israeli? Huyo kuhani moyo wake ukafurahi, naye akaitwaa hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kuchonga, akaenda katikati ya hao watu. Basi wakageuka wakaenda zao, lakini watoto wadogo na wanyama wao wa mifugo, na vyombo vyao, wakawatanguliza mbele yao. Walipokuwa wamekwenda kitambo kizima kutoka nyumba ya Mika, wale watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na nyumba ya Mika walikutana, wakawaandama na kuwapata hao wana wa Dani. Wakawapigia kelele wana wa Dani. Nao wakageuza nyuso zao na kumwambia Mika, Una nini wewe, hata ukaja na mkutano namna hii? Akasema, Ninyi mmeichukua miungu niliyoifanya, na huyo kuhani, nanyi mmekwenda zenu, nami nina nini tena? Basi imekuwaje ninyi kuniuliza, Una nini wewe? Hao wana wa Dani wakamwambia, Hiyo sauti yako isisikiwe kati yetu, wasije walio na hasira wakakuangukia, nawe ukapotewa na uhai wako, pamoja na uhai wa watu wa nyumbani mwako. Basi wana wa Dani wakaenda zao; naye Mika alipoona ya kuwa ni wenye nguvu kumshinda yeye, akageuka akarudi nyumbani kwake. Nao wakakitwaa hicho alichokuwa amekifanya Mika, na kuhani aliyekuwa naye nao wakafikilia Laisha, kwenye watu waliokuwa wenye starehe na hifadhi, wakawapiga kwa makali ya upanga; wakaupiga moto mji wao. Wala hakuwako mwokozi, kwa sababu huo mji ulikuwa ni mbali sana na Sidoni, nao hawakuwa na shughuli na mtu awaye yote; na mji huo ulikuwa katika hilo bonde lililo karibu na Bethrehobu. Nao wakaujenga huo mji na kukaa humo. Wakauita mji jina lake Dani, kwa kuliandama jina la baba yao Dani, aliyezaliwa kwake Israeli; lakini jina la mji huo hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Laisha. Kisha wana wa Dani wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga; na Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, yeye na wanawe walikuwa ni makuhani katika kabila ya Wadani hata siku ya kuchukuliwa mateka hiyo nchi. Basi wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga aliyoifanya Mika, wakati wote ile nyumba ya Mungu ilipokuwako huko Shilo.
Waamuzi 18:1-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika siku hizo, Waisraeli hawakuwa na mfalme. Katika siku hizo, watu wa kabila la Dani walikuwa wanatafuta mahali pao wenyewe pa kuishi, kwa sababu walikuwa hawajafika kwenye urithi wao miongoni mwa makabila ya Israeli. Hivyo Wadani wakatuma mashujaa watano kutoka Sora na Eshtaoli ili kupeleleza nchi na kuichunguza. Hawa mashujaa waliwakilisha koo zao zote. Waliwaambia, “Nendeni mkaichunguze hiyo nchi.” Wanaume hao wakaingia katika nchi ya vilima ya Efraimu, wakafika nyumba ya Mika, ambako walilala usiku huo. Walipofika karibu na nyumba ya Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi; hivyo wakaingia humo na kumuuliza, “Ni nani aliyekuleta hapa? Unafanya nini mahali hapa? Kwa nini uko hapa?” Akawaeleza yale Mika aliyomtendea, akasema, “Ameniajiri, nami ni kuhani wake.” Kisha wakamwambia, “Tafadhali tuulizie kwa Mungu kama safari yetu itafanikiwa.” Yule kuhani akawajibu, “Nendeni kwa amani. Safari yenu ina kibali cha BWANA.” Basi hao wanaume watano wakaondoka na kufika Laishi, mahali ambapo waliwakuta watu wanaishi salama, kama Wasidoni, kwa amani na utulivu. Nchi yao haikupungukiwa kitu, hivyo wakastawi. Pia walikaa mbali sana na Wasidoni, wala hawakushughulika na mtu yeyote. Waliporudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, ndugu zao wakawauliza, “Mlionaje mambo huko?” Wakajibu, “Twendeni, tukawavamie! Tumeona kuwa nchi ni nzuri sana. Je, hamtafanya chochote? Msisite kupanda ili kuimiliki. Mtakapofika huko, mtawakuta watu walio salama, na nchi kubwa ambayo Mungu ameitia mikononi mwenu, isiyopungukiwa kitu chochote duniani.” Ndipo wanaume mia sita kutoka ukoo wa Wadani, waliojifunga silaha za vita, wakaondoka Sora na Eshtaoli. Walipokuwa wakisafiri wakapiga kambi huko Kiriath-Yearimu katika Yuda. Hii ndiyo sababu sehemu ya magharibi ya Kiriath-Yearimu inaitwa Mahane-Dani hadi leo. Kutoka hapo wakaenda hadi nchi ya vilima ya Efraimu na kufika katika nyumba ya Mika. Ndipo wale wanaume watano waliopeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mnajua kuwa katika mojawapo ya nyumba hizi kuna kizibau, miungu ya nyumbani, sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Sasa basi, fikirini mtakalofanya.” Basi wakaelekea huko, wakafika kwa yule kijana Mlawi, katika nyumba ya Mika, wakamsalimu. Wale Wadani mia sita, wakiwa wamejifunga silaha, wakasimama penye ingilio la lango. Wale watu watano walioenda kupeleleza nchi wakaingia ndani na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, kile kizibau, na ile miungu ya nyumbani, na ile sanamu ya kusubu, wakati yule kuhani akiwa amesimama pale penye ingilio la lango pamoja na wale watu mia sita waliojifunga silaha. Hao watu walipoingia katika nyumba ya Mika na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, kile kizibau, na ile miungu ya nyumbani, na ile sanamu ya kusubu, yule kuhani akawauliza, “Mnafanya nini?” Wakamjibu, “Nyamaza! Weka mkono wako juu ya kinywa chako na ufuatane nasi, uwe baba yetu na kuhani wetu. Si ni afadhali utumikie kabila na ukoo katika Israeli kama kuhani kuliko kumtumikia mtu mmoja na watu wa nyumbani mwake?” Yule kuhani akafurahi. Akachukua kile kizibau, ile miungu ya nyumbani, na sanamu ya kuchonga, naye akaenda pamoja na wale watu. Ndipo wakageuka na kuondoka, wakiwatanguliza mbele watoto wao wadogo, mifugo na mali yao. Walipokuwa wamefika mbali toka nyumbani kwa Mika, watu walioishi karibu na Mika walikusanywa pamoja, nao wakawakimbiza Wadani. Walipofuatilia huku wakipiga kelele, Wadani wakageuka, wakamwambia Mika, “Una nini wewe hata ukawaita watu waje kupigana nasi?” Akawajibu, “Mmechukua miungu niliyoitengeneza, mkamchukua kuhani wangu, nanyi mkaondoka. Nimebaki na nini kingine? Mnawezaje kuniuliza, ‘Una nini wewe?’ ” Wadani wakamjibu, “Usibishane nasi, la sivyo watu wenye hasira watakushambulia, nawe na watu wa nyumbani mwako mtapoteza maisha yenu.” Basi Wadani wakaenda zao, naye Mika alipoona kuwa wana nguvu kuliko yeye, akageuka na kurudi nyumbani mwake. Kisha wakachukua vitu vile Mika alikuwa amevitengeneza, na kuhani wake, wakaendelea hadi Laishi, dhidi ya watu walioishi na amani na utulivu. Wakawashambulia kwa upanga na kuuteketeza mji wao. Hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa, kwa kuwa waliishi mbali na Sidoni, na hawakuwa na ushirikiano na mtu mwingine yeyote. Mji huo ulikuwa kwenye bonde karibu na Beth-Rehobu. Wadani wakaujenga upya huo mji na kuishi humo. Wakauita ule mji Dani kwa kufuata jina la baba yao aliyezaliwa na Israeli, ingawa mji huo uliitwa Laishi hapo awali. Kule Wadani wakajisimamishia ile sanamu ya kuchonga, naye Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa pamoja na wanawe walikuwa makuhani kwa kabila la Dani hadi nchi hiyo ilipotekwa. Wakaendelea kuiabudu ile sanamu ambayo Mika alizitengeneza, wakati wote ule nyumba ya Mungu ilikuwa huko Shilo.