Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 16:21-30

Waamuzi 16:21-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Wafilisti walimkamata, wakamngoa macho, wakampeleka Gaza, wakamfunga kwa pingu za shaba, na kumlazimisha kufanya kazi ya kusaga unga huko gerezani. Lakini nywele zake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa. Wakuu wa Wafilisti walikusanyika ili kusherehekea na kumtolea tambiko mungu wao aitwaye Dagoni. Basi, wakawa wanaimba, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu Samsoni.” Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao na kusema, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu ambaye amekuwa akiharibu nchi yetu na kuwaua wengi wetu.” Walipojawa na furaha sana mioyoni mwao, wakasema, “Mleteni Samsoni atutumbuize.” Basi wakamtoa Samsoni gerezani, wakamleta naye akawatumbuiza. Wakamweka katikati ya nguzo. Samsoni akamwambia kijana aliyekuwa anamwongoza, “Niruhusu nizipapase nguzo zinazotegemeza jumba hili ili nami niziegemee.” Jumba hilo lilikuwa limejaa watu: Wakuu wote wa Wafilisti walikuwapo na kwenye paa kulikuwa na watu 3,000 wanaume na wanawake, wakimtazama Samsoni akiwatumbuiza. Hapo Samsoni akamwomba Mwenyezi-Mungu: “Bwana Mwenyezi-Mungu nakuomba unikumbuke. Nitie nguvu, mara hii moja tu, ee Mungu, ili niwalipize kisasi mara moja hii tu Wafilisti ambao waliyangoa macho yangu mawili.” Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo zilitegemeza uzito wote wa jumba hilo, mkono mmoja nguzo hii na mkono mwingine nguzo ya pili. Kisha akasema, “Na nife pamoja na Wafilisti.” Akasukuma kwa nguvu zake zote. Jumba likawaangukia wakuu hao wote wa Wafilisti waliokuwamo humo ndani. Wale waliouawa wakati wa kifo chake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake.

Shirikisha
Soma Waamuzi 16

Waamuzi 16:21-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakateremka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza. Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake. Kisha wakuu wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana walisema, mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu. Na hao watu walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, mungu wetu amemtia mikononi mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu. Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili. Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea. Basi nyumba ile ilikuwa imejaa wanaume kwa wanawake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu wanaume kwa wanawake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza. Samsoni akamwita BWANA, akasema, Ee Bwana MUNGU, nikumbuke nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili. Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akaziegemea, moja kwa mkono wake wa kulia na moja kwa mkono wake wa kushoto. Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake.

Shirikisha
Soma Waamuzi 16

Waamuzi 16:21-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza. Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake. Kisha wakuu wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana walisema, Mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu. Na hao watu walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, Mungu wetu amemtia mikononi mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu. Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili. Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea. Basi nyumba ile ilikuwa imejaa watu waume kwa wake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu waume kwa wake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza. Samsoni akamwita BWANA, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili. Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto. Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake.

Shirikisha
Soma Waamuzi 16

Waamuzi 16:21-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi Wafilisti wakamkamata, wakamngʼoa macho yake, wakamteremsha hadi Gaza. Wakamfunga kwa pingu za shaba, wakamweka gerezani ili asage ngano. Wakati huo nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa. Basi viongozi wa Wafilisti wakakusanyika pamoja ili kutoa kafara kuu kwa mungu wao Dagoni, wakisherehekea na kusema, “Mungu wetu amemtia adui yetu Samsoni mikononi mwetu.” Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao, wakisema: “Sasa mungu wetu amemtia adui yetu mikononi mwetu, yule aliyeharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.” Mioyo yao ilipokuwa imefurahishwa, wakapaza sauti, wakisema, “Mleteni Samsoni aje ili atutumbuize.” Basi wakamleta Samsoni kutoka gerezani, naye akawatumbuiza. Wakamsimamisha katikati ya nguzo mbili. Samsoni akamwambia mtumishi aliyeushika mkono wake, “Niweke mahali ambapo ninaweza kuzigusa nguzo ambazo zinategemeza jengo ili nipate kuziegemea.” Basi lile jengo lilikuwa na wanaume na wanawake wengi; viongozi wote wa Wafilisti walikuwa humo, na kwenye dari walikuwepo watu wapatao elfu tatu, wanaume kwa wanawake, wakimtazama Samsoni akiwatumbuiza. Ndipo Samsoni akamwomba BWANA, akasema, “Ee BWANA Mwenyezi, unikumbuke. Ee Mungu, nakusihi ukanitie nguvu mara hii moja tu, ili kwa tendo hili nipate kulipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa sababu ya macho yangu mawili.” Ndipo Samsoni akazikaribia zile nguzo mbili za katikati zilizokuwa zimelisimamisha lile jengo. Akazishika moja kwa mkono wa kuume, na nyingine kwa mkono wa kushoto. Samsoni akasema, “Acha nife pamoja na Wafilisti!” Ndipo akazisukuma zile nguzo kwa nguvu zake zote, nalo jengo lile likaanguka juu ya viongozi na watu wote waliokuwamo ndani. Hivyo, akawaua watu wengi wakati wa kufa kwake kuliko siku za uhai wake.

Shirikisha
Soma Waamuzi 16