Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 16:1-25

Waamuzi 16:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku moja Samsoni alikwenda mjini Gaza, akakutana na malaya mmoja akalala naye. Watu wa Gaza walipoambiwa kuwa Samsoni yuko huko, walilizingira eneo hilo na kumvizia kwenye lango la mji usiku kucha. Wakakaa kimya huko langoni usiku wote wakifikiri kwamba wanaweza kungojea mpaka mapambazuko wapate kumuua. Lakini Samsoni akabaki mjini mpaka usiku wa manane. Wakati wa usiku wa manane akaamka akashika miimo miwili ya malango, akaingoa pamoja na makomeo yake akaibeba na kwenda nayo mpaka karibu na Hebroni. Baada ya hayo, Samsoni alimpenda mwanamke mmoja aitwaye Delila ambaye aliishi katika bonde la Soreki. Wakuu wa Wafilisti wakamjia Delila, wakamwambia, “Mbembeleze Samsoni ili ujue asili ya nguvu zake nyingi ili tuweze kumkamata na kumfunga. Ukifanya hivyo, kila mmoja wetu atakupa vipande thelathini vya fedha.” Delila akamwambia Samsoni, “Tafadhali, niambie asili ya nguvu zako, na jinsi gani mtu anaweza kukushinda na kukufunga.” Samsoni akamjibu, “Wakinifunga kwa kamba saba mbichi za upinde, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” Wakuu wa Wafilisti wakamletea Delila kamba hizo saba mbichi za upinde, naye akamfunga Samsoni kwa kamba hizo. Delila alikuwa ameweka watu wamvizie katika chumba cha ndani. Kisha, akamwambia Samsoni kwa sauti kubwa, “Samsoni, Wafilisti wamekujia kukushambulia.” Samsoni akazikata kamba hizo kama nyuzi za kitani zinapogusa moto. Hivyo hakuna aliyegundua siri ya nguvu zake. Delila akamwambia Samsoni, “Wewe umenidhihaki. Umenidanganya. Tafadhali niambie jinsi unavyoweza kufungwa.” Samsoni akamjibu, “Wakinifunga kwa kamba mpya ambazo hazijatumiwa, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” Basi, Delila akachukua kamba mpya, akamfunga nazo. Kisha akamwambia Samsoni kwa sauti kubwa, “Samsoni! Wafilisti wamekuja kukushambulia!” Wakati huo kulikuwa na watu chumbani wakimvizia. Samsoni akazikata kamba hizo kama uzi. Delila akamwambia Samsoni, “Mpaka sasa bado unanidhihaki. Umenidanganya. Niambie unavyoweza kufungwa.” Samsoni akamwambia, “Ukivisuka vishungi vyangu saba vya nywele zangu katika mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi, nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” Wakati Samsoni alipokuwa analala Delila akavisuka pamoja vishungi saba vya nywele za Samsoni akavifunga kwa mtandio wa nguo na kuvikaza kabisa kwa kigingi. Kisha akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia.” Samsoni akaamka kutoka usingizini akakingoa kile kigingi na kuutatua ule mtandio wa nguo. Delila akamwambia Samsoni, “Unawezaje kusema kuwa unanipenda na moyo wako hauko pamoja nami? Umenidhihaki sasa mara tatu. Hujaniambia asili ya nguvu zako iko wapi.” Delila alipoendelea kumbana sana Samsoni kwa maneno, siku baada ya siku na kumkera hata akachoka rohoni karibu kufa, hakuweza kuvumilia, akamfunulia siri yake, akisema, “Nywele zangu kamwe hazijapata kunyolewa. Mimi nimewekwa wakfu kwa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nikinyolewa nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu kama mtu yeyote.” Basi, Delila alipoona kwamba Samsoni amemwambia siri yake yote, akawaita wakuu wa Wafilisti, akawaambia, “Njoni safari hii moja tu maana Samsoni ameniambia siri yake yote.” Wakuu wa Wafilisti wakamwendea Delila huku wamemletea fedha walizomwahidi. Naye Delila akamfanya Samsoni alale usingizi magotini mwake, akamwita mtu amnyoe vile vishungi vyake saba. Kisha Delila akaanza kumtesa Samsoni kwa kuwa sasa nguvu zilikuwa zimemtoka. Delila akamwambia Samsoni, “Samsoni! Wafilisti wanakuja kukushambulia!” Samsoni akaamka usingizini huku akifikiri kwamba atatoka na kujiokoa kama hapo awali. Kumbe hakujua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwacha. Wafilisti walimkamata, wakamngoa macho, wakampeleka Gaza, wakamfunga kwa pingu za shaba, na kumlazimisha kufanya kazi ya kusaga unga huko gerezani. Lakini nywele zake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa. Wakuu wa Wafilisti walikusanyika ili kusherehekea na kumtolea tambiko mungu wao aitwaye Dagoni. Basi, wakawa wanaimba, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu Samsoni.” Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao na kusema, “Mungu wetu amemtia mikononi mwetu adui yetu ambaye amekuwa akiharibu nchi yetu na kuwaua wengi wetu.” Walipojawa na furaha sana mioyoni mwao, wakasema, “Mleteni Samsoni atutumbuize.” Basi wakamtoa Samsoni gerezani, wakamleta naye akawatumbuiza. Wakamweka katikati ya nguzo.

Shirikisha
Soma Waamuzi 16

Waamuzi 16:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Samsoni akaenda Gaza, akaona huko mwanamke kahaba, akaingia kwake. Watu wa Gaza wakaambiwa, ya kwamba, huyo Samsoni amekuja huku. Wakamzingira, wakamvizia usiku kucha, penye lango la mji, wakanyamaza kimya usiku kucha, wakisema, Na tungoje mpaka mapambazuko, ndipo tutamwua. Basi Samsoni akalala hadi usiku wa manane, akaamka katikati ya usiku, akaishika milango ya lango la mji, na miimo yake miwili, akaing'oa pamoja na komeo lake, akajitwika mabegani, akavichukua hadi katika kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni. Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila. Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja. Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali niambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe. Samsoni akamwambia, Wakinifunga kwa kamba mbichi saba ambazo hazijakauka bado, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamletea kamba mbichi saba zisizokauka, naye akamfunga nazo. Na yule mwanamke alikuwa na watu katika chumba cha ndani, wakimwotea. Basi akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Ndipo akazikata zile kamba kama vile uzi wa pamba ukatwavyo ukiguswa na moto. Basi hiyo asili ya nguvu zake haikujulikana. Delila akamwambia Samsoni, Tazama, umenidhihaki, na kuniambia uongo; sasa tafadhali, niambie, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia Wakinifunga tu kwa kamba mpya ambazo mtu hakufanya kazi nazo, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Basi Delila akatwaa kamba mpya akamfunga nazo, akamwambia, Wafilisti wanakujia, Samsoni. Na wale wenye kuotea walikuwa katika chumba cha ndani. Naye akazikata, akazitupa kutoka mikononi mwake kama uzi. Delila akamwambia Samsoni, Hata sasa umenidhihaki, umenidanganya; niambie sasa, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia, Ukivifuma hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu katika mtande wa nguo. Basi akazifunga kwa msumari, akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Naye akaamka usingizini, akaung'oa ule msumari, na ule mtande. Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi. Hatimaye, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumuudhi, roho yake ikataabika karibu kufa. Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia siri yake yote. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa BWANA amemwacha. Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakateremka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza. Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake. Kisha wakuu wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana walisema, mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu. Na hao watu walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, mungu wetu amemtia mikononi mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu. Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili.

Shirikisha
Soma Waamuzi 16

Waamuzi 16:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Samsoni akaenda Gaza, akaona huko mwanamke kahaba, akaingia kwake. Watu wa Gaza wakaambiwa, ya kwamba, huyo Samsoni amekuja huku. Wakamzingira, wakamvizia usiku kucha, penye lango la mji, wakanyamaza kimya usiku kucha, wakisema, Na tungoje mpaka mapambazuko, ndipo tutamwua. Basi Samsoni akalala hata usiku wa manane, akaondoka katikati ya usiku, akaishika milango ya lango la mji, na miimo yake miwili, akaing’oa pamoja na komeo lake, akajitwika mabegani, akavichukua hata kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni. Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila. Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja. Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali uniambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe. Samsoni akamwambia, Wakinifunga kwa kamba mbichi saba ambazo hazijakauka bado, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamletea kamba mbichi saba zisizokauka, naye akamfunga nazo. Na yule mwanamke alikuwa na watu katika chumba cha ndani, wakimwotea. Basi akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Ndipo akazikata zile kamba kama vile uzi wa pamba ukatwavyo ukiguswa na moto. Basi hiyo asili ya nguvu zake haikujulikana. Delila akamwambia Samsoni, Tazama, umenidhihaki, na kuniambia uongo; sasa tafadhali, niambie, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia Wakinifunga tu kwa kamba mpya ambazo mtu hakufanya kazi nazo, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Basi Delila akatwaa kamba mpya akamfunga nazo, akamwambia, Wafilisti wanakujia, Samsoni. Na wale wenye kuotea walikuwa katika chumba cha ndani. Naye akazikata, akazitupa kutoka mikononi mwake kama uzi. Delila akamwambia Samsoni, Hata sasa umenidhihaki, umeniambia maneno ya uongo; niambie sasa, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia, Ukivifuma hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu katika mtande wa nguo. Basi akazifunga kwa msumari, akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Naye akaamka usingizini, akaung’oa ule msumari, na ule mtande. Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi. Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa. Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa BWANA amemwacha. Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza. Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake. Kisha wakuu wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana walisema, Mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu. Na hao watu walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, Mungu wetu amemtia mikononi mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu. Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili.

Shirikisha
Soma Waamuzi 16

Waamuzi 16:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Siku moja Samsoni alienda Gaza, akamwona mwanamke kahaba, naye akaingia kwake. Watu wa Gaza wakaambiwa, “Samsoni amekuja huku!” Hivyo, wakapazingira mahali pale, nao wakamvizia usiku kucha penye lango la mji. Wakakaa kimya usiku kucha, wakiwaza, “Kutakapopambazuka, tutamuua.” Samsoni akalala tu hadi usiku wa manane. Akaamka, na kushika milango ya lango la mji, na miimo yake miwili, akaingʼoa pamoja na makomeo yake. Akaviweka mabegani mwake na kuvipeleka hadi kilele cha mlima unaokabili Hebroni. Baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika Bonde la Soreki aliyeitwa Delila. Viongozi wa Wafilisti wakamwendea yule mwanamke na kumwambia, “Mshawishi ili upate kujua siri ya nguvu zake zilizo nyingi na jinsi tutakavyoweza kumshinda ili tuweze kumfunga na kumtiisha. Kila mmoja wetu atakupa shekeli elfu moja na mia moja za fedha.” Hivyo Delila akamwambia Samsoni, “Naomba uniambie siri ya hizi nguvu zako nyingi, na jinsi unavyoweza kufungwa ili kukutiisha.” Samsoni akamjibu, “Kama nikifungwa kwa kamba saba za upinde ambazo hazijakauka, hapo ndipo nitakapokuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.” Basi viongozi wa Wafilisti wakamletea yule mwanamke kamba saba za upinde ambazo hazijakauka, naye akamfunga Samsoni. Wakati watu wakiwa wanamvizia katika chumba cha ndani, yule mwanamke akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Lakini yeye akazikata zile kamba za upinde, kama vile uzi wa pamba unapoguswa na moto. Hivyo siri ya nguvu zake haikujulikana. Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Tafadhali niambie unaweza kufungwa kwa kitu gani?” Akamwambia, “Kama nikifungwa kwa uthabiti kwa kamba mpya ambazo hazijatumika, basi nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.” Hivyo, Delila akachukua kamba mpya na kumfunga nazo. Kisha akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Wale watu waliokuwa wanamvizia walikuwa katika chumba cha ndani. Lakini akazikata zile kamba zilizokuwa zimefunga mikono yake kama nyuzi. Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Hata sasa umenifanyia mzaha na kuniambia uongo. Nieleze ni jinsi gani unavyoweza kufungwa.” Samsoni akamwambia, “Kama ukivifuma hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu kwa nguo iliyo katika mtande, na kuukaza kwa msumari, ndipo nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote.” Hivyo, Samsoni alipokuwa amelala, Delila akachukua vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake na kuvifuma pamoja na nguo kwenye mtande, na kuukaza kwa msumari. Kisha akamwambia, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” Samsoni akaamka kutoka usingizini na kungʼoa msumari na mtande, pamoja na ile nguo. Ndipo Delila akamwambia, “Wawezaje kusema, ‘Nakupenda,’ wakati moyo wako haupo pamoja nami? Umenifanyia mzaha mara hizi tatu na hujaniambia siri ya hizi nguvu zako nyingi.” Hatimaye, baada ya kusumbuliwa kwa maneno kwa siku nyingi na kuudhiwa, roho yake ikataabika kiasi cha kufa. Hivyo, akamwambia yule mwanamke siri yake yote, akisema, “Wembe haujapita kamwe kichwani mwangu, kwa kuwa mimi ni Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yangu. Kama nywele za kichwa changu zikinyolewa, nguvu zangu zitanitoka, na nitakuwa dhaifu kama mtu mwingine yeyote!” Delila alipoona kuwa amemweleza siri yake yote, akatuma ujumbe kwa viongozi wa Wafilisti na kusema, “Njooni tena mara nyingine, maana amenieleza siri yake yote.” Basi viongozi wa Wafilisti wakarudi kwa Delila, wakiwa na fedha mikononi mwao. Delila akamfanya alale usingizi magotini pake, akamwita mtu amnyoe vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake. Delila akaanza kumnyongʼonyesha Samsoni, nazo nguvu zake zikamtoka. Yule mwanamke akamwita, “Samsoni! Hao, Wafilisti wanakujia!” Akaamka toka usingizini, akisema, “Nitatoka nje kama hapo awali; nitajinyoosha, niwe huru.” Lakini hakujua kwamba BWANA alikuwa amemwacha. Basi Wafilisti wakamkamata, wakamngʼoa macho yake, wakamteremsha hadi Gaza. Wakamfunga kwa pingu za shaba, wakamweka gerezani ili asage ngano. Wakati huo nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa. Basi viongozi wa Wafilisti wakakusanyika pamoja ili kutoa kafara kuu kwa mungu wao Dagoni, wakisherehekea na kusema, “Mungu wetu amemtia adui yetu Samsoni mikononi mwetu.” Watu walipomwona Samsoni wakamsifu mungu wao, wakisema: “Sasa mungu wetu amemtia adui yetu mikononi mwetu, yule aliyeharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.” Mioyo yao ilipokuwa imefurahishwa, wakapaza sauti, wakisema, “Mleteni Samsoni aje ili atutumbuize.” Basi wakamleta Samsoni kutoka gerezani, naye akawatumbuiza. Wakamsimamisha katikati ya nguzo mbili.

Shirikisha
Soma Waamuzi 16