Waamuzi 15:1-20
Waamuzi 15:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya muda fulani, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni alichukua mwanambuzi, akaenda kumtembelea mkewe. Akamwambia baba mkwe wake kwamba anataka kumwona mke wake chumbani mwake. Lakini baba mkwe hakumruhusu, akamwambia, “Mimi nilidhani ulimchukia kabisa. Kwa hiyo nilimwoza rafiki yako. Hata hivyo, dada yake mdogo ni mzuri kuliko yeye. Tafadhali, umwoe huyo badala yake.” Samsoni akamwambia, “Safari hii sitakuwa na lawama kwa yale nitakayowatendea Wafilisti.” Basi, Samsoni akaenda, akawakamata mbweha 300 na akawafunga mikia yao pamoja wawiliwawili. Kisha akaweka mwenge katika kila jozi ya mbweha. Halafu akaiwasha hiyo mienge na kuwaachilia hao mbweha ambao waliingia kwenye mashamba ya Wafilisti na kuteketeza miganda ya ngano na pia ngano iliyokuwa bado haijavunwa hata na mashamba ya mizeituni. Wafilisti walipotaka kujua aliyefanya hayo, waliambiwa, “Ni huyo Samsoni, mkwewe Mtimna, amefanya hivyo kwa sababu huyo baba mkwe wake amemchukua mke wake na kumwoza kwa kijana mmoja aliyekuwa mdhamini wake mwenyewe Samsoni katika harusi.” Basi Wafilisti wakaenda kumchoma moto yule mwanamke pamoja na baba yake. Samsoni akawaambia hao Wafilisti, “Kama hayo ndiyo mliyoyafanya, naapa kwamba sitaondoka mpaka nimelipiza kisasi.” Basi, akawashambulia vikali na kuwaua wengi. Kisha akaenda kuishi katika pango la mwamba wa Etamu. Wafilisti wakaja, wakapiga kambi yao nchini Yuda na kuushambulia mji wa Lehi. Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kutushambulia?” Nao wakawajibu, “Tumekuja ili tumfunge Samsoni na kumtendea kama alivyotutendea.” Basi, watu 3,000 wa Yuda wakamwendea Samsoni pangoni mwa mwamba wa Etamu wakamwambia, “Je, hujui kwamba Wafilisti wanatawala juu yetu? Tazama basi, mkosi uliotutendea!” Samsoni akawajibu, “Kama walivyonitendea ndivyo nilivyowatendea.” Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga ili tukutie mikononi mwao.” Samsoni akawaambia, “Niapieni kwamba nyinyi wenyewe hamtaniua.” Nao wakamwambia, “Sisi hatutakuua ila tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi, wakamfunga kwa kamba mbili mpya na kumtoa humo pangoni. Alipofika Lehi, Wafilisti walimwendea mbio huku wakipiga kelele. Ghafla roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Samsoni kwa nguvu na zile kamba walizomfunga mikononi mwake zikakatika kama kitani kilichoshika moto, navyo vifungo vikaanguka chini. Samsoni akapata utaya mbichi wa punda, akautumia kuwaua watu 1,000. Kisha Samsoni akasema, “Kwa utaya wa punda, nimeua watu elfu moja. Kwa utaya wa punda, nimekusanya marundo ya maiti.” Alipomaliza kusema, akatupa utaya huo. Mahali hapo pakaitwa Ramath-lehi, yaani mlima wa utaya. Kisha Samsoni akashikwa na kiu sana. Basi, akamwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Ee Mungu, wewe ndiwe uliyeleta ukombozi huu, kwa kunitumia mimi mtumishi wako. Je, sasa utaniacha nife kwa kiu na kutekwa na Wafilisti hawa wasiotahiriwa?” Mungu akafungua mahali palipokuwa na shimo huko Leki, akatiririsha maji. Samsoni akanywa maji hayo na nguvu zake zikamrudia. Chemchemi hiyo ikaitwa En-hakore; nayo iko huko Lehi mpaka leo. Samsoni alikuwa mwamuzi wa Waisraeli kwa miaka ishirini, nyakati za Wafilisti.
Waamuzi 15:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini ikawa baadaye, wakati wa mavuno ya ngano Samsoni akaenda kumtazama mkewe, akamchukulia mwana-mbuzi; akasema, Nitaingia chumbani kwa mke wangu. Lakini baba yake mwanamke hakumwacha kuingia. Baba yake akasema, Hakika mimi nilidhani ya kuwa umemchukia kabisa; basi nilimpa rafiki yako. Je! Si dada yake mdogo ni mzuri kuliko yeye? Tafadhali, mtwae huyo badala yake. Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia kwa hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru. Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa mienge ya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia mwenge kati ya kila mikia miwili. Alipokwisha kuiwasha moto ile mienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni. Ndipo Wafilisti wakasema, Ni nani aliyetenda hivi? Wakasema, Ni huyo Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu alimchukua mkewe akampa mwenzake. Wafilisti wakaenda wakamteketeza yeye na baba yake kwa moto. Samsoni akawaambia, Ikiwa ninyi mnafanya mambo kama hayo, hakika sitakoma hadi nitakapojilipizia kisasi juu yenu. Ndipo akawashambulia vikali na kuwaua wengi, kisha akateremka na kukaa katika ufa wa jabali la Etamu. Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakashambulia Lehi. Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi. Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakateremka hadi katika ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao. Wakamwambia, Tumeshuka ili kukufunga, tupate kukutia katika mikono ya Wafilisti. Samsoni akawaambia, Niapieni ya kwamba ninyi wenyewe hamtaniua. Wakamwambia, wakisema, Vema, lakini tutakufunga sana, na kukutia katika mikono yao; lakini hakika hatutakuua. Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakamchukua kutoka huko jabalini. Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo Roho ya BWANA ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akaua watu elfu moja kwa mfupa huo; Samsoni akasema, Kwa taya ya punda, chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda nimeua watu elfu moja. Ikawa, alipokuwa amekwisha kunena akautupa ule mfupa wa taya mkononi mwake; na mahali pale pakaitwa Ramath-lehi. Kisha akaona kiu sana, akamwita BWANA akasema, Wewe umetupa wokovu huu kwa mkono wa mtumishi wako; na sasa nitakufa kwa kiu, na kuanguka katika mikono ya watu wasiotahiriwa. Lakini Mungu akapasua mahali penye shimo palipo katika Lehi, pakatoka maji; naye alipokunywa, roho yake ikamrudia, akaburudika; kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Enhakore, napo pa katika Lehi hata hivi leo. Naye akawa mwamuzi wa Israeli: katika siku za Wafilisti muda wa miaka ishirini.
Waamuzi 15:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini ikawa baadaye, wakati wa mavuno ya ngano Samsoni akaenda kumtazama mkewe, akamchukulia mwana-mbuzi; akasema, Nitaingia chumbani kwa mke wangu. Lakini baba yake mwanamke hakumwacha kuingia. Baba yake akasema, Hakika mimi nalidhani ya kuwa umemchukia kabisa; basi nalimpa rafiki yako. Je! Ndugu yake mdogo mzuri kuliko yeye? Tafadhali, mtwae huyo badala yake. Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru. Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili. Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni. Ndipo Wafilisti wakasema, Ni nani aliyetenda hivi? Wakasema, Ni huyo Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu alimchukua mkewe akampa mwenzake. Wafilisti wakaenda wakamteketeza yeye na baba yake kwa moto. Samsoni akawaambia, Ikiwa ninyi mnafanya mambo kama hayo, hakika nitajilipiza kisasi juu yenu, na baadaye nitakoma. Akawapiga upeo, mapigo makuu sana, kisha akatelemka akakaa katika ufa wa jabali la Etamu. Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakajieneza katika Lehi. Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi. Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakatelemka hata ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao. Wakamwambia, Tumeshuka ili kukufunga, tupate kukutia katika mikono ya Wafilisti. Samsoni akawaambia, Niapieni ya kwamba ninyi wenyewe hamtaniangukia. Wakamwambia, wakisema, Vema, lakini tutakufunga sana, na kukutia katika mikono yao; lakini hakika hatutakuua. Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakamchukua kutoka huko jabalini. Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya BWANA ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo; Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu. Ikawa, alipokuwa amekwisha kunena akautupa ule mfupa wa taya mkononi mwake; na mahali pale pakaitwa Ramath-lehi. Kisha akaona kiu sana, akamwita BWANA akasema, Wewe umetupa wokovu huu kwa mkono wa mtumishi wako; na sasa nitakufa kwa kiu, na kuanguka katika mikono ya watu wasiotahiriwa. Lakini Mungu akapasua mahali penye shimo palipo katika Lehi, pakatoka maji; naye alipokwisha kunywa, roho yake ikamrudia, akaburudika; kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Enhakore, napo pa katika Lehi hata hivi leo. Naye akawa mwamuzi wa Israeli: katika siku za Wafilisti muda wa miaka ishirini.
Waamuzi 15:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya kitambo kidogo, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni akachukua mwana-mbuzi, kwenda kumzuru mkewe. Akasema, “Nataka kuingia chumbani kwa mke wangu.” Lakini baba yake huyo mwanamke hakumruhusu kuingia. Baba mkwe wake akamwambia, “Nilikuwa na hakika kwamba ulimchukia, hivyo nikampeana kwa rafiki yako. Je, dada yake mdogo si mzuri kuliko yeye? Mchukue huyo badala yake.” Samsoni akawaambia, “Wakati huu, nitakapowadhuru Wafilisti, sitakuwa na lawama.” Hivyo Samsoni akaondoka na kuwakamata mbweha mia tatu, akawafunga wawili wawili, mikia kwa mikia. Kisha akafungia mwenge wa moto kwenye kila jozi la mikia hiyo. Akawasha ile mienge na kuwaachia wale mbweha katika mashamba ya Wafilisti ya nafaka zilizosimamishwa katika matita. Akateketeza matita ya nafaka, pamoja na mashamba ya mizabibu na mashamba ya mizeituni. Wafilisti walipouliza, “Ni nani aliyetenda jambo hili?” Wakaambiwa, “Ni Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu mkewe alipeanwa kwa rafiki yake.” Hivyo Wafilisti wakapanda, wakamteketeza kwa moto yeye huyo mwanamke pamoja na baba yake. Samsoni akawaambia, “Kwa kuwa mmetenda hivyo, hakika sitatulia hadi niwe nimelipiza kisasi juu yenu.” Akawashambulia kwa ukali na kuwaua watu wengi sana. Kisha akateremka na kukaa kwenye pango katika mwamba wa Etamu. Wafilisti wakapanda na kupiga kambi huko Yuda na kuenea huko Lehi. Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kupigana nasi?” Wakawajibu, “Tumekuja ili kumkamata Samsoni na kumtenda kama alivyotutendea.” Ndipo watu elfu tatu wa Yuda waliteremka hadi kwenye pango katika mwamba wa Etamu, wakamwambia Samsoni, “Je, hujatambua kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hiki ulichotutendea?” Akawajibu, “Nimewatendea tu kile walichonitendea.” Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga na kukutia mikononi mwa Wafilisti.” Samsoni akawaambia, “Niapieni kuwa hamtaniua ninyi wenyewe.” Wakamjibu, “Sisi hatutakuua, bali tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya na kumchukua toka huko kwenye pango katika mwamba. Alipokaribia Lehi, Wafilisti wakamjia wakipiga kelele. Roho wa BWANA akaja juu yake kwa nguvu. Kamba zilizomfunga mikono zikawa kama kitani iliyochomwa kwa moto, na vifungo vyake vikaanguka chini toka mikononi mwake. Ndipo akaona mfupa mpya wa taya la punda, akanyoosha mkono, akauchukua na kuua nao Wafilisti wapatao elfu moja. Ndipo Samsoni akasema, “Kwa taya la punda malundo juu ya lundo, kwa taya la punda nimeua watu elfu moja.” Alipomaliza kusema, akautupa ule mfupa wa taya; na mahali pale pakaitwa Ramath-Lehi. Kwa kuwa alihisi kiu sana, akamlilia BWANA, akisema, “Umempa mtumishi wako ushindi huu mkuu. Je, sasa nife kwa kiu na kuangukia mikononi mwa hawa watu wasiotahiriwa?” Ndipo Mungu akafunua shimo huko Lehi, na maji yakatoka. Samsoni alipoyanywa maji hayo, nguvu zikamrudia, akahuika. Hivyo chemchemi ile ikaitwa En-Hakore, nayo iko hadi leo huko Lehi. Samsoni akawa mwamuzi wa Waisraeli katika siku za Wafilisti kwa muda wa miaka ishirini.